HOSPITALI ya Rufaa ya Wanyama ya Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) imeendelea kuwa nguzo muhimu katika utoaji wa huduma za kisasa za tiba ya wanyama nchini, huku ikitoa huduma za matibabu, upasuaji, uchunguzi, uangalizi maalumu na mafunzo kwa wanafunzi wa tiba ya wanyama.
Hospitali hiyo iliyopo katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo, Morogoro, chini ya Chuo cha Tiba ya Wanyama na Sayansi za Tiba, inahudumia aina mbalimbali za wanyama wakiwemo mbwa, paka, ndege, wanyama wa kufugwa kama ng'ombe, mbuzi, kondoo na nguruwe pamoja na wanyama wengine.
Hayo yamebainishwa na Prof, Raphael Chibunda Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo ( SUA) akizungumza na waaandishi wa habari Jijini Dodoma Agosti 31, 2026, kuhusu utekelezaji wa Mwaka wa Fedha 2025/26 na Mwelekeo wa 2026/27.
.
Kwa mujibu wa Prof, Chibunda, hospitali hiyo ina wataalamu wa tiba ya wanyama, madaktari bingwa na wanafunzi wanaofanya kazi kwa pamoja kuhakikisha wanyama wanapata huduma bora za matibabu na dharura.
Ametaja huduma zinazotolewa kuwa ni pamoja na tiba za jumla, tiba ya magonjwa ya mfumo wa uzazi, upasuaji wa mifupa na tishu laini, upasuaji wa macho, tiba ya saratani, magonjwa ya mfumo wa fahamu na magonjwa ya moyo.
HUDUMA MASAA 24
Moja ya huduma muhimu zinazotolewa na hospitali hiyo ni huduma za dharura na uangalizi maalumu kwa wanyama wenye hali mbaya.
TAARIFA ZAIDI KUHUSU HOSPITALI HIYO;
Kwa mujibu wa SUA, hospitali iko wazi muda wote kwa ajili ya kushughulikia wagonjwa wa dharura na walio katika hali mahututi, wakiwemo wanyama wachanga wanaohitaji uangalizi maalumu na wanyama wenye mimba zilizo katika hatari.
Hatua hiyo imeifanya hospitali kuwa sehemu muhimu kwa wafugaji na wamiliki wa wanyama wanaohitaji huduma za kitaalamu ambazo huenda zisipatikane katika vituo vya kawaida vya tiba ya wanyama.
KITUO CHA MAFUNZO
Mbali na kutoa huduma kwa wanyama, Hospitali ya Rufaa ya Wanyama ya SUA ni hospitali ya kufundishia, inayowawezesha wanafunzi wa tiba ya wanyama kupata uzoefu wa vitendo kwa kushiriki katika mazingira halisi ya matibabu.
Maboresho yaliyofanyika hospitalini humo yamelenga pia kuongeza uwezo wa kufundishia wanafunzi kwa kuwapatia mazingira bora na vifaa vya kisasa.
Mchango huo unaifanya hospitali kuwa sehemu muhimu katika maandalizi ya wataalamu watakaoshughulikia afya ya mifugo na wanyama nchini.
ZAIDI YA MATIBABU
Hospitali hiyo pia imekuwa ikishiriki katika huduma za jamii, ikiwemo kampeni za chanjo na elimu kuhusu magonjwa yanayoweza kuathiri wanyama na binadamu.
Miongoni mwa mifano ni kampeni ya chanjo dhidi ya kichaa cha mbwa iliyofanyika katika kata za Bigwa na Mindu, Manispaa ya Morogoro, ambapo zaidi ya mbwa 340 walipatiwa chanjo katika vituo mbalimbali. Wanafunzi wa Shahada ya Tiba ya Wanyama wa SUA walishiriki katika zoezi hilo kama sehemu ya mafunzo yao kwa vitendo.
Kwa upande mwingine, taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kuhusu SUA inaonyesha kuwa katika mwaka wa fedha 2023/24, Hospitali ya Rufaa ya Wanyama ya Chuo Kikuu ilitoa huduma za tiba kwa wanyama zaidi ya 994.
KITUO CHA RUFAA KITAIFA
SUA imekuwa ikiitaja hospitali hiyo kama hospitali ya rufaa ya wanyama yenye umuhimu wa kitaifa, huku ikihudumia wafugaji na wamiliki wa wanyama wanaohitaji huduma za kibingwa.
Taarifa ya SUA imeeleza kuwa hospitali hiyo imekuwa na mchango mkubwa katika kutatua changamoto mbalimbali za afya ya wanyama nchini, huku maboresho ya miundombinu na vifaa yakilenga kuongeza kiwango cha huduma.
Kwa sasa, hospitali hiyo inaendelea kujenga nafasi yake kama kituo kinachounganisha tiba, utafiti, elimu na huduma kwa jamii, jambo linaloifanya kuwa sehemu muhimu katika kuimarisha sekta ya mifugo na afya ya wanyama nchini Tanzania.
Prof, Raphael Chibunda Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo ( SUA) akizungumza na waaandishi wa habari Jijini Dodoma Agosti 31, 2026, kuhusu utekelezaji wa Mwaka wa Fedha 2025/26 na Mwelekeo wa 2026/27.
Wanahabari wakiwa katika mkutano huo.





No comments:
Post a Comment
Tupia Comments👇