SEKTA binafsi ambayo ina nafasi ya kimkakati na ya msingi katika utekelezaji wa Dira 2050, ndiyo injini kuu ya ukuaji wa uchumi kupitia uwekezaji, uzalishaji, ubunifu na utoaji ajira nchini.
Hayo yameelezwa na Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Dkt. Hussein Ali Mwinyi alipokuwa akifungua Mkutano wa Uhakiki wa Rasimu ya Mpango wa Pili wa Kuboresha Mazingira ya Biashara na Uwekezaji (MKUMBI II) kwenye Ukumbi wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere Dar es Salaam Machi 27, 2026.
“Mtakumbuka kuwa Mwezi April, 2025, tulizindua Maandalizi ya Mpango wa Pili wa Kuboresha Mazingira ya Biashara na Uwekezaji (MKUMBI II) sambamba na Kamati ya Kitaifa ya Wataalamu ya kuandaa Mpango huo.”
“Pamoja na mambo mengine, Kamati hiyo ilipewa majukumu ya kuhakikisha MKUMBI II unaandaliwa kwa wakati na kwa kuzingatia ushirikishwaji wa wadau wote katika uwekezaji na biashara ikiwepo sekta binafsi ambayo ina nafasi ya kimkakati na ya msingi katika utekelezaji wa Dira 2050, kwani ndiyo injini kuu ya ukuaji wa uchumi kupitia uwekezaji, uzalishaji, ubunifu na utoaji ajira.” Alisisitiza Rais Dkt. Mwinyi.
Aidha, Kamati ilielekezwa kuhakikisha MKUMBI II unaweka vipaumbele katika utoaji wa huduma kwa haraka, ufanisi, na kwa kuzingatia viwango vya kimataifa, ili kuiwezesha Tanzania kuendelea kuongeza ushindani katika masoko ya kikanda na kimataifa.
Kuhusu ushirikishaji wa Sekta binafsi, Rais Dkt. Mwinyi amesema kuwa Kamati ilielekezwa kushirikisha sekta bianafsi ili iweze kutoa mapendekezo ambayo ni maboresho yanayohitajika ili nchi yetu iendelee kuwa kivutio kwa wawekezaji wa ndani na nje na hivyo kufikia malengo ya Dira 2050.
Pia, Sekta binafsi iliaswa kuhakikisha kuwa wawekezaji na jumuiya za wafanyabiashara zinashirikishwa katika mchakato wa maandalizi ya MKUMBI-II kwa njia ya kupokea maoni ya wadau wote kwa uwakilishi (wafanyabiashara wakubwa na wadogo na wawekezaji wakubwa na wadogo) na kuhakikisha kwamba mapendekezo yao yanawasilishwa katika Kamati ya maandalizi ya MKUMBI-II.
Rais Dkt. Mwinyi aliwajulisha washiriki wa mkutano huo kuwa Kamati imekamilisha kazi ya kuandaa Rasimu ya MKUMBII II baada ya kupokea maoni kutoka kwa wadau wa sekta binafsi pamoja na sekta ya umma na kwa kuzingatia miongozo iliyotolewa wakati wa Uzinduzi wa Maandalizi ya MKUMBI II na Kamati yake.
“Ni matumaini yangu kuwa sehemu kubwa ya mliopo hapa mlipata fursa ya kutoa maoni katika Rasimu iliyoandaliwa. Ndugu Wageni Waalikwa, Tumekutana hapa leo (jana) ili kujiridhisha na kuthibitisha maoni yaliyotolewa na kuchambuliwa yamezingatiwa katika rasimu hii itakayowasilishwa ambayo ni ya mwisho.”
“Hivyo naomba kutoa rai kwenu nyote kuwa huru na kutumia nafasi hii katika kuhakiki maoni yaliyotolewa katika rasimu hii. Kamati ya wataalamu itawapatia utaratibu mzuri wa kuhakiki maoni yaliyotolewa na wadau mbalimbali katika rasimu hiyo na kuiboresha.”
“Napenda kusisitiza kuwa mafanikio ya MKUMBI II yatategemea kwa kiasi kikubwa ushirikiano kati ya sekta ya umma na sekta binafsi. Hivyo ni wajibu wetu kuhakikisha kuwa sekta binafsi inawezeshwa kwa kufanya kazi katika mazingira rafiki, yenye uwazi na yanayotabirika. “
Rais Dkt. Mwinyi alimalizia kusema kwa kutilia umuhimu kuendelea kuimarisha miundombinu, huduma za kifedha, na matumizi ya teknolojia za kisasa ili kuongeza ushindani wa biashara zetu kikanda na kimataifa. Vilevile, tunapaswa kuweka mifumo madhubuti ya ufuatiliaji na tathmini ili kuhakikisha utekelezaji wa mpango huu unaleta matokeo yaliyokusudiwa.
No comments:
Post a Comment
Tupia Comments👇