Wito umetolewa kwa wanawake nchini kuwa sehemu ya hamasa ya kuelimisha jamii kuepuka uchochezi wa kufanya maandamano badala yake waitunze tunu ya amani iliyopo.
Hayo yameelezwa na Mwenyekiti Taifa wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), Mary Chatanda, Julai 3, 2026, Jijini Dodoma.
Amesema, kama ambavyo ukimwelimisha mwanamke umeelimisha jamii nzima, hivyo mwanamke akisimama imara atakuwa sehemu ya kuepusha maandamano yanayoratibiwa na baadhi ya wanasiasa na wanaharakati, Julai 7.
"Leo, nina ujumbe mahsusi kwa wanawake wenzangu. Nina wajibu wa kuongea na wanawake na wananchi kwa ujumla juu ya kutunza tunu ya amani tuliyonayo. Wanawake, hebu tukae chini na waume zetu, tuwaelimishe umuhimu wa amani na kuepuka maandamano".
"Kimsingi, shughuli wanazofanya za kuingiza vipato ambavyo tunapata chakula na mahitaji muhimu ya watoto wetu wanaosoma shuleni na vyuoni hazitafanyika katikati ya vurugu na maandamano," amesema Chatanda.
Aidha, Chatanda amesema, wanawake wasiache kuzungumza na watoto na vijana wao ambao wakati mwingine wamekuwa wakishawishiwa kushiriki matukio ambayo hayana tija kwa maendeleo.
"Wanawake pia wazungumze na vijana wao ambao mara nyingi wanakuwa mstari wa mbele kuandamana wakati waratibu wa maandamano hayo, watoto wao wako nyumbani au nje ya nchi wametulia majumbao mwao, wakiangalia TV," amesisitiza.
Mwenyekiti huyo ameongeza kuwa, kuharibu amani ni rahisi lakini kuijenga ni kazi kubwa inayorudisha nyuma harakati za ujenzi wa taifa kuanzia matumizi ya raslimali muda na fedha, jambo ambalo halikubaliki.
Pia, amesisitiza kuwa, tupo katika nyakati ambazo serikali imeanza utekelezaji wa bajeti mpya ya mwaka wa fedha 2026/2027, ambayo msisitizo wake ni utatuzi wa kero za wananchi na uboreshaji wa ustawi wao.
Katika siku za hivi karibuni, kumekuwa na hamasa hasa mitandaoni kushawishi wananchi kuandamana Julai 7, mwaka huu, jambo ambalo limeshapigwa marufuku na serikali kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama, huku wananchi wakihimizwa kuendelea na shughuli zao za kimaendeleo ili kukuza maendeleo yao na ya taifa pia.
</

No comments:
Post a Comment
Tupia Comments👇