UNAWEZA KUSEMA MBUYU WA SIASA UMEANGUKA TANZANIA, kwani William Vangimembe Lukuvi ndiye aliyekuwa mbunge mkongwe kuliko wote katika Bunge la 13 linaloendelea sasa na waziri mwenye uzoefu mkubwa kuliko wengine.
Waziri Lukuvi aliyeingia bungeni tangu mwaka 1995 aligombea na kushinda ubunge mfululizo kwa vipindi saba. Pia amekuwa waziri katika maeneo tofauti mpaka alipofariki Machi 25, 2026.
Taarifa iliyotolewa na Rais Samia Suluhu Hassan kupitia taarifa ya Katibu Mkuu Kiongozi, Dk Moses Kusiluka Machi 25, 2026, imesema kifo cha Lukuvi aliyekuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu) na Mbunge wa Isimani, amefariki dunia majira ya saa moja asubuhi katika Hospitali ya Benjamin Mkapa, jijini Dodoma alipokuwa akipatiwa matibabu ya ugonjwa wa mshtuko wa moyo.
Wasifu wake
William Vangimembe Lukuvi alizaliwa Agosti 15, 1955 alikuwa mwanasiasa mkongwe wa Tanzania (CCM) na Mbunge wa muda mrefu wa Ismani tangu 1995.
Aliingia bungeni mwaka 1995 na kwa kipindi chote hicho amekuwa Mbunge kwa miaka 31.
Lukuvi ambaye kitaaluma ni mwalimu, alianza safari yake ya siasa katika Umoja wa Vijana wa CCM, akiwa katibu wa Wilaya za Masasi, Mtwara, Arusha na Dodoma.
Pia aliwahi kuwa Mjumbe wa Baraza Kuu na kamati ya utekelezaji ya Taifa ya UVCCM, kabla ya kuwa mkuu wa idara ya Oganaizesheni.
Nafasi nyingine alizoshika UVCCM ni pamoja na kuwa Katibu Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam na baadaye kuwa Naibu Katibu Mkuu wa jumuiya hiyo kitaifa.
Mbali na UVCCM, amewahi pia kuwa mjumbe wa Halmashauri kuu ya Wilaya, mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Mkoa, amewahi kuwa mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC), Mjumbe wa Kamati Kuu na Mjumbe wa Kamati ya Maadili Taifa.
Katika Serikali, aliteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Bukoba mkoani Kagera mwaka 1994 na baada ya kushinda ubunge mwaka 1995 aliteuliwa kuwa Naibu Waziri Kazi na Maendeleo ya Vijana, nafasi aliyoshika hadi mwaka 2000.
Mwaka 2000 hadi 2005, aliteuliwa kuwa Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu na mwaka 2005 aliteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa kwanza wa Dodoma na baadaye Dar es Salaam akiwa pia mbunge.
Baada ya uchaguzi wa 2010 alirejeshwa Ofisi ya Waziri Mkuu hadi mwaka 2014 na baada ya hapo aliteuliwa kuwa Waziri wa Ardhi, nafasi aliyoendelea nayo hadi Januari 2022 alipoenguliwa, hata hivyo bado anaendelea kuwa Mbunge.
Atemwa ujumbe NEC
Mwaka 2022 haukuwa mzuri kwa Lukuvi, kwani licha ya kupoteza uwaziri, aliangushwa pia kwenye ujumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM (NEC).
Hata hivyo, alisema licha ya kushindwa kwenye kinyang’anyiro cha ujumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC), kura alizopata ni za heshima na ujasiri.
Mbali na Lukuvi, wabunge wengine walioangushwa kwenye kura hizo walikuwa pamoja na Jerry Silaa (Ukonga), Deodatus Mwanyika (Njombe), Daniel Nsanzugwanko (Kasulu Mjini), Japhet Hasunga (Vwawa) na Abbas Tarimba (Kinondoni).
Pia, Waziri wa Sera, Bunge na Uratibu, George Simbachawene na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Jumanne Sagini nao walishindwa.
Alizungumza na gazeti la Mwananchi kuhusu anguko hilo, Lukuvi alisema katika uchaguzi kuna kushinda na kushindwa, hivyo anawashukuru wajumbe wa Mkutano Mkuu kwa kura walizompa.
“Utamaduni wa chaguzi ndani ya chama chetu mimi naujua una majibu mawili tu, kuna kushinda na kushindwa. Mimi kura zangu hazikutosha safari hii, lakini nimepata kura za heshima, hazikushinda kwa ile margin, maana nimekosa kura 11, lakini ni kura za heshima,” alisema.
Utata wa elimu
Lukuvi aliwahi kuingia kwenye orodha ya vigogo serikalini wenye zelimu zenye utata, huku ikidaiwa kuwa baadhi ya vyuo walivyosema havikuwa vikitambuliwa na mamlaka husika.
Mwenyewe hakuwahi kujibu lolote, lakini taarifa zake kwenye tovuti ya Bunge la Jamhuri ya Muungano ilionyesha kuwa alianza elimu ya msingi katika Shule ya Msingi ya Kitanewa mkoani Iringa mwaka 1962 hadi 1970 na baadaye kujiunga na Chuo cha Ualimu cha Tabora mwaka 1974 hadi mwaka 1975 na kupata cheti.
Mwaka 1982 hadi 1983 alipata stashahada ya Sayansi ya siasa katika Chuo cha Komsomol High School, kilichopo Moscow nchini Russia na mwaka 1999 hadi 2001 alipata shahada ya kwanza katika Chuo Kikuu cha Washington International na mwaka 2008 hadi 2011 alisoma shahada ya uzamivu ya sayansi ya siasa katika Chuo Kikuu Huria cha Tanzania.
Arejeshwa barazani
Agosti 14, 2024 William Lukuvi na Profesa Palamagamba Kabudi walirejeshwa katika Baraza la Mawaziri, baada ya kukaa nje kwa takriban miaka miwili tangu Januari 2022, kipindi ambacho Rais Samia Suluhu Hassan alieleza kuwa aliwaweka kando kwa "kazi maalumu" na kama washauri wake wa karibu.
Safari ya mwisho
Kutokana na umri kwenda na kukaa muda mrefu bungeni, ilidhaniwa mwaka 2025, Lukuvi hatagombea ubunge, lakini haikuwa hivyo.
Miongoni mwa vijana waliotarajiwa kurithi mikoba yake ni aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Monduli Mkoa wa Arusha, Festo Kiswaga.
Akizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa Lumilo Hotel, Manispaa ya Iringa Juni 3, 2025, Kiswaga alitangaza nia ya kugombea ubunge katika jimbo la Isimani akisema amepata wito wa wananchi wa Isimani na nafasi iliyojitokeza baada ya Mbunge wa sasa, William Lukuvi, kutangaza mwaka 2020 kuwa hatogombea tena ifikapo uchaguzi wa mwaka huu.
“Nina dhamira ya dhati kulitumikia Jimbo la Isimani. Mheshimiwa Lukuvi mwenyewe alitangaza kuwa hatagombea tena mwaka 2025, na ninasimama kwa ujasiri mkubwa kuchukua kijiti na kuendeleza maendeleo,” alisema Kiswaga mbele ya waandishi wa habari.
Akiendelea kufafanua, Kiswaga alisema kuwa mwaka 2022 aliitwa na Lukuvi jijini Dodoma, ambapo walizungumza kwa kina, na Lukuvi alimueleza kuwa amehudumu kwa zaidi ya miaka 30 na hatakuwa tena kwenye kinyang’anyiro cha ubunge.
“Kama ni kweli kwamba anapenda maendeleo ya Jimbo hili, basi kwa maslahi mapana ya wananchi wa Isimani, ni vyema akaheshimu kauli yake na kustaafu kwa hiari. Vinginevyo, wananchi wamesema wako tayari kumstaafisha kwa lazima kupitia sanduku la kura,” aliongeza Kiswaga.
Licha ya cheche za Kiswaga, katika kura za maoni za CCM zilizofanyika Agosti 2025, Lukuvi alishinda kwa kupata jumla ya kura 5,746 huku mpinzani wake Kiswaga, akipata kura 1,159 tu.
Baada ya kurudi bungeni Oktoba 2025, Rais Samia alimteua Lukuvi kuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu.
Akizungumza wakati wa zoezi la kuwapokea Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu na Naibu Waziri wa Ofisi hiyo katika Ofisi za Waziri Mkuu Ngome, Novemba, 18 2025 Jijini Dodoma, Lukuvi alimshukuru Rais Samia kwa kumuamini na kumrudisha kwenye wizara hiyo.

No comments:
Post a Comment
Tupia Comments👇