Afisa Tarafa ya Mohoro iliyopo Wilaya ya Rufiji mkoani Pwani Bwanku Musa na Diwani wa Kata ya Chumbi Ali Nguyu Jana Jumatatu Novemba 23, 2026, waliongozana na viongozi na maafisa mbalimbali kufanya mkutano wa hadhara kwenye Kitongoji cha Kipoka Msomeni kusikiliza kero za wakulima na wafugaji na kuweka mikakati ya kukabiliana na kero kubwa ya mifugo kulishwa kwenye mashamba ya wakulima.
Viongozi walioshiriki ni Mtendaji wa Kata Pili Mnema, Polisi Kata, Maafisa Kilimo na mifugo wa Kata pamoja na viongozi wa Kijiji cha Chumbi B na Kitongoji cha Kipoka Msomeni
Mkutano huo ulipokea kero nyingi zilizowasilishwa na upande wa wakulima waliolalamika mifugo kuwa kero kubwa kwenye mashamba yao ikilalamikiwa kuharibu mazao na hivyo kwa pamoja kukubaliana kuimarisha timu za sungusungu za doria za kuhakikisha wafugaji na ng'ombe haziingizwi kwenye mashamba na badala yake ichungiwe kwenye maeneo maalum yaliyotengwa kwa ufugaji kitongojini hapo (Ranchi).
Mkutano huo ulihudhuliwa pia na timu ya viongozi wa wafugaji wilaya pamoja na wale wa sungusungu na wananchi walipata nafasi ya kutoa kero zao na kisha kukubaliana kuweka mikakati ya kukabiliana na suala la migogoro ya wakulima na wafugaji.
Kwa zaidi ya saa nne, mkutano ulijikita kupokea kero za wananchi na kutambulisha timu ya sungusungu kwa wananchi na kila mmoja kusisitizwa kufuata taratibu na sheria zilizowekwa ili kuhakikisha kila mmoja anafanya shughuli zake bila kuwa kikwazo na changamoto kwa mwingine.
Kupitia mkutano huo, Afisa Tarafa Bwanku amesisitiza kwamba mikutano na vikao vitaendelea mara kwa mara kuhakikisha kila mmoja anafuata taratibu zilizowekwa ili wananchi wote wafanye shughuli zao kwa amani na usalama.









No comments:
Post a Comment
Tupia Comments👇