Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, akihutubia katika hafla ya kufungua mwaka mpya 2026 pamoja na Mabalozi wanaowakilisha nchi zao Tanzania, wawakilishi wa heshima, na Wakuu wa mashirika ya kimataifa katika hafla iliyofanyika Ikulu Chamwino ameeleza kuwa Tanzania imefanikisha Uchaguzi wa 7 wa kidemokrasia, uliofanyika Oktoba 29, 2025
Rais Samia ameongeza kuwa Uchaguzi huo ulifadhiliwa kikamilifu kupitia rasilimali za ndani, jambo linalothibitisha umiliki wa kitaifa, ukomavu wa Kitaasisi, na dhamira ya Serikali ya kujitegemea katika kusimamia mchakato wa kidemokrasia.
Rais Samia pia alikiri changamoto zilizotokea kutokana na vurugu na ukosefu wa utulivu siku ya uchaguzi na muda mfupi baada yake, akisema:
“Licha ya mafanikio haya makubwa, kwa masikitiko tunatambua changamoto zilizotokea kutokana na vurugu na ukosefu wa utulivu siku ya uchaguzi na muda mfupi baada yake. Hatua tulizochukua zilikuwa muhimu ili kudumisha utaratibu wa Kikatiba na kuhakikisha usalama wa Wananchi wote pamoja na Jamii ya Kidiplomasia.”
Aidha, Rais Samia akiwapa pole Washirika wa Kidiplomasia na wageni wanaoishi nchini kutokana na changamoto waliokumbana nazo alisema:
“Kwa Washirika wetu katika Jamii ya Kidiplomasia na wageni wanaoishi hapa nchini Tanzania, ninatoa pole ya dhati kutokana na hali ya kutokuwa na uhakika, usumbufu wa huduma, na kufungwa kwa mtandao wa intaneti. Nawaahidi kuwa tunakuwa makini kuhakikisha usalama wenu na kuzuia hali kama hiyo kujirudia katika siku zijazo.”

No comments:
Post a Comment
Tupia Comments👇