LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Oct 4, 2026

‎NEEMA LUGANGIRA ASITISHA KAZI WPL, ATII WITO WA RAIS SAMIA

 Asema atahakikisha wananchi wanasikilizwa, changamoto zao zinatatuliwa

‎

‎ARUSHA. Baada ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kumteua kuwa Mkuu wa Wilaya (DC) ya Arumeru, Neema Lugangira amesitisha mkataba wake wa kazi kama Katibu Mkuu wa Shirika la Kimataifa la Wanawake Viongozi Duniani (Women Political Leaders—WPL), akisema amerejea nchini kwa ajili ya kutekeleza dhamana mpya aliyopewa.

‎

‎Lugangira ameeleza kuwa uamuzi huo umefikiwa baada ya kupokea wito wa kulitumikia Taifa kupitia uteuzi huo, huku akisema ameomba ofisi ya WPL iliyopo Brussels, Ubelgiji, kusitisha mkataba wake na kuanza rasmi majukumu yake mapya nchini.

‎

‎Akizungumza baada ya kuapishwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Oktoba 3, 2026, jijini Arusha, Lugangira amesema amepokea uteuzi huo kwa unyenyekevu mkubwa na yuko tayari kushirikiana na wananchi pamoja na viongozi katika kuhakikisha malengo ya Serikali yanafikiwa.

‎

‎“Nimeupokea kwa unyenyekevu mkubwa uteuzi wa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwa DC Arumeru. Kwa hatua hiyo, nimeomba ofisi yangu iliyopo Brussels nchini Ubelgiji kukatisha mkataba wangu wa Katibu Mkuu WPL, na nimerejea nchini na kuanza kazi,” amesema Lugangira.

‎

‎Amesema anamtanguliza Mwenyezi Mungu kwa kumpa fursa hiyo, huku akimshukuru Rais Samia kwa kumwamini na kumpa nafasi ya kumsaidia katika kuwatumikia wananchi wa Arumeru.

‎

‎“Kwanza kabisa namshukuru Mwenyezi Mungu kwa fursa hii. Pia namshukuru sana Mhe. Rais Dkt. Samia kwa uteuzi alionipatia wa kumsaidia kwenye wilaya yetu ya Arumeru,” amesema.

‎

‎Lugangira amesema katika utekelezaji wa majukumu yake mapya, atajikita katika kuhakikisha wananchi wanapata viongozi wanaowasikiliza, wanaowafikia na kuchukua hatua za kutatua changamoto zinazowakabili.

‎

‎Amesema dhamira yake ni kujenga ushirikiano wa karibu na wananchi na viongozi katika ngazi mbalimbali ili kuhakikisha changamoto zinazowakabili wananchi wa Arumeru zinapatiwa ufumbuzi na utekelezaji wa mipango ya Serikali unakuwa na matokeo yanayoonekana.

‎

‎Uteuzi wa Lugangira unampa nafasi ya kuanza rasmi utumishi wa Serikali katika Wilaya ya Arumeru baada ya uzoefu wake katika nafasi ya Katibu Mkuu wa WPL, taasisi inayowakutanisha viongozi wanawake wa kisiasa duniani, wakiwemo marais, makamu wa marais, mawaziri wakuu, mawaziri na wabunge.






‎


No comments:

Post a Comment

Tupia Comments👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages