LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Dec 18, 2025

MSIGWA AWAASA TBN NA JUMIKITA KUWA MASHUJAA WA KUILINDA NCHI YAO, SIYO WA KUIBOMOA

CCB Blog, Dar es Salaam
Waandishi wa habari wakiwemo Tanzania Bloggers Network (TBN) na Jukwaa la Mitandao Tanzania (JUMIKITA) wametakiwa kuwa  mashujaa wa kujenga nchi yao na siyo kuwa mashujaa wa kuibomoa kwa namna yoyote, huku wakiaswa kuyafanya majukwaa yao ya Blogu na mitandao mimgine ya kijamii yawe ya kutetea na kulinda maslahi ya taifa, amani na utulivu nchini.

"Waandishi muwe mashujaa wa kujenga nchi yenu siyo mashujaa wa kubomoa nchini yenu na pia majukwaa yenu ya Blogu na mitandao mingine ya kijamii yawe ya kutetea na kulinda maslahi ya taifa, utulivu na amani katika nchi yenu", amesema hayo Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa Serikali.

Amesema kwa kutambua teknolojia ya mawasiliano ya habari kwa njia ya mtandao katika zama hizi yana nguvu kubwa katika kulijenga au kulibomoa taifa lolote, Serikali ya Awamu ya Sita imeendelea kuimarisha ushirikiano na Mabloga na Waandishi wengine wa habari wakiwemo wa mitandaoni kwa lengo la kujenga tasnia ya habari iliyo imara, yenye weledi na inayolinda maslahi ya taifa.

Msigwa aliyekuwa akizungumza wakati akifunga kikaokazi baina ya Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Dk. Jabir Bakari, na Wanachama wa Tanzania Bloggers Network (TBN) na Jukwaa la Mitandao Tanzania (JUMIKITA) kilichofanyika leo jijini Dar es Salaam, amesema, Serikali imechagua mkondo wa kushirikiana na kutengeneza maudhui ya habari badala ya kuwachukulia hatua za adhabu, kwa kuwa imajua  mitandao ya kijamii imekuwa sehemu muhimu ya mawasiliano ya kisasa na ujenzi wa taifa.

Amesema katika dunia ya sasa, mapambano mengi yamehama kutoka kwenye matumizi ya silaha za kivita kama vifaru, mabomu na bunduki na kwenda kwenye uwanja wa taarifa, hali inayofanyakazi ya waandishi wa habari kuwa nyeti kwa mustakabali wa nchi.

Msigwa aliipongeza Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kwa mwelekeo wake wa kulea wadau wa sekta ya habari, akisema hatua hiyo imeongeza imani kati ya serikali na waandishi wa habari wa mitandaoni. Pia alitaja TBN na JUMIKITA kuwa ni wadau wakubwa wa serikali katika kusambaza taarifa sahihi kwa umma.

Aliwahakikishia waandishi wa habari ulinzi wa serikali, akieleza kuwa endapo sheria, kanuni au sera zitabainika kuwa kikwazo katika utekelezaji wa majukumu yao, serikali iko tayari kuzifanyia marekebisho kwa maslahi mapana ya taifa.

Msigwa alidokeza kuwa hadi sasa serikali kwa kushirikiana na TCRA na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ipo katika maandalizi ya kutoa mafunzo maalum kwa waandishi wa habari wa mitandaoni na kuandaa mikakati ya kuwawezesha kiuchumi ikiwemo njia ya mikopo.

Kuhusu masuala ya kodi, Msigwa alisema serikali itaendelea kushirikiana na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ili kutatua changamoto zinazowakabili Mabloga na Waandishi wa habari wa mitandaoni, huku ikitambua mchango wao mkubwa katika kuitangaza Tanzania na kuvutia wawekezaji.

Aidha, Msigwa aliwataka waandishi wa habari kutumia majukwaa yao kwa uzalendo, uwajibikaji na weledi, akisisitiza kuwa serikali inawaona kama washirika muhimu katika ujenzi wa taifa na kuimarisha demokrasia.

Mapema, akizungumza katika kikaokazi hicho, Dk. Bakari alijibu maswali mbalimbali ikiwemo kwa nini Serikali huchukua hatua ya kufunga mitandao ya kijamii, ilhali inawafahamu wanaoweka picha au kuandika taarifa zinazozusha taharuki na uvunjifu wa amani, alisema; Wakati mwingine tunalazimika kufunga mitandao kwa sababu tunapoongea na wamiliki wa mitandao hiyo kimataifa, hutuambia kwamba tunayoyalalamikia hayamo kwenye sera zao kisheria kuweza kumfungia mteja wao."

Sasa ukitazama kwamba wakati sera zao wao zinaruhusu mambo ambayo kwetu, kitaifa, kijamii na kwa usalama wa nchi yetu hayatakiwi kisheria, basi ndiyo hulazimika kufunga tu, lakini tukijua athari zake kiuchumi hasa ninyi mnaotumia mitandao hiyo kuingiza kipato".

Kaba ya Dk. Bakari kuzungumza Viongozi wa TBN na JUMIKITA walipata nafasi ya kueleza hali, masimamo na matumaini yao kwa serikali ili wanachama wao waweze kufanyakazi kwa ari na kujituma bila kukabiliwa na vikwazo vikiwemo vya kanuni, sheria na kodi.

Kusoma Taarifa ya Mwenyekiti wa TBN Beda Msimbe, Tafadhali Bofya👉 HAPA



Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa Serikali, akizungumza wakati akifunga kikaokazi baina ya Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Dk. Jabir Bakari (Wapili kushoto) na Wanachama wa Tanzania Bloggers Network (TBN) na Jukwaa la Mitandao Tanzania (JUMIKITA), kilichofanyika leo jijini Dar es Salaam, Kushoto ni Mwenyekiti wa TBN Beda Msimbe.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa Serikali, akizungumza wakati akifunga kikaokazi baina ya Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Dk. Jabir Bakari (Wapili kushoto) na Wanachama wa Tanzania Bloggers Network (TBN) na Waandishi wa habari za mitandaoni (JUMIKITA), kilichofanyika leo jijini Dar es Salaam,
Mwenyekiti wa TBN Beda Msimbe akizungumza katika kikaokazi hicho.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Dk. Jabir Bakari, akizungumza wakati akifungua kikaokazi hicho






No comments:

Post a Comment

Tupia Comments👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages