WAZIRI Mkuu Mstaafu, Mizengo Pinda, ameongoza shughuli ya upandaji wa takribani miti 7,000 katika eneo la Ndejengwa jijini Dodoma, ikiwa ni hatua ya kuelekea utekelezaji wa mradi wa kuanzisha Msitu wa Mjini (Urban Forest) utakaohusisha upandaji wa miti 20,000 katika Jiji la Dodoma.
Shughuli hiyo imeandaliwa na Habari Conservation Organisation (HCO) kwa ufadhili wa East African Crude Oil Pipeline (EACOP) na ni sehemu ya kampeni ya "Kijanisha Dodoma" iliyoasisiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, alipokuwa Makamu wa Rais.
Akizungumza baada ya kushiriki upandaji wa miti hiyo, Pinda amesema uanzishwaji wa misitu ya mijini ni hatua muhimu katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, kupunguza ongezeko la joto, kuhifadhi vyanzo vya maji na kuboresha mazingira ya makazi.
Amesema ukuaji wa miji unapaswa kwenda sambamba na uwekezaji katika maeneo ya kijani ili kuhakikisha maendeleo yanakuwa endelevu.
"Hatupaswi kupanda miti tu, bali tuihudumie mpaka ikue. Kila Mtanzania ana wajibu wa kushiriki katika kulinda mazingira kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho," amesisitiza Pinda.
Afisa Uhusiano wa HCO, Royce Joseph, amesema lengo la mradi huo ni kupanda miti 20,000 ya aina mbalimbali na kuanzisha msitu wa mijini utakaosaidia kufyonza hewa ukaa, kuboresha mfumo wa ikolojia, kuimarisha biashara ya kaboni na kuongeza maeneo ya kijani katika makao makuu ya nchi.
Amesema miti 7,000 iliyopandwa ni hatua muhimu kuelekea kufikiwa kwa lengo hilo, huku akiwataka wananchi, taasisi na kampuni kushiriki kwa kupanda miti wakati wa maadhimisho ya matukio mbalimbali ya maisha na shughuli zao.
Kwa upande wake, mwanafunzi wa EG White Secondary School iliyoshiriki katika upandaji miti, Renata Kimata, amesema shule hiyo tayari imepanda miti zaidi ya 1,000, hatua ambayo imeboresha mazingira ya kujifunzia na kuwajengea wanafunzi utamaduni wa kuhifadhi mazingira.
Naye mdau wa mazingira, Mhandisi Athuman Futakamba, ameipongeza EACOP kwa kufadhili mradi huo na kutoa wito kwa wadau wengine wa maendeleo kuunga mkono juhudi za kuongeza maeneo ya kijani nchini.
Mradi huo umewashirikisha taasisi za serikali, sekta binafsi, viongozi wa dini, wanafunzi na wananchi, huku HCO ikieleza kuwa itaendelea kushirikiana na Serikali katika kutekeleza kampeni za upandaji miti, uhifadhi wa misitu na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Kampeni ya "Kijanisha Dodoma" inalenga kuifanya Dodoma kuwa jiji la kisasa lenye mazingira bora kupitia ongezeko la maeneo ya kijani, sambamba na kuhamasisha wananchi kushiriki katika utunzaji wa mazingira.
Waziri Mkuu Mstaafu, Mizengo Pinda akizungumza wakati wa upandaji miti.
IMEANDALIWA NA RICHARD MWAIKENDA - 0754264203





No comments:
Post a Comment
Tupia Comments👇