Na Mwandishi wetu, Dodoma
Chama Cha Mapinduzi (CCM), kama taasisi kongwe ya kisiasa nchini, kimeendelea kujitahidi kuimarisha mifumo ya ndani ya uteuzi wa wagombea kwa nafasi za udiwani na ubunge. Moja ya maboresho yaliyowekwa ni mchakato wa kuchuja wagombea hadi kubaki majina matatu pekee, ambayo hupelekwa kupigiwa kura.
Lakini pamoja na nia nzuri ya kuhakikisha uongozi bora, utaratibu huu wa kupunguza majina kabla ya kuwafikia wapiga kura unaibua sintofahamu na hatari ya kisiasa, kiuongozi na kimaadili ndani ya chama.
*WAJUMBE WA CHAMA WENGI WANAPUUZWA KWA MAAMUZI YA WACHACHE*
Ukweli muhimu ambao haupaswi kupuuzwa ni huu:
Wapiga kura kwenye kura za maoni si wanachama wa kawaida tu – ni Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Wilaya/Kata. Katika maeneo mengi, idadi yao ni kubwa mno ikilinganishwa na wajumbe wa Kamati ya Siasa.
Kwa mfano:
Katika Kata, Kamati ya Siasa haina zaidi ya wajumbe 9, lakini wajumbe wanaopiga kura za maoni hufika hadi 1000 au zaidi.
Katika Wilaya, Kamati ya Siasa huwa na chini ya wajumbe 10, lakini Mkutano Mkuu una wajumbe wanaofika hadi 10,000 katika baadhi ya majimbo.
Je, ni busara wachache 9 kuwachujia elfu 10 majina ya watu watatu tu, halafu wakabidhiwe majina hayo ya kuwachagua? Hapo demokrasia haijavunjika tu – bali imeporomoka.
Hili linapelekea hisia ya ubaguzi wa kisiasa, kuzuiwa kwa haki ya kuchagua na kuchaguliwa, na kusababisha hali ya manung’uniko, chuki, na mwisho wake kuwa ni mpasuko wa ndani ya chama.
*HATARI TATU KUU KWA CCM KUTOKANA NA UTARATIBU HUU*
1. Waliokatwa Kabla ya Kura: Wanaasi na Kujitenga
Mgombea anayetumia muda, fedha, na maarifa kujipanga, anaondolewa mapema bila kupewa nafasi ya kujaribiwa na wapiga kura wake halali – wajumbe wa mkutano mkuu. Hii husababisha kuvunjika kwa imani, kuibuka kwa makundi ("fundi"), kuunga wagombea wa vyama vingine, au hata kugombea kama mgombea binafsi. Haya ni madhara yanayoumiza chama kimya kimya.
2. Waliopigiwa Kura Lakini Hawateuliwi: Hofu ya Uamuzi wa Kisiasa
Wagombea wanaopitishwa kwenye kura za maoni kwa idadi kubwa ya kura wanapokatwa, husababisha mtafaruku mkubwa. Inaleta maswali: Je, kura za maoni zina maana gani kama hazizingatiwi?
Wajumbe wa Mkutano Mkuu nao huona hawaheshimiwi, hivyo hushindwa kushiriki kikamilifu kwenye kampeni au huamua kuunga mkono wagombea wa nje kwa siri. Chama hujikuta kikishughulika na migogoro badala ya kutafuta ushindi.
3. Chama Kupoteza Ushindi Katika Ngome Zake
Pale panapotarajiwa ushindi wa moja kwa moja, huanza kuyumba kwa sababu ya makundi, manung’uniko, na usaliti wa ndani. Hii ni hatari ya kweli. Kuna uwezekano wa kupoteza viti vya udiwani au ubunge hata katika maeneo ambayo yamekuwa ngome kwa miaka mingi.
*SULUHISHO: TUREJEE NGUVU YA DEMOKRASIA YA NDANI YA CHAMA*
Chama kina suluhisho rahisi, la haki na lenye tija:
Ruhusu wagombea wote waliotimiza vigezo kushiriki kwenye kura za maoni, isipokuwa wale tu waliofeli kimaadili au kisheria.
Wajumbe wa Mkutano Mkuu ndio waachiwe mamlaka kamili ya kupima uwezo, maadili na mapenzi ya wagombea wao.
Hii itaimarisha mshikamano, haki, na kuondoa lawama zisizo za lazima kwa viongozi wa juu wa chama.
*HITIMISHO: USHINDI HAUJENGWI NA MAAMUZI YA WACHACHE, BALI NA RIDHAA YA WENGI*
CCM ni chama cha wanachama, wajumbe, na wananchi. Kinyume na hivyo, ni kuvunja misingi ya Mapinduzi. Tukipuuza sauti ya wengi, tunapanda mbegu ya maumivu ya kisiasa. Ushindi hauwezi kujengwa kwa kuwazuia maelfu kutumia sauti yao halali kwa matakwa ya wachache.

No comments:
Post a Comment
Tupia Comments👇