CCM MKOA WA DAR ES SALAAM YAUNGA MKONO NEC KUMVUA UANACHAMA DK. NCHIMBI
Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Dar es Salaam, imeunga mkono maamuzi ya kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, kilichofanyika Agosti 8, 2026 ya kumvua uanachama wa CCM Katibu Mkuu wake wa zamani ambaye pia alikuwa Makamu wa Rais Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi.
Akizungumza na Waandishi wa Habari, Ofisini kwake, katika Ofisi ya CCM mkoa wa Dar es Salaam, Mwenyekiti wa CCM mkoa huo, Abbas Mtemvu, amesema, azimio la kuunga mkono uamuzi huo wa NEC, ulipitishwa na Kikao cha Halmashauri Kuu ya (CCM), mkoa, kilichofanyika jana, Septemba 6, 2026, katika Ukumbi wa Karimjee.
Amesema, katika kikao hichi pia Halmashauri Kuu ya CCM mkoa wa Dar es Salaam ilipongeza maamuzi ya CCM Taifa, na kwamba Halmashauri Kuu inasema maamuzi hayo yamebeba maslahi mapana ya Taifa na yamezingatia ibara ya 103 (8) ya Katiba ya CCM ya mwaka 1977, na ibara 50 (2) (c) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania ya mwaka 1977.
"Pia, kwa kauli moja Halmashauri Kuu ya CCM mkoa wa Dar es Salaam inampongeza Ndg. Deogratius Ndenjembi kwa kupendekezwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuthibitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na hatimaye kuapishwa kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa mujibu wa ibara ya 50 (4) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (1977).
Halmashauri Kuu ya CCM mkoa wa Dar es Salaam inamtakia Makamu wa Rais kazi njema na mafanikio katika jukumu hilo aliloaminiwa na Rais na Mwenyekiti wa Chama chetu Mh. Dkt. Samia Suluhu Hassan", amesema Mtemvu.
Amesema, Halmashauri Kuu ya CCM mkoa wa Dar es Salaam, kwa kauli moja inaunga mkono Mwenyekiti wetu wa Chama Cha Mapinduzi Dk. Samia, kwa kazi nzuri anayoifanya ya kukijenga Chama na nchi na Tanzania.
"Halmashauri Kuu ya CCM mkoa wa Dar es Salaam inamtakia Mh. Rais Afya na Kazi njema", Mtemvu amesema akihitimisha tamko hilo.
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Dar es Salaam, Abbas Mtemvu, akizungumza na Waandishi wa Habari, Ofisini kwake, katika Ofisi ya CCM mkoa huo, leo Septemba 7, 2026. Kulia ni Katibu wa CCM mkoa wa Dar es Salaam Stanley Mkandawire. KUSIKILIZA MTEMVU AKITOA TAMKO HILO BOFYA👉 HAPA

No comments:
Post a Comment
Tupia Comments👇