Na Mwandishi Wetu, Arumeru
MKUU mpya wa Wilaya ya Arumeru, Neema Lugangira, ametangaza mpango wa kufanya ziara ya miezi miwili ya mchakamchaka, akilenga kutembelea kata zote za wilaya hiyo ili kusikiliza na kutatua kero za wananchi pamoja na kuimarisha usimamizi wa shughuli za maendeleo.
Lugangira alitangaza mkakati huo baada ya kukabidhiwa rasmi Ofisi ya Mkuu wa Wilaya leo Oktoba 9, 2026, akisisitiza kuwa utendaji wake utajikita katika kutembelea maeneo mbalimbali na kujionea hali halisi ya maisha ya wananchi badala ya kutegemea taarifa za mezani pekee.
Alisema anataka uongozi wake ujengwe katika kufahamu changamoto za wananchi kwa vitendo na kuhakikisha hatua stahiki zinachukuliwa kuzitatua.
"Nataka ninaposema mimi ni Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, iwe ni kwa sababu nimefika mwenyewe, si kwa sababu nimeyasoma maeneo hayo kwenye taarifa za mezani," alisema Lugangira.
ASEMA USALAMA, ARDHI KIPAUMBELE
Katika utekelezaji wa majukumu yake, Lugangira alitaja ulinzi na usalama, utatuzi wa kero za wananchi, migogoro ya ardhi, usafi na utunzaji wa mazingira kuwa miongoni mwa maeneo atakayoyapa kipaumbele.
Pia alisisitiza umuhimu wa kuboresha huduma za kijamii, kusimamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kuhakikisha fedha za umma zinatumika kwa nidhamu, uwazi na kwa kuzingatia malengo yaliyokusudiwa.
Akizungumzia uwajibikaji wa Serikali za Mitaa, alieleza umuhimu wa kuendeleza usimamizi mzuri wa fedha za umma katika Halmashauri za Arusha (Arusha DC) na Meru (Meru DC), ili ziendelee kupata hati safi kutoka kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).


No comments:
Post a Comment
Tupia Comments👇