LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Oct 13, 2026

DC LUGANGIRA ATANGAZA OPERESHENI KUDHIBITI UHALIFU WA BODABODA ARUMERU*

 *_Wananchi kuhamasishwa kutotumia bodaboda zisizotambuliwa_* 

. *_Katibu Mkuu mstaafu wa Bunge la dunia (IPU) aahidi kuwa Balozi wa Arumeru_*

. *_Ofisi ya Mkuu wa Wilaya kuchangia samani Ofisi ya Bodaboda_*


Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Mhe. Neema Kichiki Lugangira, ametangaza kuanza kwa operesheni maalumu ya kuwatambua waendesha bodaboda wote Wilayani humo, akieleza kuwa hatua hiyo inalenga kudhibiti vitendo vya uhalifu vinavyofanywa na baadhi ya watu wanaotumia shughuli za bodaboda kuchafua taswira ya kundi hilo.

Amesema operesheni hiyo itahusisha Jeshi la Polisi na vyombo vingine vya ulinzi na usalama, huku akisisitiza kuwa hakuna kijana atakayeruhusiwa kufanya biashara ya bodaboda katika Wilaya hiyo bila ya kutambulika na uongozi wa eneo lake, huku elimu kwa Umma ikiwa sehemu ya Operesheni hiyo ili kuhakikisha wananchi wanaepuka kutumia bodaboda isiyotambulika na Uongozi husika.

Akizungumza leo Jumanne, Oktoba 13, 2026, wakati wa uzinduzi wa ofisi za Umoja wa Waendesha Bodaboda Halmashauri ya Arusha Dc, Mhe. Lugangira amesema waendesha bodaboda watatakiwa kuwa na vitambulisho maalumu vitakavyoambatana na mavazi ya kuwatambulisha yatakayokuwa na msimbo wa QR (QR Code), ili kurahisisha utambuzi wao na kusaidia kubaini wahusika wa vitendo vya uhalifu. 

Akiwataja bodaboda kama wadau muhimu katika ulinzi na usalama wa jamii, Mhe. Lugangira amewataka kushirikiana na vyombo vya dola kwa kutoa taarifa kuhusu watu wanaotumia shughuli hiyo kufanya uhalifu, akisema lengo ni kuhakikisha waendesha bodaboda wa Arumeru wanakuwa mfano bora nchini kwa kuzingatia weledi, nidhamu na sheria, huku akiahidi kushirikiana nao katika kuboresha mazingira yao ya kiuchumi.

Katika hatua nyingine, Mhe. Lugangira amesema Ofisi yake itagharamia samani za ofisi ya umoja huo, ikiwa ni pamoja na meza, viti na kabati kama ilivyoombwa kwenye risala ya waendesha bodaboda, akiwahimiza pia kutumia fursa za mikopo ya Halmashauri ya vikundi kwa vijana ili waweze kumiliki pikipiki zao na kujikwamua kutoka kwenye pikipiki za mikataba zenye masharti magumu.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu Mstaafu wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU), Mhe. Martin Chung’ong, amewataka waendesha bodaboda kufanya kazi kwa weledi na kutambua nafasi yao kama mabalozi wa Tanzania kwa wageni wanaotembelea Arusha na kuahidi kuwa balozi wa Arumeru katika kuwaunganisha wananchi na fursa za kimataifa, huku akichangia dola za Marekani 200 kusaidia ununuzi wa kompyuta ya matumizi ya ofisi hiyo, akiungwa mkono na Benki ya NMB walioahidi kutoa kichapishi (Printer).

Naye Katibu wa Umoja wa Bodaboda Mkoa wa Arusha, Bw. Hakim Msemo, amempongeza Mhe. Lugangira kwa kukutana na kundi hilo na kuonesha dhamira ya kushughulikia changamoto zao, akisema ni imani yao kuwa historia njema ya Mhe. Lugangira itaendelea kuandikwa katika utumishi wake ndani ya Wilaya hiyo.







 

No comments:

Post a Comment

Tupia Comments👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages