Na Roida Andusamile-TBS
Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara Prof. Riziki Shemdoe amewataka watumishi wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), kuepuka vishawishi na urasimu katika utendaji kazi zao ili nchi iwe salama na kuvutia wawekezaji zaidi.
Prof. Shemdoe aliyasema hayo hivi karibuni alipotembelea TBS kwa mara ya kwanza baada ya kuteuliwa na Rais Dk. John Magufuli kuwa Katibu Mkuu wa Wizara hiyo na kufafanua kuwa ili kuwezesha biashara TBS inapaswa kufanya kazi kwa uadilifu na kuepuka urasimu ambao unakwamisha biashara na kukatisha tamaa wawekezaji wapya.
“Tunapaswa kushirikiana katika utendaji kazi na kufanya kazi kwa ufanisi zaidi kwa manufaa ya taifa,” alisisitiza Prof. Shemdoe na kuongeza kuwa kwa sasa Tanzania iko nafasi ya 141 Duniani katika urahisi wa ufanyaji wa biashara hivyo jitihada zaidi zinahitajika ili kuwa katika nafasi nzuri zaidi na kuongeza kuwa Wizara ya Viwanda na Biashara ndiyo inayotekeleza Blue Print kwa kuhakikisha kuwa vikwazo vyote vya kibiashara vinaondolewa na kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji na biashara.
Mapemai Mkurugenzi Mkuu wa TBS, Dk. Athuman Ngenya akimkaribisha Katibu Mkuu aliyeambatana na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Ludovick Nduhiye, alimhakikishia Katibu Mkuu kuwa Shirika hilo litaendelea kufanyakazi katika kiwango kinachotakiwa licha ya kukabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ukosefu wa vifaa vya kisasa vya maabara ili kwenda sanjari na maendeleo ya sayansi na teknolojia.
Dkt. Ngenya alisema Shirika limeendelea kujizatiti katika kuhakikisha kuwa soko la Tanzania linakuwa na bidhaa bora pekee ikiwa ni pamoja na kuendelea kufungua ofisi mipakani na Kanda, ambazo zinatoa huduma kwa haraka tofauti na ilivyokuwa hapo awali ambapo huduma za TBS zilikuwa zinapatikana Dar es Salaam pekee.
Alisema Desemba mwaka jana TBS ilifungua ofisi mpya ya Kanda ya Magharibi mkoani Kagera ambayo kwa sasa inahudumia mikoa ya Kigoma, Katavi na Rukwa na kwamba kufunguliwa kwa kanda ya Magharibi kumefanya idadi ya Kanda kwa sasa kufikia sita.
Alizitaja kanda zingine zenye ofisi kuwa ni ya Kati Dodoma (Dodoma, Singida na Tabora), Nyanda za Juu Kusini Mbeya (Mbeya, Iringa, Njombe, na Songwe), Kanda ya Kusini Mtwara (Mtwara,Lindi na Ruvuma) Kanda ya Kaskazini Arusha(Arusha, Kilimanjaro, Manyara na Tanga na Kanda ya Ziwa Mwanza (Mwanza, Kagera, Mara, Geita, Simiyu na Shinyanga).
Dk. Ngenya alisema pia TBS imefungua ofisi katika viwanja vya ndege vya Kilimanjaro, Dar es Salaam na Mwanza na katika Bandari za Mwanza, Tanga, Dar es Salaam na Bagamoyo na kutaja ofisi za mipakani kuwa ni pamoja na Rusumo, Kabanga, Kasumulo,Tunduma, Holili, Horohoro, Namanga, Sirari, Mutukula, Tarakea na Mtambaaswala.
Katibu Mkuu wa Wizara
ya Viwanda na Biashara Prof. Riziki
Shemdoe (katikati) akiwa na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS) Dk. Athuman Ngenya na Watendaji wengine wa Shirika hilo, baada ya ziara yakehivi karibuni. (Picha na TBS)
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇