LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Oct 7, 2026

JUWATA YAMPONGEZA SPIKA ZUNGU KUCHAGULIWA KUWA RAIS WA MKUTANO WA 153 WA IPU

 

UONGOZI wa Jukwaa Huru la Wahariri Tanzania (JUWATA) umempongeza Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Mussa Azzan Zungu, kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa Mkutano wa 153 wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU), unaofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano Arusha (AICC).

Mhe. Zungu amechaguliwa leo, Oktoba 6, 2026, katika Mkutano wa Baraza la Uongozi la IPU, baada ya jina lake kupendekezwa na Spika wa Bunge la Uingereza (House of Commons), Sir Lindsay Hoyle, na kuungwa mkono na Spika kutoka Falme za Kiarabu pamoja na Bunge la Uganda.

Katika taarifa yake, JUWATA imesema kuchaguliwa kwa Mhe. Zungu kushika nafasi hiyo ya kimataifa ni heshima kubwa kwa Tanzania, ikieleza kuwa hatua hiyo inaendelea kuonyesha nafasi na ushawishi unaokua wa Tanzania katika diplomasia ya mabunge duniani.

“JUWATA inaamini kuwa Mhe. Zungu atatumia nafasi hii kuongoza kwa weledi, hekima na busara, huku akisimamia misingi ya ushirikiano, amani, demokrasia na diplomasia ya mabunge,” imesema sehemu ya taarifa hiyo.

JUWATA pia imempongeza Mhe. Zungu kwa uongozi wake wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ikisema kuchaguliwa kwake katika nafasi hiyo ya kimataifa ni sehemu ya matokeo ya heshima ambayo Bunge la Tanzania limeendelea kujijengea katika medani ya kimataifa.

TANZANIA YAWEKA HISTORIA IPU

JUWATA imesema uchaguzi wa Mhe. Zungu umeifanya Tanzania kuweka historia katika Mkutano wa 153 wa IPU, kutokana na ukweli kwamba kwa wakati mmoja viongozi wawili kutoka Tanzania wanashika nafasi za juu katika uongozi wa IPU.

Mhe. Zungu amechaguliwa kuwa Rais wa Mkutano wa 153 wa IPU, wakati Spika Mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Tulia Ackson, ni Rais wa IPU.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha, Mhe. Zungu amesema hali hiyo ni historia kubwa kwa Tanzania na kwa IPU, taasisi iliyoanzishwa mwaka 1889.

“Kwa mara ya kwanza katika historia ya Bunge hili ambalo lilianzishwa mwaka 1889, linaendeshwa na Watanzania wawili; Rais wa IPU wa dunia, Dkt. Tulia, na Spika wa Bunge la Tanzania. Hii ni historia kwa Tanzania,” amesema Mhe. Zungu.

Kwa upande wake, JUWATA imesema hatua hiyo ni ishara ya kuongezeka kwa nafasi ya Tanzania katika masuala ya kimataifa, hususan katika kujenga mahusiano na ushirikiano kati ya mabunge ya mataifa mbalimbali.

JUWATA YAIPONGEZA TANZANIA KWA DIPLOMASIA

Jukwaa hilo pia limepongeza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa juhudi zinazoiwezesha Tanzania kuwa mwenyeji wa Mkutano Mkuu wa 153 wa IPU.

Kwa mujibu wa Mhe. Zungu, ushiriki wa Spika wa Bunge la Uingereza, Sir Lindsay Hoyle, katika Mkutano wa 153 wa IPU jijini Arusha ni tukio la kihistoria, akisema kwa zaidi ya miaka 40 Spika wa Bunge hilo hajawahi kuhudhuria kikao kamili cha IPU.

Mhe. Zungu amesema ujio wa Spika huyo nchini Tanzania ni ishara ya hatua kubwa iliyofikiwa na Tanzania katika diplomasia ya kimataifa.

“Kupendekezwa na Spika wa Uingereza kuwa Rais wa Mkutano huu ni suala la diplomasia kubwa sana duniani. Hii inajenga uhusiano mkubwa kati ya Tanzania, mabunge na mataifa mbalimbali,” amesema.

JUWATA imesema fursa ya Tanzania kuwa mwenyeji wa mkutano huo inapaswa kutumika zaidi kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia, kisiasa na kibunge kati ya Tanzania na mataifa mengine duniani.

JUWATA YAMTAKIA ZUNGU MAFANIKIO

JUWATA imemtakia Mhe. Mussa Azzan Zungu kila la heri katika utekelezaji wa majukumu yake mapya, ikisema inaamini ataitumia nafasi hiyo kuitangaza Tanzania, kuimarisha diplomasia ya mabunge na kukuza ajenda za amani, demokrasia, ushirikiano na maendeleo duniani.

Jukwaa hilo pia limelitaja tukio hilo kuwa ni hatua muhimu katika historia ya Bunge la Tanzania na Taifa kwa ujumla, huku likisisitiza umuhimu wa kutumia mafanikio hayo kujenga fursa zaidi za ushirikiano wa kimataifa.

“JUWATA inampongeza kwa dhati Mhe. Mussa Azzan Zungu pamoja na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa hatua hii kubwa ya kihistoria na inamtakia kila la heri katika majukumu yake mapya,” imesema taarifa hiyo.

Mungu ibariki Tanzania.

Richard Mwaikenda
Mwenyekiti – JUWATA
6 Oktoba 2026


 

No comments:

Post a Comment

Tupia Comments👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages