LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Aug 19, 2026

JWTZ YATANGAZA HUDUMA BURE KATIKA WIKI YA USHIRIKIANO WA MAJESHI YA EAC

JESHI la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) linatarajia kuwa mwenyeji wa Maadhimisho ya Sita ya Wiki ya Ushirikiano wa Majeshi ya Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Raia, yatakayofanyika kuanzia Agosti 2026 hadi Septemba Mosi, mwaka huu.

Katika maadhimisho hayo, majeshi kutoka nchi wanachama wa EAC yatatoa huduma mbalimbali kwa wananchi, ikiwemo huduma za afya bure zitakazotolewa na madaktari bingwa kutoka Burundi, Somalia, Tanzania, Rwanda, Kenya na Uganda.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma jana, Agosti 19, 2026, Mkurugenzi wa Huduma za Tiba Utawala Jeshini, Brigedia Jenerali Dkt. Agatha Mary Katua, alisema huduma hizo zitatolewa katika hospitali na vituo vya afya vilivyoainishwa katika maeneo mbalimbali nchini.

Alisema maadhimisho hayo hufanyika kila mwaka katika mojawapo ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, huku Tanzania ikiwa imepewa nafasi ya kuwa mwenyeji mwaka huu, baada ya mara ya mwisho kufanya hivyo mwaka 2022.

Kwa mujibu wa Brigedia Jenerali Dkt. Katua, mikoa itakayohusika na utoaji wa huduma hizo ni Dar es Salaam, Pwani, Arusha na Zanzibar.

DAR ES SALAAM

Kwa upande wa Dar es Salaam, huduma za afya zitatolewa katika Hospitali ya Wilaya ya Ubungo, Hospitali ya Vijibweni Kigamboni na Kituo cha Afya Yombo Malawi.

Aidha, shughuli hizo zitagusa pia vituo vya kulelea watoto yatima na wenye mahitaji maalumu, ambapo huduma zitatolewa katika Makao ya Taifa ya Watoto Kurasini Temeke, Mwandaiwa Orphanage Centre, Bunju Kinondoni, Kituo cha Makazi ya Watoto Chanika, Ilala, pamoja na SOS Zanzibar.

PWANI, ARUSHA NA ZANZIBAR

Mkoani Pwani, wananchi watanufaika na huduma hizo katika Hospitali Teule ya Rufaa ya Mkoa wa Pwani Tumbi na Hospitali ya Wilaya ya Bagamoyo.

Kwa upande wa Zanzibar, huduma zitatolewa katika Hospitali ya Wilaya ya Mwerapongwe, Unguja, na Hospitali ya Wilaya ya Vitongoji, Pemba.

Pia, majeshi hayo yatatoa huduma kwa wafungwa katika Gereza la Segerea jijini Dar es Salaam na Gereza la Kisongo mkoani Arusha, ikiwa ni sehemu ya mpango wa kuwafikia wananchi katika makundi mbalimbali.

UKARABATI WA MIUNDOMBINU

Mbali na huduma za afya na misaada kwa makundi maalumu, maadhimisho hayo yatahusisha pia ukarabati wa baadhi ya miundombinu ya kijamii, ikiwemo katika Kituo cha Makao ya Taifa Kurasini, Kituo cha Afya Mapinduzi Dodoma Chamwino na Kituo cha Afya Kibokoni Pemba.

Brigedia Jenerali Dkt. Katua alisema shughuli hizo ni sehemu ya utekelezaji wa dhana ya ushirikiano kati ya majeshi ya nchi wanachama wa EAC na wananchi, kwa lengo la kuimarisha uhusiano, mshikamano na ustawi wa jamii.

JWTZ limewataka wananchi katika maeneo yatakayohusika kutumia fursa hiyo kunufaika na huduma zitakazotolewa wakati wa maadhimisho hayo.


Mkurugenzi wa Huduma za Tiba Utawala Jeshini, Brigedia Jenerali, Dkt Katua akizungumza katika mkutano huo.






IMEANDALIWA NA RICHARD MWAIKENDA - 0754264203
 

No comments:

Post a Comment

Tupia Comments👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages