Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (UWT), umepongeza uamuzi wa wabunge kumthibitisha Deogratius Ndejembi kuwa Makamu wa Rais kwa kura 324, sawa na ushindi wa asilimia 100.
Akisoma tamko la UWT, Agosti 28, 2026, Jijini Dodoma, Mwenyekiti wa Umoja huo Taifa, Mary Chatanda, amesema ushindi wa asilimia 100 unadhihirisha imani kubwa waliyonayo wabunge kuwa Makamu wa Rais mteule, atatimiza kikamilifu majukumu yake katika kumsaidia Rais Dk. Samia Suluhu Hassan.
"UWT tunawapongeza wabunge kwa kupiga kura za kishindo kwa asilimia 100 na hivyo kufanikisha hatua muhimu iliyokuwa mbele ya kuthibitishwa bungeni," amesema Chatanda.
Ameongeza kuwa, UWT inaiunga mkono Halmashauri Kuu ya CCM Taifa kwa kupitisha jina la Deogratius Ndejembi kuwa Makamu wa Rais kwani ni kiongozi mzalendo, mchapakazi na muadilifu katika utekelezaji wa majukumu.
"Halmashauri Kuu haikufanya makosa kupitisha jina hili kwani kote alipofanya kazi, Ndejembi ameonyesha uwezo mkubwa wa utekelezaji wa majukumu, hivyo kuwa chachu ya maendeleo," amesema.
UWT YABARIKI NCHIMBI KUFUTWA UANACHAMA
Katika hatua nyingine, amesisitiz kuwa, UWT inabariki maamuzi yaliyofanywa na Halmashauri Kuu ya kumfuta uanachama, aliyekuwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Dk. Emmanuel Nchimbi, kufuatia vitendo vya utovu wa nidhamu na maadili vinavyotokana na kukiuka katiba, kanuni na miongozo ya Chama.
"UWT inaunga mkono uamuzi wa kumfuta uanachama, Emmanuel Nchimbi, kutokana na makosa ya kimaadili na kinidhamu. Ni vyema wanachama wa CCM wazingatie kuwa hakuna aliye juu ya Chama wala aliye maarufu zaidi ya Chama na kamwe Chama hakiwezi kumfumbia macho mtu anayekibagaza Chama," ameongeza.



No comments:
Post a Comment
Tupia Comments👇