LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Jul 7, 2014

MAKAMU WA RAIS DKT. BILAL AIWAKILISHA TANZANIA KATIKA SHEREHE ZA MAADHIMISHO YA MIAKA 50 YA UHURU WA MALAWI


  Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Mohammed Gharib Bilal akiagana na Rais wa Malawi, Profesa Arthur Peter Mutharika, baada ya shughuli za maadhimisho ya Sherehe ya miaka 50 ya uhuru wa Malawi kukamilika katika uwanja wa Civo, jana Julai 06, 2014. Nyuma yake ni Mama Asha Bilal. Picha na OMR

 Wa pili (kushoto) ni Rais wa Zimbabwe, Robert Mugabe, Rais wa Malawi 
Profesa Arthur Mutharika akifuatiwa na mkewe, Mheshimiwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Mohammed Gharib Bilal, Mama Asha Bilal na viongozi wengine wakifuatilia sala maalum ya kuombea nchi ya Malawi wakati wa sherehe za miaka 50 ya uhuru wa nchi hiyo zilizofanyika jana Jumapili Julai 06, 2014 katika uwanja wa Civo jijini Lilongwe, Malawi. Picha na OMR

  Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Mohammed Gharib Bilal akiongozana na Mwenyeji wake Makamu wa Rais wa Malawi Saulos Klaus Chilima kukagua gwaride maalum la makaribisho kwa Mheshimiwa Makamu wa Rais wa Tanzania baada ya kuwasili kwenye uwanja wa Ndege wa Lilongwe kwa ajili ya kuhudhuria sherehe za miaka 50 ya uhuru wa Malawi zilizofanyika Jumapili tarehe Julai 06,  2014. Picha na OMR

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na mwenyeji wake 
Makamu wa Rais wa Malawi, Saulos Klaus Chilima, wakifurahia ngoma za asili 
za Malawi, wakati wa mapokezi kwenye Uwanja wa Lilongwe, alipowasili kuhudhuria sherehe za miaka 50 ya uhuru wa Malawi zilizofanyika Jumapili tarehe Julai 06,  2014. Picha na OMR

MAKAMU WA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA AIWAKILISHA TANZANIA KATIKA MAADHIMISHO YA MIAKA 50 YA UHURU WA MALAWI
Julai 06, 2014 Lilongwe

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Mohammed Gharib 
Bilal, leo Jumapili Julai 06, 2014 ameiwakilisha Tanzania katika maadhimisho ya miaka 50 ya Uhuru wa Malawi, sherehe zilizofanyika katika 
Uwanja wa Civo jijini Lilongwe.

Katika sherehe hizo pamoja na Makamu wa Rais wa Tanzania, pia alihudhuria 
Rais wa Zimbabwe Robert Mugabe, Waziri Mkuu wa Msumbiji na viongozi 
mbalimbali waliowakilisha nchi kutoka Afrika.

Sherehe hizo zilianza kwa ibada ya misa asubuhi na kisha kuhamia katika 
uwanja wa Civo mchana ambapo Rais wa Malawi Prof. Athur Peter Mutharika  
alikagua gwaride na kisha kuwasha Mwenye wa Jubilee ya miaka 50 na baadaye 
kulihutubia taifa.

Akizungumza katika sherehe hizo, Rais Mutharika alisisitiza kuhusu umuhimu 
wananchi wa Malawi kuwa wamoja na akaeleza nia yake ya kujenga umoja kwa 
nchi zinazoizunguka Malawi pamoja na zile za Kusini mwa Afrika. Baada ya 
hotuba hiyo, sherehe hizo ziliendelea na mchezo wa soka baina ya timu ya taifa ya Malawi na Msumbiji.

Malawi ilipata uhuru wake mwaka 1984 ikiongozwa na Rais wake wa kwanza Dkt. Kamuzu Banda hadi mwaka 1994. Baada ya mwaka huo alifuata Rais Dkt. Bakili 
Muluzi aliyetawala kuanzia mwaka 1994 hadi 2004. 

Baaada ya mwaka huo alifuata Rais Profesa Bingu wa Mutharika aliyetawala hadi mauti yalipomkuta mwaka 2012. Dkt. Joyce Banda aliyekuwa Makamu wa Rais wa Mutharika alichukua madaraka na kukaa hadi mwaka huu 2014 ambapo Malawi iliingia katika uchaguzi mkuu na kisha Rais Profesa Arthur Peter Mutharika aliposhinda uchaguzi huo na hivyo kuwa Rais wa nne wa Malawi.

Katika sherehe hizo Mheshimiwa Makamu wa Rais pia alifuatana na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Mheshimiwa Mahadhi Juma Maalim na Mheshimiwa Makamu wa Rais amerejea nyumbani Tanzania Julai 07, 2014 tayari kuendelea na majukumu mengine ya kitaifa.

Imetolewa na: Ofisi ya Makamu wa Rais
Julai 06, 2014 Lilongwe: Malawi

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages