Jun 21, 2025

WANANCHI MANYONI WAMUUNGA MKONO RAIS SAMIA KUPITIA MKUTANO WA MWENYEKITI WA CCM

 Na Mwandishi wetu



Manyoni, Singida
– Katika mwendelezo wa mikutano ya hadhara inayoendeshwa na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Manyoni, Ndg. Jumanne Ismail Makhanda, wananchi wa Wilaya hiyo wametumia jukwaa hilo kutangaza kwa sauti moja kumuunga mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, na kumpa baraka zote kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.


Katika mkutano mkubwa uliofanyika katika eneo la Majengo, wananchi walijitokeza kwa wingi wakionesha imani yao kwa Mwenyekiti Makhanda kutokana na jitihada zake za kusikiliza na kushughulikia kero zao. Hata hivyo, mkutano huo pia uligeuka kuwa jukwaa la heshima kwa Rais Samia, ambapo wananchi walieleza wazi kuwa hawana sababu ya kutafuta kiongozi mwingine kutokana na ufanisi mkubwa alioonyesha tangu aingie madarakani.

“Tunampongeza Mwenyekiti wetu kwa kutufikia mashinani, lakini pia tunapenda kusema wazi kuwa Rais wetu, Mama Samia, ametufanyia mambo makubwa. Tunamuunga mkono kwa asilimia mia moja. 2025 ni yeye tena bila shaka,” alisema mmoja wa wananchi waliopata fursa ya kuchangia katika mkutano huo.


Kauli hiyo iliungwa mkono na umati wa wananchi waliokuwa wamebeba mabango yenye ujumbe wa kumpongeza Rais Samia kwa miradi ya maendeleo inayotekelezwa wilayani humo, ikiwemo sekta za afya, elimu, maji, na miundombinu.

Mwenyekiti Makhanda naye alitumia fursa hiyo kuwahimiza wananchi kuendelea kuiamini serikali ya CCM na kuonesha mshikamano katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi, akisisitiza kuwa maendeleo hayawezi kuletwa na mtu mmoja bali kwa ushirikiano kati ya viongozi na wananchi.

“Rais wetu ni msikivu, mtulivu na mwenye dira sahihi ya kuijenga Tanzania mpya. Kazi yetu kama viongozi wa ngazi za chini ni kuhakikisha kuwa tunamsaidia kwa vitendo. Mikutano hii ni sehemu ya mkakati wa kusikiliza wananchi na kumfikishia kila kilio chao,” alisema Makhanda.


Mkutano huo ni sehemu ya mfululizo wa ziara za Mwenyekiti huyo katika kata mbalimbali za Wilaya ya Manyoni, zenye lengo la kuimarisha mawasiliano kati ya chama, serikali na wananchi, huku pia ukitumika kama jukwaa la kuhamasisha mshikamano wa kisiasa na uzalendo.

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Pages