Na Richard Mwaikenda, Dodoma
CHAMA Cha Washauri Elekezi wa Mazingira Tanzania (TEEA) kimetaka Serikali kuweka wazi manufaa ya moja kwa moja ambayo Tanzania itapata kwa kujiunga na Taasisi ya Kimataifa ya Ukuaji wa Uchumi wa Kijani (GGGI), kabla ya Bunge kuridhia mkataba huo.
Ushauri huo umetolewa na Katibu Mkuu wa TEEA, Reuben Makalla, baada ya chama hicho kuwasilisha maoni yake mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira, iliyokutana Agosti 15, 2026 katika Ukumbi wa Philip Marmo, Bungeni Dodoma.
Makalla alisema TEEA imeamua kutoa maoni hayo ili kuhakikisha kuwa kabla ya Tanzania kuingia katika mkataba huo, kunakuwa na uelewa wa wazi kuhusu thamani na manufaa yatakayoongezwa na GGGI ikilinganishwa na taasisi nyingine za kimataifa ambazo Tanzania tayari inashirikiana nazo.
“Tunataka kufahamu mapema manufaa ambayo Serikali ya Tanzania itapata ambayo hayapatikani au hayatoshi katika taasisi nyingine za kimataifa tunazoshirikiana nazo,” alisema Makalla.
Alisema ni muhimu pia kuangalia namna ushiriki wa Tanzania katika GGGI utakavyoongeza uwezo wa wataalamu na taasisi za ndani, pamoja na fursa za kiuchumi zitakazopatikana kutokana na utekelezaji wa miradi ya mazingira na uchumi wa kijani.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira, Jackson Kiswaga, alisema Tanzania inaweza kupata manufaa makubwa katika sekta ya mazingira na uchumi wa kijani endapo Bunge litaridhia mkataba wa GGGI.
Kiswaga, ambaye pia ni Mbunge wa Kalenga, alisema moja ya manufaa makubwa ni kuimarika kwa uwezo wa Tanzania kuibua na kuandaa miradi ya uhifadhi wa mazingira na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Alisema hatua hiyo itaongeza uwezo wa nchi kunufaika na fursa zinazotokana na mipango na mifuko ya kimataifa inayolenga kukabiliana na changamoto za mazingira na mabadiliko ya tabianchi.
“Tutakuwa na fursa kubwa zaidi ya kupata fedha za misaada na mikopo yenye masharti nafuu kwa ajili ya kutekeleza miradi ya mazingira na uchumi wa kijani,” alisema Kiswaga.
Kwa mujibu wa Kiswaga, kuridhiwa kwa mkataba huo kutasaidia pia kuongeza taasisi za ndani zenye ithibati na uwezo wa kusimamia fedha kutoka mifuko ya kimataifa inayolenga mazingira na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Alisema Tanzania inaweza pia kunufaika kwa kuongezeka kwa uwekezaji katika hatifungani za kijamii, huku ushiriki katika GGGI ukiimarisha nafasi ya nchi katika diplomasia na kuongeza ushawishi wake katika masuala ya kisiasa, kiuchumi na mazingira.
Kiswaga aliongeza kuwa fursa nyingine ni kuongezeka kwa ajira kwa Watanzania, hususan kupitia miradi na programu zitakazotekelezwa katika maeneo ya mazingira, mabadiliko ya tabianchi na uchumi wa kijani.
Aidha, alisema ushiriki huo unaweza kuongeza uwezo wa wataalamu wa ndani kupitia tafiti, mafunzo na kubadilishana uzoefu katika masuala ya ukuaji wa uchumi wa kijani.
“Ni muhimu kuona namna nchi yetu inavyoweza kutumia fursa hizi kuimarisha uwezo wa ndani, kuongeza ajira, kuvutia uwekezaji na kuhakikisha mazingira yanahifadhiwa kwa ajili ya kizazi cha sasa na kijacho,” alisema.
GGGI ni taasisi ya kimataifa inayolenga kukuza ukuaji wa uchumi wa kijani unaozingatia ustahimilivu, ushirikishwaji na uendelevu.
Taasisi hiyo hushirikiana na nchi zinazoendelea na zinazoibukia kiuchumi katika kuandaa sera, mikakati na miradi inayolenga kuunganisha maendeleo ya kiuchumi na uhifadhi wa mazingira.
Kikao cha Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira kilikuwa sehemu ya mchakato wa kukusanya maoni ya wadau kuhusu mkataba huo kabla ya Bunge kuchukua hatua zaidi katika mchakato wa kuuridhia.
Mdau kutoka TEEA akiwasilisha maoni katika kamati hiyo ya bunge,
No comments:
Post a Comment
Tupia Comments👇