Aanzisha mfumo wa “Chap kwa DC Arumeru” kupokea malalamiko ya wananchi kupitia simu
MKUU wa Wilaya ya Arumeru, Neema Lugangira, ameanzisha mfumo wa mawasiliano wa “Chap kwa DC Arumeru” unaolenga kuwawezesha wananchi kuwasilisha kero na changamoto zinazowakabili moja kwa moja kwake kwa njia ya ujumbe mfupi wa simu (SMS) au WhatsApp.
Mfumo huo unalenga kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa wananchi, kuimarisha mawasiliano kati ya uongozi wa wilaya na wananchi, pamoja na kuwezesha changamoto mbalimbali kufikishwa kwa mamlaka husika kwa ajili ya kufanyiwa kazi.
Kupitia mfumo huo, wananchi wa Arumeru wanahimizwa kutuma ujumbe wenye kueleza kero zao kupitia namba 0744 663 739, wakati wowote wanapokabiliwa na changamoto zinazohitaji kufikishwa kwa uongozi wa wilaya.
Kwa mujibu wa taarifa ya mfumo huo, Lugangira ameahidi kutoa mrejesho ndani ya siku saba baada ya kupokea kero kutoka kwa wananchi.
Hatua hiyo inaendana na azma ya kuifanya Arumeru kuwa wilaya inayopiga hatua za maendeleo kwa kuzingatia mahitaji ya wananchi, kuboresha huduma na kuimarisha upatikanaji wa fursa za kiuchumi.
Kupitia kaulimbiu ya #TukutaneSite na #ChapKwaDCArumeru, wananchi wanahimizwa kushiriki katika kuibua changamoto zinazowakabili ili ziweze kufikishwa kwa uongozi na kufanyiwa kazi kwa mujibu wa taratibu zilizopo.

No comments:
Post a Comment
Tupia Comments👇