Sea Breeze, Kunduchi
Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Dar es Salaam, Cde Stanley Mkandawire, kwa niaba ya Katibu Mkuu wa CCM Dk. Asha-Rose Migiro, amemtembelea kumjua hali, Mjumbe wa Kamati Kuu ya kwanza ya CCM, chini ya Mwenyekiti wa kwanza wa Chama, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Bi Hindu Lilla, nyumbani kwake, Sea Breeze, Kunduchi Jijini Dar es Salaam, leo Novemba 18, 2026.
Pamoja na Hindu, Kamati Kuu ya kwanza ya CCM ilikuwa na viongozi wakuu wa chama na serikali kutoka pande zote mbili za Muungano. Baadhi ya viongozi na wajumbe muhimu waliokuwa sehemu ya uongozi na Kamati Kuu wakati huo walikuwa ni Julius Kambarage Nyerere – Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Aboud Jumbe Mwinyi – Makamu Mwenyekiti wa CCM (Zanzibar) na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Tanzania, Rashidi Mfaume Kawawa – Kiongozi Mwandamizi na Waziri Mkuu/Makamu wa Pili wa Rais wa wakati huo, Pius Msekwa – Katibu Mkuu wa kwanza wa CCM (1977–1981).
Akizungumza, Bi Hindu, amewambia Cde Mkandawire kuwa ni muhimu sana Chama kuhuisha mashina yake kama ilivyokuwa zamani, ikiwemo kuhakikisha vinafanyika vikao vya mashina na utambuzi wa wapiga kura kutokea kwenye mashina.
"Nimeishi Magomeni Mikumi, lakini sikumjua Mjumbe wangu wa shina na hata sasa hapo ninapoishi See Breeze, Kunduchi, simjui balozi na sijawahi kuona kikao chochote cha shina", akasema Bi Hindu akitoa mfano.
Bi Hindu, amesisitiza pia umuhimu wa kutumia Jumuiya za Chama kuimarisha Chama, akitolea mfano Jumuiya za Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) na Jumuiya ya Wazazi ziingie mitaani, mashuleni na vyuoni kutafuta wanachama wapya.
Kwa upande wa utendaji wa Serikali, amepongeza miradi mingi inayofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mwenyekiti wa CCM, Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, kama Daraja la Kigamboni, Tanzanite na Kigongo Busisi, lakini ameshangaa kuwa yeye binafsi haoni wana CCM wakiisemea miradi hiyo kwa nguvu zote kwa wananchi. Hivyo ameomba mabalozi wawe sehemu ya kuisemea miradi hiyo na mingine mingi kwa kuwa ndiyo wanaoishi na wananchi.
Bi Hindu, amesisitiza pia umuhimu wa Chama kutumia wasanii ambao ni makada haswa wa CCM kutangaza miradi ya CCM iliyofanyika akitolea mifano Mji wa Kiserikali Dodoma na Ujenzi wa Barabara za lami katika maeneo mbalimbali nchini.
Mwishoni mwa mazungumzo hayo, Bi Hindu mwenye umri wa miaka 92, ameomba apatiwe kadi nyingine ya CCM, akisema kuwa aliyokuwa nayo ya zamani ilipotea, ambapo Katibu wa CCM wa Mkoa Cde Mkandawire, ameagiza Afisa Tehama wilaya ya Kinondoni na Katibu wa Wazazi wilaya hiyo kesho Novemba 19, 2026 saa 9:00 alasiri aende nyumbani kwake akamsajili kietronic na Ada ya uwanachama atalipia yeye.
Wakiagana, Bi Hindu amemshukuru Katibu Mkuu wa CCM Dk. Asha-Rose Migiro, kwa kumtuma Katibu wa CCM wa Mkoa Cde Mkandawire kwenda kumsalimia na kwamba amefarijika kuona kwamba Chama kinathamini wastaafu.









No comments:
Post a Comment
Tupia Comments👇