LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Jun 30, 2026

BARAZA LA UWT KIBAHA MJI LAAZIMIA KULETA MAGEUZI KATIKA KUJIKWAMUA KIUCHUMI

Umoja wa wanawake Tanzania (UWT) Wilaya ya Kibaha katika kupambana na changamoto ya wimbi la umasikini imejiwekea mikakati kabambe ya kuweza kuanzisha miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo  vitega uchumi mbalimbali kuanzia ngazi za matawi na kata ambayo itaweza kuwasaidia kuondokana na kuwa tegemezi na kujikwamua kiuchumi.

Hayo yamebainishwa na Katibu wa UWT Wilaya ya Kibaha, Cesilia Ndalu wakati wa kikao cha baraza la kikanuni ambalo limehudhuliwa na viongozi mbalimbali wa Jumuiya hiyo pamoja na viongozi wa chama ambapo wameweza kujadili mambo mbali mbali ambayo yataweza kusaidia katika kuimarisha jumuiya yao.


Katibu huyo amebainisha kwamba lengo lao kubwa ni kuhakikisha wanajipanga kuwa wabunifu ya kuanzisha miradi mbalimbali ya maendeleo na kuwa na vitega uchumi vipya ikiwa pamoja na kuendeleza na kuwa na miradi ya ujenzi wa nyumba kwa ajili ya kuishi makatibu wa jumuiya,


"Tumefanya kikao cha kikanuni cha kikao cha baraza letu la UWT Wilaya ya Kibaha mjini ambapo tumeweza kujadili mambo mbalimbali ikiwemo suala la kuwa na miradi ya vitega uchumi, mradi wa ujenzi wa nyumba ya mtumishi pamoja na suala zima la wanawake kuanzisha vikundi mbalimbali vya ujasiriamali,"amebainisha Katibu Ndalu.


Kwa upande wake Katibu wa chama cha mapinduzi (CCM) Wilaya ya Kibaha Isack Kalleiya ambaye mgeni rasmi katika ufunguzi wa baraza hilo amewataka wanawake hao kuchapa kazi kwa bidii na weledi na kuwahimiza kwamba viongozi wanapaswa kuboresha mahusiano mazuri katika ngazi mbalimbali ikiwa sambamba na kufanya kazi kwa kuzingatia sheria na kanuni zilizowekwa na kudumisha suala la amani.

Aidha Katibu Kalleiya amewaasa wanawake kuhakikisha kwamba wanatekeleza majukumu yao ipasavyo na kufanya vikao vya mara kwa mara ambayo vitaweza kusaidia katika kuleta mageuzi na kuweka misingi imara katika kukipambania chama cha mapinduzi pamoja na kuimarisha umoja wao wa wanawake sambamba na kuboresha mahusiano.


Mwenyekiti wa UWT Wilaya ya Kibaha mjini Elina Mgonja amesema kwamba wanawake wanapaswa kuwa na vikundi vya ujasiriamali ambapo pia amejipanga kufanya ziara maalumu ambayo itatoa fursa kwa ajili kutoa mafunzo ya ujasiriamali ambapo hadi sasa wanufaika wa mafunzo hayo wameshanufaika wanawake 500.


Katibu wa UWT Mkoa wa Pwani Aziza Hussein amewataka wanawake kuachana kabisa tabia ya kutengenezeana chuki na kufanya kazi kwa maslahi ya jumuiya pamoja na kuhakikisha wanaacha alama katika suala zima la utekelezaji wa majukumu yao na kuweka mikakati ya kuongeza idadi ya wanachama.  


Katika hatua nyingine akifunga kikao hicho cha baraza la UWT Mwenyekiti wa chama cha mapinduzi (CCM), Mwalimu Mwajuma Nyamka amewahimiza wanawake hao kuwa na umoja na mshikamano sambamba na kudumisha hali ya amani katika ngazi zote.


Katika kikao cha baraza hilo ajenda mbalimbali zimeweza kujadiliwa ikiwemo suala la kuwepo na vitega uchumi, kuendelea na mradi wa nyumba ya mtumishi, pamoja na kuwasilisha taarifa ya utekelezaji wa kazi kuanzia kipindi cha kuanzia mwezi Januari hadi Juni mwaka 2026.




 

No comments:

Post a Comment

Tupia Comments👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages