LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Apr 10, 2026

WAKAZI WA DAR WAIPONGEZA NMB IKIZINDUA HUDUMA YA MATAWI YANAYOTEMBEA

 

 Mkuu wa Idara ya Mauzo na Mtandao wa Matawi ya Benki ya NMB, Donatus Richard (katikati), akimhudumia Mwajuma Athumani Saidi aliyehudhuria uzinduzi rasmi wa utoaji huduma kupitia magari maalum (Matawi Yanayotembea – Bank on Wheels’), uliofanyika jijini Dar es Salaam. Magari hayo nane ni sehemu ya mkakati endelevu wa usambazaji Huduma za Kibenki Vijijini ‘NMB Rural Banking Strategy. ‘

BENKI ya NMB imepuliza rasmi kipyenga cha matumizi ya Magari Maalum Yanayotoa Huduma za Kibenki (Matawi Yanayotembea – Bank on Wheels), huku wakazi wa Dar es Salaam wakiipongeza benki hiyo kwa kuiishi kwa vitendo kaulimbiu yake ya Karibu Yako.

Mapema mwaka huu, NMB iliyatambulisha rasmi magari nane yatakatotumika kama Matawi Yanayotembea, yakilenga kuwafikishia Huduma Jumuishi za Kibenki wakazi wa mijini na vijijini, hususani kwenye masoko, minada ya mifugo, biashara na machimbo ya madini.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa utoaji huduma jijini Dar es Salaam Alhamisi Aprili 9, Mkuu wa Idara ya Mauzo na Mtandao wa Matawi ya NMB, Donatus Richard, alisema ‘Bank on Wheels’ ni sehemu ya mkakati wao wa usambazaji wa Huduma za Kibenki Vijijni ‘NMB Rural Banking Strategy.’

Alibainisha kuwa, magari hayo yatagawanywa katika kanda mbalimbali za beni hiyo, kuyaongezea nguvu yale waliyokuwa nayo awali, lengo likiwa ni kuwafikia wateja wao zaidi ya Mil. 10 na kuvutia wengine kufungua akaunti na kuwa sehemu ya benki hiyo ili kuharakisha ukuaji wao kiuchumi.

“Magari haya ni zaidi ya fursa kwa wateja wetu, wajasiriamali, wafanyabiashara kwenye masoko na minada na kwa wadau wa mnyororo wa thamani kilimo unaojumuisha kilimo chewe, ufugaji na uvuvi, kuwawezesha kupata huduma za kifedha, ushauri, bima, mikopo na elimu ya fedha. 

“Tafiti mbalimbali zinaonesha kuwa taasisi nyingi za fedha hususani mabenki, yamejikita katika kuimarisha utoaji huduma mijini, lakini sisi NMB tunatambua ukubwa wa mzunguko wa fedha uliopo huko na ndio maana tumechagua kuwafuata huko kuwahudumia kwa ukaribu bila kuwapotezea muda.

“Leo tumeanza rasmi kutoa huduma kupitia magari haya yaliyozinduliwa wakati wa uzinduzi wa Mpango Mkakati wa Muda wa Kati wa Mwaka 2026 hadi 2030 (MTP Agenda 2030). Haya yanaenda kuungana na yale yaliyokuwepo awali na, lakini tutayaongeza kulingana na mahitaji,” alisema.

Donatus alibainisha kwamba watayagawa katika Kanda za Dar es Salaam, Zanzibar, Kanda ya Kati, Kanda ya Kusini, Kanda ya Kaskazini, Kanda ya Ziwa, Kanda ya Magharibi na Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, ambako yatapangiwa ratiba ya kutoa huduma katika mikoa inayounda kanda hizo.

Aliwataka Watanzania kuhakikisha wanaendana na kasi ya benki yake katika kujenga Uchumi Jumuishi, tangu walipoanza na NMB Mkononi, kisha wakaja na mawakala ambao sasa wamefikia zaidi ya 73,000 kote nchini na sasa kuja na Matawi Yanayotembea, lengo likiwa kuharakisha ukuaji wao kiuchumi.

Hellen Mushi, ambaye ni mfanyabiashara wa Duka la Simu katika Jengo la Manzese Plaza, lililopo Manzese Bakhresa, alikiri kufurahishwa na namna NMB inavyowajali wateja wao kwa kuwasogezea huduma za kibenki mahali walipo na kwamba hiyo ndio maana halisi ya Karibu Yako.

“Binafsi hii imenivutia sana, nimekuwa mteja ninayetumia huduma za NMB kwa muda mrefu, lakini kila uchao wamekuwa na utamaduni wa kubuni bidhaa na huduma rafiki kwa wateja. Hii ‘Bank on Wheels’ ni kubwa na bora zaidi, kwa sababu inatupa uhuru sisi tusiopenda kupoteza muda matawini.

“Nawapongeza na kuwashukuru, huku nikiwataka Watanzania kuchangamkia fursa zilizomo katika huduma za benki hii, ambayo licha ya kuwa na matawi mengi karibu katika kila wilaya, lakini bado inaona umuhimu wa kuwafikia walioko vijijini, minadani na mashambani,” alisema Hellen. 

Naye Mchungaji Elias Masangu Waburuba, Mkazi wa Kahama mkoani Shinyanga, aliyeshuhudia uzinduzi wa utoaji huduma wa ‘Bank on Wheels’ jijini Dar es Salaam, aliipongeza NMB kwa huduma bora, bunifu, rahisi, salama na nafuu kwa wateja wao wadogo, wa kati na wakubwa.

“Benki hii imekuwa rafiki kwa wateja wao na wananchi kwa ujumla, wakiwemo walioko mbali na miji, kwa sababu huduma zao zimesambaa mpaka vijijini sio tu kupitia matawi, bali mawakala wao, huku pia kukiwa na huduma za NMB Mkononi, ambayo ni rahisi kutumia ikiwa na fursa kibao.

“Ndio maana nakiri kwamba NMB ni benki iliyorahisisha sana huduma za kifedha kwa wananchi, binafsi naipongeza kwa huduma bora na kwa kuwa nimekuja Dar es Salaam kibiashara tu kutoka Kahama, basi naamini tutakutana tena huko vijijini na naahidi kuwa balozi mwema wa benki hii. 

“Kule kwenye magulio na minada ya mifugo, mazao na madini, vihatarishi kwa watu wenye pesa taslimu mkononi ni vingi, ikiwemo wizi, uporaji, upotevu na mengineyo, kwa hiyo NMB kuja na Matawi Yanayotembea, ni kutusaidia sisi wadau wa biashara,” alisisitiza Mchungaji Elias.

Madereva wa malori, mama lishe, wauza mitumba na bidhaa zingine wanaozunguka eneo la Manzese Darajani, walioshuhudia uzinduzi wa utoaji huduma za kibenki kupitia Matawi Yanayotembea, waliipongeza NMB kwa kuwa mbele ya wakati kupitia huduma zao bunifu.

No comments:

Post a Comment

Tupia Comments👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages