LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Aug 7, 2026

TANZANIA YAZALISHA TANI 45,101 ZA MBEGU

 Utegemezi wa mbegu kutoka nje wapungua


Na Richard Mwaikenda, Dodoma

Uzalishaji wa mbegu bora za mazao ya kilimo nchini umeongezeka kwa asilimia 55.35 ndani ya kipindi cha miaka minne, hatua inayotajwa kuwa ni sehemu ya utekelezaji wa mpango wa Tanzania wa kujitegemea kwa mbegu na kupunguza utegemezi wa uagizaji kutoka nje.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kudhibiti Ubora wa Mbegu Tanzania (TOSCI), Nyasebwa Chimangu, uzalishaji wa mbegu bora umeongezeka kutoka tani 50,750 mwaka 2021/2022 hadi kufikia tani 78,842 mwaka 2025/2026.

Chimangu amesema kati ya kiasi hicho, tani 45,101 sawa na asilimia 57.2 zimezalishwa nchini kupitia Wakala wa Mbegu za Kilimo (ASA) na kampuni binafsi, huku tani 33,741 sawa na asilimia 42.8 zikiagizwa kutoka nje ya nchi.

Amesema ongezeko hilo linaashiria hatua kubwa katika utekelezaji wa mpango wa kujitegemea kwa mbegu, sambamba na kuimarisha uwezo wa wazalishaji wa ndani kukidhi mahitaji ya wakulima.

Uzalishaji wa mbegu bora umeongezeka kutoka tani 50,750 mwaka 2021/2022 hadi tani 78,842 mwaka 2025/2026, sawa na ongezeko la asilimia 55.35,” amesema Chimangu.

Mkurugenzi huyo ameyasema hayo leo, Agosti 7, 2026, jijini Dodoma, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa majukumu ya TOSCI katika mwaka wa fedha 2025/2026 pamoja na mwelekeo wa mwaka wa fedha 2026/2027.

Kwa mujibu wa takwimu hizo, uzalishaji wa ndani sasa unachangia zaidi ya nusu ya mbegu bora zinazopatikana, huku sekta binafsi na ASA zikiendelea kuwa nguzo muhimu katika kuongeza upatikanaji wa mbegu bora kwa wakulima.

Hatua hiyo inatarajiwa kuongeza upatikanaji wa mbegu bora nchini, kuchochea uzalishaji wa mazao na kuimarisha usalama wa chakula, wakati Serikali ikiendelea kusisitiza matumizi ya mbegu bora kama moja ya msingi wa kuongeza tija katika kilimo.






 

No comments:

Post a Comment

Tupia Comments👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages