LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Dec 23, 2025

MICHUANO YA AFCON: TANZANIA KUISHANGAZA NIGERIA LEO?

Tanzania (Taifa Stars) inaanza kampeni yake ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2025) leo kwa mtihani mzito dhidi ya vigogo Nigeria, kabla ya kuwakabili Uganda siku nne baadaye na kisha kumaliza hatua ya makundi dhidi ya Tunisia tarehe 30 Desemba.

Nigeria na Tanzania zitakutana katika AFCON kwa mara ya pili. Mechi pekee waliyokutana awali kwenye fainali hizi ulikuwa mwaka 1980, wakati Nigeria walipoifunga Tanzania 3-1 katika mechi ya ufunguzi huko Lagos, kabla ya kutwaa ubingwa wao wa kwanza wa Afrika.

Kwa ujumla, timu hizo zimekutana mara nane katika mashindano yote. Nigeria hawajawahi kufungwa na Tanzania, wakishinda mechi tano na kutoka sare tatu.

Michezo yao waliyokutana hivi karibuni ilikuwa katika kufuzu AFCON 2017, walitoka sare ya 0-0 Dar es Salaam kabla ya Nigeria kushinda 1-0 mjini Uyo.

Chini ya kocha Miguel Gamondi, Taifa Stars wamewasili kwenye fainali hizi wakiwa na mchanganyiko wa wachezaji wanaocheza nje ya nchi na nyota wa ndani kutoka klabu kubwa za Tanzania Simba SC, Yanga na Azam FC.

Huu ni ushiriki wa nne wa Tanzania katika AFCON, ikiwa ni mara ya pili mfululizo kufuzu.

Tanzania wamepangwa Kundi A linalotajwa kuwa moja ya magumu zaidi, likiwajumuisha Nigeria, Tunisia na majirani Uganda.

Takwimu za Tanzania AFCON


Nahodha wa Tanzania, Mbwana Samatta

Tanzania ilifuzu fainali za AFCON kwa mara ya kwanza mwaka 1980, kabla ya kurejea tena mwaka 2019. Mafanikio ya karibuni yameifanya Taifa Stars kufuzu mfululizo kwa mara ya kwanza katika historia yao AFCON 2023 na 2025.

Hata hivyo, rekodi yao katika fainali za AFCON bado haivutii. Tanzania haijawahi kushinda hata mechi moja katika mashindano hayo, ikicheza mechi 9 za makundi bila ushindi.

Katika fainali za AFCON 1980 zilizofanyika Nigeria, Tanzania ilikuwa Kundi B pamoja na wenyeji Nigeria, Misri na Ivory Coast. Walifungwa 3-1 na Nigeria katika mechi ya ufunguzi, wakapoteza 2-1 dhidi ya Misri, kabla ya kutoka sare ya 1-1 dhidi ya Ivory Coast. Walimaliza mkiani mwa kundi kwa alama moja na wakaaga mashindano mapema.

Tanzania pia ina rekodi ya kupoteza mechi zote tatu za awali za ufunguzi wa AFCON. Sare ya 0-0 dhidi ya DR Congo mwaka 2023 ndiyo ilikuwa mara yao pekee kutofungwa bao katika fainali za AFCON. Kwa ujumla, wamefunga bao moja tu katika mechi zao nne za mwisho za AFCON.

Katika kufuzu AFCON 2025, Simon Msuva na Feisal Salum walikuwa wafungaji bora wa Taifa Stars, kila mmoja akifunga mabao mawili.

Takwimu za Nigeria


Nigeria wanashiriki fainali zao za 21 za AFCON na ni moja ya mataifa yenye historia kubwa zaidi barani Afrika. Wametwaa ubingwa mara tatu 1980, 1994 na 2013 na wamekuwa washindi wa pili mara tano, ikiwemo fainali ya mwaka 2023.

Super Eagles wametolewa katika hatua ya makundi mara mbili pekee katika historia yao yote ya AFCON. Tangu mwaka 1988, wamefika angalau nusu fainali katika mashindano 13 kati ya 15.

Katika mechi za makundi, Nigeria wamepoteza mchezo mmoja tu kati ya mechi 14 zilizopita za AFCON, na hawajashindwa katika mechi zao tatu za mwisho za ufunguzi.

Mechi hii dhidi ya Tanzania itakuwa ya 105 kwa Nigeria katika historia ya AFCON, wakiwa miongoni mwa timu zilizocheza mechi nyingi zaidi katika mashindano hayo. Kwa jumla, wamefunga mabao 146 kwenye AFCON.

Katika kufuzu, Nigeria walipita bila kupoteza mechi, wakishinda nne na kutoka sare mbili. Ademola Lookman na Victor Osimhen waliongoza safu ya ushambuliaji kwa kufunga mabao mawili kila mmoja.

Nigeria wanaongozwa na kocha Éric Chelle, aliyeteuliwa Januari, ambaye aliwahi kuipeleka Mali hadi robo fainali katika AFCON 2023.


Je, Tanzania wanaweza kuvunja mwiko?

Tanzania bado wanasaka ushindi wao wa kwanza kabisa katika historia ya AFCON. Ingawa wanatajwa kuwa timu ndogo ukilinganisha na Nigeria, maendeleo ya hivi karibuni na uzoefu wa wachezaji kadhaa wanaocheza nje ya nchi vinatoa matumaini mapya.

Nahodha Mbwana Samatta anaiongoza timu baada ya kurejesha kiwango chake akiwa na klabu ya Le Havre nchini Ufaransa. Samatta ndiye Mtanzania pekee aliyewahi kucheza Ligi Kuu England, na amefunga mabao 22 akiwa na Taifa Stars, ikiwemo bao lake la kwenye fainali za AFCON 2019.

Mshambuliaji mwenye uzoefu Simon Msuva, kwa sasa akicheza Iraq, pamoja na nyota wa Ligi Kuu Tanzania Bara kama Feisal Salum, Pascal Msindo, Yakoub Suleiman na Mohammed Hussein, nao wanabeba matumaini ya taifa. Vipaji chipukizi kama Kelvin Nashon na Novatus Dismas pia vimejumuishwa kikosini., wakicheza soka nje ya nchi.

"Tunawaheshimu Nigeria lakini hatuwaogopi", anasema Kibu Denis mmoja wa nyota wa kutegemewa Tanzania.

Kwa upande mwingine, Nigeria wana kikosi kilichojaa nyota wa soka la Afrika. Ademola Lookman, mchezaji bora wa Afrika 2024, pamoja na Victor Osimhen aliyefunga mabao 31 katika mechi 45 za kimataifa wanabaki kuwa tishio kubwa kwa Tanzania. Wachezaji kama Calvin Bassey, Alex Iwobi na Samu Chukwueze pia wanatarajiwa kuanza mchezo huo.

Kwa kuzingatia historia na ubora wa vikosi, Nigeria wanaingia kama wababe wa mchezo huu. Hata hivyo, soka la Afrika limejaa matokeo ya kushtua, na Tanzania wataingia uwanjani wakitafuta kuandika historia mpya.

Je, Taifa Stars wanaweza kuvunja mwiko wao wa AFCON leo? na kupata ushindi wa kwanza dhidi ya vigogo hao wa Afrika?



 

No comments:

Post a Comment

Tupia Comments👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages