Martin Kobler akizungumza |
Hayo yameelezwa siku ya jana, Mwakilishi wa Katibu Mkuu katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Mkuu wa Misheni ya Kulinda Amani katika DRC, ( MONUSCO), Martin Kobler
Alikuwa akiwasilisha mbele ya Baraza Kuu la Usalama la Umoja wa Mataifa, taarifa ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Misheni ya Kulinda Amani ya Umoja wa Mataifa katika DRC ( MONUSCO).
“Tunazo taarifa za uhakika kabisa kwamba kundi hili la M23 baada ya kusambaratishwa vibaya mwezi Novemba mwaka jana, sasa limeanza kujiunda na kujipanga upya” akasema Bw. Kobler na kuongeza, “ Ninapenda kutumia nafasi hii, kuitaka Serikali ya DRC kuanza kutekeleza makubaliano ya Nairobi.
Na kwa nchi za Uganda na Rwanda kutoruhusu ardhi yao kutumiwa na kundi la M23 iwe ni kujipanga upya au kwa mafunzo ya aina yoyote ”.
Mbali ya Mkuu wa MONUSCO kutoa taarifa yake kwa Baraza hilo, Mjumbe Maalum wa Katibu Mkuu katika eneo la Maziwa Makuu, Bi. Mary Robinson naye aliwasilisha taarifa yake.
Mkuu huyo wa Misheni ya MONUSCO alieleza bayana kwamba makundi ya waasi katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo bado ni tishio kubwa katika mchakato mzima wa utafutaji wa Amani ya kudumu katika DRC na hususani katika eneo la Mashariki ya nchi hiyo.
“Uwepo wa Brigedi Maalum ( FIB) na matumizi ya ndege zisizoendeshwa na binadamu ( UAVs), makundi yote ya waasi yanajua wazi kwamba, sasa tuna nia na uwezo wa kutumia nguvu kubwa wakati wowote”. Akasisitiza Mkuu huyo wa MONUSCO.
Katika taarifa yake kwa Baraza Kuu la Usalama, Bw. Kobler ,alielezea kwa kina hali ya usalama ilivyo nchini DRC na kazi kubwa inayofanywa na MONUSCO katika kuyakabili makundi ya waasi na vilevile kutoa ulinzi kwa raia.
Bw. Kobler alibainisha zaidi kwa kusema kuwa,“ Katika wiki zijazo, tutakuwa tumekamilisha mapitio ya mkao wa kijeshi katika eneo lote la Mashariki ya Kongo. Baada ya kukamilisha kazi hiyo tutakuwa na urahisi wa kwenda mahali popote na wakati wowote tunapohitajika, kukabiliana na tishio la aina yoyote na kutoa ulinzi kwa raia “
Naye Bi. Mary Robinson, Mjumbe Maalum wa Katibu Mkuu katika eneo la Maziwa Makuu, akizungumza kwa njia ya video tele-conferencing kutokea Kishansa DRC, ameliambia Baraza Kuu la Usalama, kwamba wakati umefika sasa kwa nchi zile zilizotia saini Mpango Mpana wa Umoja wa Mataifa kuhusu Siasa, Usalama na Maendeleo katika DRC na Maziwa Makuu kuanza kutekeleza maamuzi magumu.
Akasema juhudi za kutafuta Amani na usalama katika DRC zipo katika kipindi muhimu hivi sasa na kutoa wito kwa viongozi waliosaini mpango huo kuanza kutelekeza ahadi zao ili hatimaye Amani iweze kupatikana.
Bi. Robinson ambaye kesho ( Jumanne) atahudhuria mkutano wa Wakuu wa Nchi za Maziwa Makuu ( ICGLR)utakaofanyika nchini Rwanda alieleza pia kwamba, mazingira ya utulivu yaliyokuwapo baada ya kusambaratishwa kundi la M23 yamepotea na kwamba eneo hilo sasa lipo katika kipindi cha kurejea kwa machafuko.
Akasema utulivu huo umetoweka hasa baada ya kutokea kwa mashambulizi yaliyofanywa na kundi la waasi la Alliend Democratic Forces ( ADF) katika eneo la Mashariki ya DRC.
Aidha kuendelea kwa hali ya machafuko katika Jamhuri ya Afrika ya Kati na kuibuka kwa mapigano katika Sudan ya Kusini, pia kumechangia kuwepo mdororo huo wa kiusalama mashariki ya DRC.
Na kwa sababu hiyo anasema, utekelezaji wa mpango mpana wa kisiasa bado unabaki kuwa suluhu pekee ya upatikanaji wa Amani ya kudumu, usalama, ushirikiano na maendeleo katika eneo la Maziwa Makuu.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇