LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Mar 27, 2026

RAIS DKT.MWINYI AFUNGUA MPANGO WA PILI WA KUBORESHA MAZINGIRA YA BIASHARA NA UWEKEZAJI (MKUMBI II)


Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Dkt. Hussein Ali Mwinyi akihutubia wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Uhakiki wa Rasimu ya Mpango wa Pili wa Kuboresha Mazingira ya Biashara na Uwekezaji (MKUMBI II) kwenye Ukumbi wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere Dar es Salaam Machi 27, 2026.

Mkumbi huo umeandaliwa na Kamati ya Kitaifa ya Wataalamu (NTT- MKUMBI II) iliyoongozwa na Mwenyekiti, Prof. Faustine Kamuzora  Chini ya Wizara ya Mipango na Uwekezaji.


HOTUBA YA RAIS DKT. HUSSEIN ALI MWINYI

 'Kazi naUtu.................... Tunasonga Mbele' Ndugu Wageni Waalikwa, awali ya yote, ninapenda kuanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehma kwa kutujaalia afya njema na kutuwezesha kushiriki katika Warsha ya Uhakiki (Validation Workshop) wa Rasimu ya Mpango wa Pili wa Kuboresha Mazingira ya Biashara na Uwekezaji (MKUMBI-II).


Ndugu Wageni Waalikwa, nitumie fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Profesa Kitila Alexander Mkumbo (Mb.), Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji na Uongozi mzima wa Ofisi kwa kushirikiana na wizara za Kisekta kwa namna ambavyo wanatekeleza kazi ya kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini. Hongereni Sana.


 Mpango wa kuboresha mazingira ya Biashara na Uwekezaji (MKUMBI) umekuwa nguzo muhimu ya kuhakikisha kuwa, kila sekta inatimiza wajibu wake katika kuweka mazingira wezeshi ya uwekezaji na ufanyaji biashara na hivyo kuvutia Uwekezaji na Biashara Nchini. 

Ndugu Wageni Waalikwa, Kama mnavyofahamu, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeandaa Dira 2050, inayolenga kuiwezesha Tanzania kufikia hadhi ya nchi yenye uchumi wa kipato cha juu ifikapo mwaka 2050. 

Dira hiyo inalenga kufikia uchumi wenye thamani ya Dola za Marekani trilioni 1, pamoja na kipato cha kila mtu cha wastani wa takribani Dola 7,000 (sawa na takribani Shilingi milioni 18.2 kwa mwaka).

 Katika Kwa muktadha huo, sekta binafsi imeainishwa kuwa kiungo muhimu na injini ya kufanikisha malengo hayo ya maendeleo.


Ili kufikia azma hiyo, nchi inahitaji ukuaji endelevu wa Pato la Taifa wa angalau asilimia 10 kwa mwaka kuanzia 2026 hadi 2050. 

Hii inahitaji uwekezaji mkubwa katika sekta za uzalishaji, viwanda, kilimo cha kisasa, uchumi wa buluu, nishati, TEHAMA, pamoja na huduma zenye tija na thamani kubwa. Ni dhahiri kuwa Serikali pekee haiwezi kufanikisha malengo haya. Hivyo, ushiriki mpana wa sekta binafsi kwa njia ya uwekezaji katika uzalishaji wa bidhaa na huduma ni jambo lililopewa uzito na kuwekewa msisitizo mkubwa katika Dira 2050.

 Sekta binafsi haitarajiwi kutoa mchango kwa serikali bali itatoa mchango katika ukuzaji wa uchumi 4 kupitia uwekezaji wenye tija katika sekta mbalimbali.

 Uwekezaji huo unatarajiwa si tu kuipa faida sekta binafsi kupitia faida ya uwekezaji bali pia kutoa ajira kwa wananchi wakiwemo vijana. 

Ndugu Wageni Waalikwa, Tumeelezwa hapa kuwa MKUMBI II umeandaliwa kwa kuzingatia Dira 2050, pamoja na Mpango wa Nne wa Maendeleo wa Taifa, unaosisitiza mageuzi katika viwanda, kilimo chenye tija, uchumi wa buluu na uchumi wa kidijitali. 

Utekelezaji wa ajenda hizi unategemea kwa kiasi kikubwa urahisi na ubora wa mazingira ya uwekezaji na ufanyaji biashara katika ngazi zote.

 Ndugu Wageni Waalikwa, Takwimu zinaonesha wazi kuwa juhudi za maboresho ya mazingira ya biashara zimeanza kuleta matokeo chanya. 

Katika mwaka 2024 pekee, Tanzania ilisajili miradi ya uwekezaji 901 yenye thamani ya takribani Dola za Marekani bilioni 9.3 (sawa na zaidi ya Shilingi trilioni 21), na miradi hiyo ilitarajiwa kuzalisha zaidi ya ajira 212,000.

 Kwa kipindi cha miaka miwili ya 2024 hadi 2025, jumla ya miradi 1,828 yenye thamani ya takribani Dola bilioni 20.3 ilisajiliwa nchini. 

Serikali imeendelea kuwekeza kwa kiwango kikubwa katika miundombinu ya kimkakati ikiwemo reli ya kisasa, bandari, barabara, nishati na TEHAMA, ili kupunguzagharama za uzalishaji na kuongeza ushindani wa uchumi wetu. 

Ndugu Wageni Waalikwa, Mtakubaliana nami kuwa mazingira yetu ya biashara yameimarika tofauti na ilivyokuwa miaka ya nyuma. 

Kupitia utekelezaji wa MKUMBI, Maboresha ya mazingira ya biashara na uwekezaji yamefanyika ikiwemo: Kufanyika kwa mapitio ya sheria zaidi ya 94 na kufutwa na kupunguzwa kwa ada, tozo na kodi zaidi ya 628 zilizobainishwa.kuwa ni kikwazo katika sekta za Uwekezaji, Viwanda, Biashara, Madini, Kilimo, Mifugo, Uvuvi, Maliasili na Misitu.

 Vilevile, mwingiliano wa majukumu ya baadhi ya taasisi umeondolewa ili kupunguza vikwazo kwa wafanyabiashara; na mifumo ya kielektroniki imeunganishwa kwa lengo la kurahisisha upatikanaji wa huduma. 

Ndugu Wageni Waalikwa, Kwa upande wa Zanzibar, tumeendelea kushuhudia ukuaji wa sekta za kimkakati kama utalii, uchumi wa buluu, na huduma za kifedha, ambazo zinachangiwa na mazingira bora ya biashara yanayoimarika. Mafanikio haya yamepatikana kutokana na mbeba maono na uongozi mahiri wa Mheshimiwa.

 Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye ameendelea kutoa miongozo na maelekezo mbalimbali katika kuweka mazingira wezeshi ya uwekezaji na ufanyaji biashara nchini. 

Vilevile, mafanikio haya yamechagizwa na ushirikiano mzuri kati ya Serikali na Washirika wa Maendeleo, hususan Umoja wa Ulaya (EU). 

Nawashukuru sana kwa mchango wao mkubwa katika utekelezaji wa MKUMBI I na maandalizi ya MKUMBI II.

 Ndugu Wageni Waalikwa, Kwa kutambua kuwa Sekta Binafsi hususan Sekta Binafsi ya ndani ni nguzo muhimu ya ukuzaji wa uchumi, Mheshimiwa Rais, Wakati wa kufungua Bunge la 13 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tarehe 14 Novemba 2025 aliahidi kuendelea kuboresha zaidi mazingira ya biashara nchini kwa kukamilisha utekelezaji wa MKUMBI sambamba na kutekeleza mapendekezo ya Tume ya Rais ya Kuboresha Mifumo ya Kodi nchini ili kuwapatia wafanyabiashara wepesi katika kufanya biashara na kuwekeza.

Ndugu Wageni Waalikwa; mtakumbuka kuwa Mwezi April, 2025, tulizindua Maandalizi ya Mpango wa Pili wa Kuboresha Mazingira ya Biashara na Uwekezaji (MKUMBI II) sambamba na Kamati ya Kitaifa ya Wataalamu ya kuandaa Mpango huo.

 Pamoja na mambo mengine, Kamati hiyo ilipewa majukumu ya kuhakikisha MKUMBI II unaandaliwa kwa wakati na kwa kuzingatia ushirikishwaji wa wadau wote katika uwekezaji na biashara ikiwepo sekta binafsi ambayo ina nafasi ya kimkakati na ya msingi katika utekelezaji wa Dira 2050, kwani ndiyo injini kuu ya ukuaji wa uchumi kupitia uwekezaji, uzalishaji, ubunifu na utoaji ajira. 

Aidha, Kamati ilielekezwa kuhakikisha MKUMBI II unaweka vipaumbele katika utoaji wa huduma kwa haraka, ufanisi, na kwa kuzingatia viwango vya kimataifa, ili kuiwezesha Tanzania kuendelea kuongeza ushindani katika masoko ya kikanda na kimataifa. 

Ndugu waalikwa, kuhusu ushirikishaji wa Sekta binafsi, Kamati ilielekezwa kushirikisha sekta bianafsi ili iweze kutoa mapendekezo ambayo ni maboresho yanayohitajika ili nchi yetu iendelee kuwa kivutio kwa wawekezaji wa ndani na nje na hivyo kufikia malengo ya Dira 2050.

 Pia, Sekta binafsi iliaswa kuhakikisha kuwa wawekezaji na jumuiya za wafanyabiashara zinashirikishwa katika mchakato wa maandalizi ya MKUMBI-II kwa njia ya kupokea maoni ya wadau wote kwa uwakilishi (wafanyabiashara wakubwa na wadogo na wawekezaji wakubwa na wadogo) na kuhakikisha kwamba mapendekezo yao yanawasilishwa katika Kamati ya maandalizi ya MKUMBI-II. 

Ndugu Wageni Waalikwa, napenda kuwajulisha kuwa Kamati imekamilisha kazi ya kuandaa Rasimu ya MKUMBII II baada ya kupokea maoni kutoka kwa wadau wa sekta binafsi pamoja na sekta ya umma na kwa kuzingatia miongozo iliyotolewa wakati wa Uzinduzi wa Maandalizi ya MKUMBI II na Kamati yake. Ni matumaini yangu kuwa sehemu kubwa ya mliopo hapa mlipata fursa ya kutoa maoni katika Rasimu iliyoandaliwa.

 Ndugu Wageni Waalikwa, Tumekutana hapa leo ili kujiridhisha na kuthibitisha maoni yaliyotolewa na kuchambuliwa yamezingatiwa katika rasimu hii itakayowasilishwa leo ambayo ni ya mwisho. 

Hivyo naomba kutoa rai kwenu nyote kuwa huru na kutumia nafasi hii katika kuhakiki maoni yaliyotolewa katika rasimu hii. Kamati ya wataalamu itawapatia utaratibu mzuri wa kuhakiki maoni yaliyotolewa na wadau mbalimbali katika rasimu hiyo na kuiboresha.

 Ndugu Wageni Waalikwa, Napenda kusisitiza kuwa mafanikio ya MKUMBI II yatategemea kwa kiasi kikubwa ushirikiano kati ya sekta ya umma na sekta binafsi. 

Hivyo ni wajibu wetu kuhakikisha kuwa sekta binafsi inawezeshwa kwa kufanya kazi katika mazingira rafiki, yenye uwazi nayanayotabirika.

 Vilevile, ni muhimu kuendelea kuimarisha miundombinu, huduma za kifedha, na matumizi ya teknolojia za kisasa ili kuongeza ushindani wa biashara zetu kikanda na kimataifa. Vilevile, tunapaswa kuweka mifumo madhubuti ya ufuatiliaji na tathmini ili kuhakikisha utekelezaji wa mpango huu unaleta matokeo yaliyokusudiwa. 

Ndugu Wageni Waalikwa, Kwa upande wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, tunaendelea kuwa na dhamira ya dhati ya kushirikiana na wadau wote katika kujenga mazingira bora zaidi ya biashara na uwekezaji kwa manufaa ya wananchi wetu na Taifa kwa ujumla. Mwisho, nawahimiza washiriki wote kutumia kikamilifu warsha hii kwa kutoa Maoni, uzoefu na mapendekezo yatakayosaidia kuboresha mpango huu.

Baada ya kusema hayo, napenda kutamka rasmi kuwa ‘WARSHA YA UHAKIKI WA RASIMU YA MPANGO WA PILI WA KUBORESHA MAZINGIRA YA BIASHARA NA UWEKEZAJI IMEFUNGULIWA RASMI’.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo akitoa neno la kumkaribisha Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Dkt. Mwinyi.

Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji (Uwekezaji), Dkt. Fred Msemwa akiwatambulisha viongozi na wageni waalikwa walioshiriki mkutano huo.


Waziri Prof. Mkumbo (katikati) akijadiliana jambo na Mwenyekiti wa Kamati ya NTT-MKUMBI II, Prof. Faustine Kamuzora (kushoto) na Katibu Mkuu Uwekezaji, Dkt. Msemwa.












Mwenyekiti wa Kamati ya MKUMBI II, Prof. Kamuzora akiwa na wajumbe wa kamati hiyo wakiwa na furaha baada ya mkutano huo kufunguliwa.na Rais Dkt. Mwinyi.

IMEANDALIWA NA RICHARD MWAIKENDA-0754264203



No comments:

Post a Comment

Tupia Comments👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages