DENI la Sh 2,000 limetosha kumaliza uhai wa mpiga debe maarufu wa
stendi ya mabasi yaendeayo mikoani ya mjini Iringa, Samwel Yengayenga
baada ya kuchomwa kisu mara mbili katika eneo la mgongoni na kifuani.
Tukio
hilo la kinyama limetokea jana majira ya saa 6.55 mchana baada ya
Yengayenga na mtuhumiwa wa mauaji yake aliyekuwa akidai kiasi hicho cha
fedha kurushiana maneno makali na kisha kupigana.
Akithibitisha
kutokea kwa tukio hilo, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa, Ramadhani
Mungi alimtaja mtuhumiwa huyo kuwa ni Festo Ruben Mkalala (26), muosha
magari, mkazi wa mjini Iringa ambaye alikamatwa mara baada ya kufanya
tukio hilo.
Mungi alisema Yengayenga, Mkalala
na mtu mwingine wa tatu (hakumtaja jina) wanadaiwa siku nne zilizopita
waliosha basi la Kimotco linalofanya safari zake kati ya Iringa na
Arusha.
“Stahiki ya kazi hiyo ilikuwa Sh 15,000; hata hivyo hawakulipwa fedha hizo baada ya kumaliza kazi hiyo,” alisema.
Alisema
siku iliyofuata Mkalala na kijana huyo mwingine waliyefanya naye kazi
walikwenda kuchukua ujira wao na kugawana Sh 5,000 kila mmoja huku
Mkalala akiahidi kutunza Sh 5,000 za Yengayenga mpaka watakapokutana.
Walipokuta,
RPC alisema Mkalala alimpa Yengayenga Sh 3,000 badala ya Sh 5,000 na
kuahidi kummalizia kiasi kilichobaki kesho yake.
Kitendo
hicho kwa mujibu wa mashuhuda kinadaiwa kumchukiza Yengayenga aliyeamua
kunyanganya simu ya Mkalala mpaka amaliziwe Sh2,000 zake zilizobaki.
Kamanda Mungi alisema Mkalala alichukizwa na uamuzi huo na kuanzisha ugomvi uliopeleka kifo cha Yengayenga.
“Uchunguzi
wa awali unaonesha Mkalala aliamua kupigana na Yengayenga ili
arudishiwe simu yake na alipozidiwa alikimbia kusikojulikana na kurudi
akiwa na kisu mkononi,” alisema.
Ili kuipata
simu yake, Kamanda Mungi alisema ushahidi wa awali unaonesha Mkalala
alitumia kisu hicho kumchoma mgongoni na kifuani Yengayenga na
kusababisha mauti yake.
Yengayenga alikufa papo
hapo katika tukio ambalo mtuhumiwa huyo alikamatwa na kufikishwa kituo
cha Polisi cha kati cha mjini Iringa.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇