SERIKALI ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan imefanikiwa kuongeza mikopo ya maendeleo kwa sekta za kilimo, ufugaji na uvuvi hadi zaidi ya shilingi trilioni 1.2, hatua inayotajwa kuchochea ongezeko kubwa la uzalishaji wa mazao na kuifanya Tanzania kujitosheleza kwa chakula kwa asilimia 130.
Mkurugenzi Mwendeshaji wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB), Frank Nyabundege, amesema ongezeko hilo limeifanya benki hiyo kuwa miongoni mwa taasisi muhimu zinazochochea mageuzi ya sekta ya kilimo nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma, Julai 30, 2026, katika Ukumbi wa Idara ya Habari–MAELEZO, Nyabundege alisema thamani ya mikopo iliyotolewa na TADB imeongezeka kwa kasi kubwa tangu Rais Samia alipoingia madarakani mwaka 2021.
Alisema wakati Serikali ya Awamu ya Sita ikiingia madarakani, mikopo iliyokuwa imetolewa na benki hiyo ilikuwa na thamani ya shilingi bilioni 294, lakini imeongezeka hadi kufikia zaidi ya shilingi trilioni 1.2.
“Tangu TADB ilipoanzishwa, benki imetoa mikopo yenye thamani ya jumla ya shilingi trilioni 1.55, ambapo zaidi ya shilingi trilioni 1.2 zimetolewa katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Sita.” — Frank Nyabundege
Nyabundege alikuwa akitoa taarifa kuhusu utekelezaji wa shughuli za TADB katika mwaka wa fedha 2025/26 pamoja na mwelekeo wa benki hiyo kwa mwaka wa fedha 2026/27.
Alisema mikopo hiyo imeelekezwa katika kuimarisha uzalishaji na kuongeza tija katika sekta za kilimo, ufugaji na uvuvi, hatua iliyochangia kuongezeka kwa uzalishaji wa mazao muhimu ya chakula.
Kwa mujibu wa Nyabundege, uzalishaji wa mahindi umeongezeka kutoka tani milioni 6.4 hadi tani milioni 12.2, sawa na ongezeko la asilimia 91.
Aidha, uzalishaji wa mpunga umeongezeka kutoka tani milioni 1.7 hadi tani milioni 3.04, sawa na ongezeko la asilimia 72.
Alisema mafanikio hayo yameiwezesha Tanzania kufikia kiwango cha kujitosheleza kwa chakula kwa asilimia 130, huku asilimia 30 ya uzalishaji ikiwa ni ziada inayoweza kuuzwa katika masoko ya nje.
Nyabundege alisema ziada hiyo inatoa fursa kwa Tanzania kuongeza mauzo ya mazao katika masoko ya kimataifa, kuingiza fedha za kigeni na kuongeza kipato cha wakulima.
Aliongeza kuwa TADB itaendelea kupanua wigo wa utoaji wa mikopo kwa wadau wa kilimo, ufugaji na uvuvi ili kuongeza uzalishaji, kuimarisha usalama wa chakula na kuchangia ukuaji wa uchumi wa taifa.
Mkurugenzi Mwendeshaji wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania ( TADB), Frank Nyabundege, akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma Julai 30, 2026, katika ukumbi wa Idara ya Habari-MAELEZO.
IMEANDALIWA NA RICHARD MWAIKENDA - 0754264203
No comments:
Post a Comment
Tupia Comments👇