Zaidi ya washiriki 2,000 kutoka nchi mbalimbali duniani wanatarajiwa kuhudhuria Mkutano wa 153 wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) utakaofanyika Oktoba 5-9, 2026 jijini Arusha.
Taarifa hiyo imetolewa na Spika wa Bunge, Mheshimiwa Mussa Azzan Zungu wakati akizungumza na waandishi wa habari leo Agosti 4, 2026 katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano (AICC) Jijini Arusha kuhusu utayari wa Bunge kuwa mwenyeji wa mkutano huo.
Mheshimiwa Spika amesema miongoni mwa watakaoshiriki mkutano huo ni Maspika wa Bunge, Wabunge, maafisa wa Bunge, wawakilishi wa mashirika ya kimataifa na kikanda, wanadiplomasia, washirika wa maendeleo, mashirika ya kiraia, taasisi za Elimu ya juu pamoja na vyombo vya habari.
Ameitaja Kauli Mbiu ya Mkutano kuwa “Kuimarisha Utawala Bora na Kuiwezesha Jamii kupitia Ushirikishwaji, Imani na Fursa kwa Wote" na kwamba ufunguzi rasmi utafanywa na Rais, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan 05 Oktoba, 2026.
Amesema Bunge la Tanzania lipo tayari kikamilifu kuwa mwenyeji wa mkutano huo wa kihistoria na kwamba ni heshima kubwa kwa nchi na ni uthibitisho wa imani ambayo jumuiya ya kimataifa ya mabunge inayo kwa Tanzania.
"Hii inathibitisha dhamira yetu ya muda mrefu katika kudumisha demokrasia, amani, ushirikiano wa kimataifa na diplomasia ya kibunge" amesema Mheshimiwa Spika.
Mheshimiwa Spika amesema ana imani mkutano huo utaleta mchango mkubwa katika kutatua changamoto zinazokabili dunia kwa sasa ikiwemo Mabadiliko ya Tabianchi, migogoro ya kimataifa na ugumu wa maisha.
Mbali na ratiba rasmi, amesema mkutano huo utaimarisha ushirikiano wa Kimataifa, kukuza ushirikiano wa kimkakati na kutoa fursa adhimu kwa sekta za utalii, usafirishaji na huduma nchini.
“Pia utatoa fursa ya kuionesha dunia utajiri wa utamaduni wa Tanzania, fursa za uwekezaji na vivutio vya utalii vinavyotambulika duniani,” amesema
Awali akizungumza baada ya kukagua Ukumbi wa AICC, Mheshimiwa Zungu amesema mandaliziyanaendelea vizuri kupitia ushirikiano wa karibu kati ya Bunge, Serikali, Sekretarieti ya IPU na wadau wengine.
Amewakaribisha washiriki wote Jijini Arusha katika mkutano huo.
No comments:
Post a Comment
Tupia Comments👇