Waziri wa Kilimo, Mhe. Daniel Chongolo (Mb), ameitaka miradi ya kilimo ikiwemo miradi ya umwagiliaji kuongeza tija na uzalishaji wa mazao ili kuwakomboa wakulima kiuchumi.
Waziri Chongolo amesema hayo wakati wa kikao kazi na viongozi kutoka Ofisi ya Mageuzi ya Kilimo (ATO), Tume ya Taifa ya Umwagiliaji (NIRC), Mfuko wa Maendeleo ya Kilimo (ADF) pamoja na Mfuko wa Pembejeo za Kilimo (AGITF) tarehe 10 Desemba 2025, jijini Dodoma.
Ameielekeza Tume ya Taifa ya Umwagiliaji (NIRC) kuhakikisha kuwa miradi yote ya umwagiliaji inayotekelezwa inakamilika kwa wakati na kwa ubora unaostahili, ili iweze kuleta matokeo chanya kwa wakulima na kwa Taifa kwa ujumla. Aidha, amesisitiza umuhimu wa NIRC kufanya ufuatiliaji wa karibu wa miradi yote ili kubaini kwa uhakika manufaa yanayotokana na uwekezaji wa Serikali.
Vilevile, Waziri ameiagiza NIRC kuanza mchakato wa kutambua mito yote nchini inayoweza kutumika katika kukuza na kuendeleza uzalishaji wa mazao kupitia umwagiliaji, hatua ambayo itachochea ukuaji wa Sekta ya Kilimo.
Kwa upande wa Mfuko wa Pembejeo za Kilimo (AGITF), Waziri Chongolo ameutaka mfuko huo kuendelea kutoa mikopo yenye tija kwa wakulima na kuimarisha ufuatiliaji wa mikopo hiyo ili kuhakikisha inarejeshwa kwa wakati, kwa kuwa urejeshaji mzuri utaiwezesha Serikali kuongeza mtaji wa mfuko huo kwa lengo la kuwafikia wakulima wengi zaidi.
Waziri Chongolo ameipongeza Ofisi ya Mageuzi ya Kilimo (ATO) kwa Mpango Kabambe wa Mageuzi ya Kilimo 2050 (Agriculture Master Plan 2050) na kuelekeza Ofisi hiyo kuongeza kasi katika kusukuma mageuzi ya kilimo nchini na kuendelea kutoa ushauri wa kitaalam utakaosaidia Sekta kusonga mbele.
Sambamba na hilo, Waziri Chongolo amepongeza juhudi za Mfuko wa Maendeleo ya Kilimo (ADF) katika kukusanya rasilimali fedha zitakazosaidia kuchochea maendeleo nchini na ameahidi kuwa Serikali itaendelea kuimarisha usimamizi na uratibu wa taasisi zote za kilimo ili kuhakikisha malengo ya Sekta ya Kilimo kufikia asilimia 10 ifikapo mwaka 2030 yanafikiwa.




No comments:
Post a Comment
Tupia Comments👇