NA BASHIR NKOROMO, MUFINDI
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimetaka uwekwe utaratibu maalum utakaowezesha wapasuaji mbao wadogo katika wilaya Mufindi mkoani Iringa, nao kupewa vibali vya kupasua mbao katika msitu wa Sao Hill, wilayani humo.
Ili kuwepo utaratibu huo kimeagiza Mkuu wa wilaya hiyo na Baraza la madiwani, kukutana na wapasuaji mbao hao wadogo ili yapatikane mapendekezo ya pamoja ya namna gani nzuri itakayowezesha wapasuaji hao kupatiwa vitalu, kisha mapendekezo yatapelekwa wizara ya Maliasili na Utalii.
Akizungumza kwenye mkutano wa hadhara katika Uwanja wa Mashujaa, katika mji mdogo wa Mafinga wilayani humo, Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa, CCM, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye alisema, hatua hiyo itawafanya wakataji mbao hao wadogo kunufaika na rasilimali hiyo ya misitu na pia kupewa fursa ya kuchangia maendeleo ya wilaya hiyo.
Nape alisema, kutokana na utaratibu wa sasa unaowapendelea kuwapa vitalu vya kukata mbao wenye mashine kubwa tu, wakataji wadogo wa mbao ndio wengi wanaoishi wilayani humo wamekuwa wakibaki kuhangaika na kuishi maisha ya kubahatisha wakati wao ndio watunzaji wakubwa wa mistu ya Sao Hill.
"Hawa wakata mbao wadogo kimsingi ndio walinzi wakubwa wa misitu hii tofauti na wakataji wakubwa ambao wengi wao wanatoka nje ya wilaya, wakishakata mbao zao wanaondoka", alisema Nape.
" Wakataji hawa wadogo wakishapata fedha watazitumia hapa hapa Mafinga, lakini hao wakataji wakubwa wataondoka nazo na kuuacha uchumi wa hapa ukiendelea kudorora" alisema Nape.
Nape aliahidi kuwa mstari wa ambele kama kiongozi wa ngazi ya Juu ya Cgama tawala, kufuatilia kwa karibu ili kuhakikisha mapendekezo yatakayokuwa yamepelekwa wizarani yanapatiwa majibu mapema.
Nape alisema, CCM inapswa kuwatetea wakataji mbao wadogo kwa sababu ndicho Chama ambacho tangu kuanzishwa kwake kimekuwa kikijipambanua kuwa ndicho chamacha kutetea wanyonge, hivyo kinapoiagiza serikali kuwahudumia wanyonge hakijipendekezi ila kinatimiza wajibu wake.
Katika hatua nyingine, Nape amewaagiza wabunge wa CCM, kuhakikisha wanapigania kwenye kikao cha bajeti cha bunge linaloendelea mjini Dodoma kuhakikisha bajeti inayotengwa kwa ajili ya pembejeo za kilimo inakuwa kubwa.
Nape alisema, anao uhakika kwamba, kama wabunge wa CCM watasimama kidete katika kupiganaia kupanda kwa bajeti ya kilimo watafanikiwa kwa sababu ndio wengi zaidi bungeni kuliko wale wa upinzani. " Ninyi wabunge wa CCM ni wengi kuliko wa upinzani, hakikisheni mnasimama kidete bungeni ili bajeti ya fedha kwa ajili ya kilimo iwe kubwa zaidi kwa ajili ya kuinua hali ya kilimo nchini", alisema Nape.
Alizungumzia kuhusu CCM kuwa mtetezi mkubwa wa wanyonye na rasilimali za nchi, alisema hiyo imekuwa ndiyo sera yake tangu ilipoanzishwa, lakini imekuwa utekelezaji wake hauonekani vizuri kutokana na kelegalelega kwa baadhi ya viongozi katika usimamizi.
Nape alisema kutokana na kutambua hivyo ndiyo sababu Chama kimeamua kufanya mageuzi makubwa ndani ya Chama katika masuala mbalimbali ili kuhakikisha kila kiongozi anawajibika katika kulinda na kutetea rasilimali za nhi na maslahi ya wanyonge.
"Kuna watu wanapita pita hapa kujinadi eti wao ndio wameanzisha harakatiza kutetea rasilimali za nchi na maslahi ya wanyonge hapa nchini, hawa wapuuuzeni ni waongo wakubwa. Sisi CCM tumekuwa na msimamo huu tangu enzi za TANU kwa hiyo watu hao kujinadi kuwa ni waasisi ni kuwafanya hamjui historia ya nchi hii", alisema.
Akizungumzia uchaguzu unaondelea ndani ya Chama, Nape alisisitiza msimamo wa Chama kwamba ni marufuku mtu yeyote anayetafuta uongozi kutumia rushwa, na kwamba atakayebainika ataondolewa jina lake na kuzuiwa na Kamati Kuu kugombea kwa muda itakaoona unafaa.
"Nawahakikishieni wana CCM na wananchi kwa jumla, kwamba katika hili hatutanii, na anayedhani kwamba tunatania ajaribu atauona moto wake, tumejipanga kuhkikisha baada ya uchaguzi huu chama kitapata viongozi bora na waadilifu watakaotuvusha kwa kishindo katika uchaguzi Mkuu wa 2015", alisema na kuongeza;
"Hakika nawaambieni baada ya uchaguzi huu, Chama Cha Mapinduzi kitakuwa chama bora kuliko chama chochote Afrika na pengine duniani kote kuliko wakati wowote".
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇