Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mussa Azzan Zungu, amechaguliwa kuwa Rais wa Mkutano wa 153 wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) baada yakupendekwa na Spika wa Bunge la Uingereza (House of Commons), SirLindsay Hoyle.
Pendekezo hilo limetolewa leo, Oktoba 6, 2026, wakati wa Mkutano wa Baraza la Uongozi la IPU uliofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano Arusha (AICC), na kuungwa mkono na Spika kutoka Falme za Kiarabu pamoja na Bunge la Uganda.
Akitoa hoja ya kumpendekeza Zungu, Sir Lindsay Hoyle amesema ana heshima kubwa kupendekeza jina la Spika huyo wa Tanzania, akieleza kuwa uhusiano wao wa muda mrefu na wenye mizizi umempa sababu ya kufanya hivyo.
“Ninayo heshima kumpendekeza Spika wa Tanzania kuwa Rais wa Mkutano wa 153 wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU). Naweza kusema urafiki wa muda mrefu, urafiki wenye mizizi, ndiyo maana kwa heshima kubwa nampendekeza Spika wa Tanzania,” amesema Sir Lindsay Hoyle.
Akitoa salamu za shukrani, Zungu amewashukuru wajumbe kwa kumuunga mkono na kueleza kuwa amekubali kushika nafasi hiyo kwa moyo mmoja.
“Mheshimiwa Rais wa IPU na wajumbe wote wa Mkutano huu, kwa moyo wa dhati, nawashukuru wajumbe wote. Tanzania inajivunia kuwakaribisha jijini Arusha na tutaendelea kuwa pamoja katika Mkutano huu wa 153 wa IPU,” amesema Zungu.
Kwa upande wake, Rais wa IPU na Spika mstaafu wa Bunge la Tanzania, Dkt.Tukia Ackson amempongeza Zungu kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa Mkutano wa 153 wa IPU.

No comments:
Post a Comment
Tupia Comments👇