Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Samia Suluhu Hassan, ametoa salamu za rambirambi kufuatia kifo cha mwanasiasa mkongwe nchini Kenya Raila Amolo Odinga.
Dk. Samie ameeleza katika salamu hizo za rambirambu kwamba Tanzania imepokea taarifa hiyo kwa masikitiko makubwa.
Kupitia taarifa hiyo ya leo Oktoba 15, Rais ametuma salamu za pole kwa Rais wa Kenya, Dk. William Samoei Ruto, Mama Ida Odinga, Watoto, Familia, Ndugu, Jamaa, Marafiki na Wananchi wote wa Kenya kwa niaba ya Serikali na Wananchi wa Tanzania.
“Nimepokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya kifo cha Mheshimiwa Raila Amolo Odinga, tumempoteza Kiongozi mahiri, Mwanamajumui wa Afrika, mpenda amani na mtafuta suluhu, ambaye ushawishi na upendo wake haukuwa tu ndani ya Kenya, bali Afrika Mashariki na Afrika kwa ujumla, msiba huu si wa Kenya pekee, bali ni wetu sote.
Tunaungana kuwaombea kwa Mwenyezi Mungu awajalie subra, faraja na imani katika kipindi hiki kigumu, na ailaze roho ya mpendwa wetu, Mheshimiwa Raila Amolo Odinga, mahali pema peponi. Amina,” amesema Rais.
Odinga, aliyekuwa mwanasiasa maarufu ndanina nje ya Kenya na aliyewahi kuhudumu kama Waziri Mkuu wa nchi hiyo, amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 80.
Taarifa kutoka vyanzo vya habari vya kimataifa zimeeleza alikumbwa na mshtuko wa moyo wakati akiwa nchini India akipatiwa matibabu.
Kwa mujibu wa hospitali na vyombo vya habari vya India, Odinga alikumbwa na shambulio la moyo wakati wa matembezi ya asubuhi katika eneo la kituo cha tiba ya Ayurvedic ambako alikuwa akisubiri matibabu.
Baada ya kuwahishwa haraka hospitalini ikatangazwa kuwa ameaga dunia asubuhi ya leo.
Alizaliwa tarehe 7 Januari 1945, na katika maisha yake ya siasa alihudumu katika nafasi kadhaa muhimu,ukiwemo Mbunge wa Langata kuanzia 1992 hadi 2007, baadaye akateuliwa kuwa Waziri wa Nishati (2001-2002) na baadaye Waziri wa Barabara, Kazi za Umma na Makazi (2003-2005). Kati ya mwaka 2008 hadi 2013 alihudumu kama Waziri Mkuu wa Kenya.
Aidha, Odinga alikuwa mgombea wa urais mara kadhaa, akiwa mmoja wa wanasiasa waliochangia sana katika sura ya demokrasia ya Kenya. Makubaliano ya kisiasa aliyofikiwa hivi karibuni yalikuwa na lengo la kuleta ushiriki mkubwa wa chama chake katika serikali ya umoja.
Bilashaka kifo cha Odinga kimezua majonzi makubwa nchini Kenya na katika eneo la Afrika Mashariki kwa ujumla.

No comments:
Post a Comment
Tupia Comments👇