LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Dec 19, 2025

JINSI MIRADI YA KIMKAKATI YENYE THAMANI YA SH 4.15 TRILIONI ITAKAVYOMALIZA SHIDA YA MAJI NCHINI

 Na Pius Ntiga,

Mwaka 2021, Rais Dkt, Samia Suluhu Hassan alipoahidi ‘kumtua mwanamke ndoo ya maji kichwani,’ maneno yake yaliashiria mabadiliko makubwa katika sera ya maji nchini. 

Maono hayo sasa yanaanza kutimia, huku serikali ikiwekeza kwa kiasi kikubwa katika upatikanaji wa maji kupitia miradi zaidi ya 100 kote nchini.

Kati ya miradi hiyo, hii hapa 25 yenye thamani ya Sh4.15 trilioni ikiwa imebuniwa mahsusi kushughulikia uhaba wa maji kwa kudumu, siyo tu mijini bali hata vijijini, kulingana na takwimu kutoka Wizara ya Maji.

Miradi hii inalenga kupunguza mzigo mkubwa ambao wanawake na watoto kwa muda mrefu wameubeba ambapo serikali inalenga kufikia 95% mijini na 85% vijijini ifikapo mwaka 2030.

Tukianza na mradi wa Maji Arusha, unaogharimu Sh520 bilioni, unafaidi wakazi 850,000 kwa kuzalisha lita milioni 200 kila siku. 

Ukikamilika, upatikanaji wa maji mijini utaongezeka hadi asilimia 91.6, huku vijijini wakifikia asilimia 83.

Katika mikoa ya Kilimanjaro na Tanga, Mradi wa Same–Mwanga–Korogwe wenye thamani ya Sh406 bilioni unahudumia wakazi 300,000 kwa kutoa lita milioni 51.65 kila siku.

Pia mradi wa Bwawa la Kidunda, mkoani Morogoro lenye thamani ya Sh335 bilioni, ambalo litahudumia watu milioni 6.77 kwa kuhifadhi lita bilioni 190 na kudumisha mtiririko wa Mto Ruvu, jambo linaloongeza usambazaji wa maji Dar es Salaam na Mkoa wa Pwani.

Aidha, Mradi wa Tabora–Nzega–Igunga–Singida, wenye thamani ya Sh602 bilioni, utaletea wananchi 1.2 milioni lita milioni 54.1 kila siku.

Miradi mingine ya kimkakati na yenye manufaa imeendelea kufanya ikilenga maeneo mahususi yaliyokuwa na kero ya maji kwa muda mrefu kama Mradi wa Bunda wa Sh29.5 bilioni na Mradi wa Kintinku–Lusilile wa Sh13 bilioni, pia inahudumia wakazi wa vijiji na miji midogo, ikitoa maji mamilioni ya lita kila siku, kwa ajili ya kuzisaidia jamii zinazoizunguka miradi hiyo.

Sambamba na hilo, awamu ya kwanza ya Mradi wa Ziwa Victoria–Dodoma–Singida, unaogharimu Sh326 bilioni, inalenga wakazi 1.5 milioni kwa kutoa lita milioni 200 kila siku.

Kwa mkoa wa Mara kuna mradi wa wa Mgango–Kiabakari–Butiama katika mkoa wa Mara, wenye Sh70.9 bilioni, unazalisha lita milioni 2 kila siku, ukihudumia vijiji 13.

Chalinze Awamu ya tatu, ikifadhiliwa na India kwa Sh96 bilioni, tayari imekamilika kwa asilimia 96, ikihudumia zaidi ya wakazi 200,000 Chalinze, Handeni na sehemu za Morogoro, huku uzalishaji wa maji kila siku ukiongezeka kutoka lita 500,000 hadi milioni 2.

Kusini mwa Tanzania, miradi ya Mtwara yenye thamani ya Sh87 bilioni itatoa lita milioni 40 kila siku kwa wakazi 600,000, huku Mradi wa Ruangwa–Nachingwea, Lindi, wa Sh119 bilioni ukihudumia wakazi 200,000 kwa lita milioni 15 kila siku, ukikabiliana na changamoto ya maji yenye chumvi.

Aidha, mijini, Mradi wa Kigamboni Awamu ya pili wa Sh65 bilioni utahudumia wakazi 250,000 kwa kutoa lita milioni 20 kila siku kupitia visima saba vya kina, bwawa la kuhifadhi lita milioni 15 na mtandao wa usambazaji wa kilomita 20.

Mwanza pia inafaidika na Mradi wa Butimba, wenye Sh71 bilioni, utakaotoa lita milioni 48 kila siku kwa wakazi 450,000 ifikapo mwaka 2025, ukiungwa mkono na AFD, EIB, na EU-Africa Infrastructure Trust Fund.

Miradi mingine mijini ikiwemo Chamwino, Nanyumbu, Kigoma, Chato, Makambako na Singida inazalisha kati ya litri milioni 3 hadi 15 kila siku, kuhakikisha mijini na miji midogo inapata maji kwa uhakika.

Baadhi ya miradi imeundwa kwa kuzingatia mabadiliko ya tabianchi, mradi wa Simiyu, wenye thamani ya Sh500 bilioni, utahudumia wakazi 495,000 pamoja na watu 2.5 milioni wanaotegemea huduma hiyo, ukitoa litri milioni 30 kila siku. 

Morogoro pia inapata mradi wa Sh185 bilioni unaoendeleza Bwawa la Mindu na kujenga kiwanda kipya cha matibabu ya maji Mafiga, kuongeza uzalishaji hadi lita milioni 89 kila siku.

Kwa ujumla, miradi hii mikubwa inalenga kuhakikisha kwamba uhaba wa maji unakuwa historia, katika serikali ya awamu ya sita, muhula wa pili chini ya Rais Dkt, Samia Suluhu Hassan, huku ikipunguza mzigo mkubwa ambao kwa muda mrefu umekuwa wa wanawake na watoto.




No comments:

Post a Comment

Tupia Comments👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages