Itigi, Singida – Mfanyabiashara maarufu wa matrekta na vifaa vya kilimo, Ndugu Msafiri Ng’ambi maarufu kwa jina la Mdau, (pichani juu) amewapongeza wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Itigi kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kukilinda na kukisimamia chama kwa umoja, amani na mshikamano mkubwa.
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kuhudhuria kikao cha ndani kilichojumuisha wanachama wa CCM kutoka kata mbalimbali, Msafiri Ng’ambi alisema amevutiwa na nidhamu, umoja na moyo wa kujitolea wa wanachama hao katika kuhakikisha chama kinaendelea kuwa na mvuto mkubwa kwa wananchi.
“Niwapongeze sana wanachama wa CCM hapa Itigi. Mmeendelea kukisimamia chama kwa utulivu mkubwa, mmekilinda, mmekikuza na mmekipa hadhi inayostahili. Chama kipo imara na kina nguvu kubwa sana ndani ya Wilaya ya Itigi,” alisema.
Ng’ambi aliongeza kuwa uimara wa chama unaanzia kwa wanachama wa ngazi za chini, ambao wameendelea kuwa mstari wa mbele kwenye shughuli zote za maendeleo na ushawishi wa sera za CCM ndani ya jamii. Alisisitiza kuwa utulivu uliopo ndani ya CCM Itigi ni ishara njema ya ushindi wa chama hicho kwenye uchaguzi ujao wa mwaka 2025.
“Nawaomba muendelee kushikamana. Umoja huu ni silaha kubwa ya mafanikio. Na mimi nikiwa miongoni mwa wapenzi wakubwa wa maendeleo na mwananchi mwenzenu, niko tayari kushirikiana nanyi katika kila hatua ya kuleta mabadiliko chanya kwa jamii yetu,” alisisitiza.
Wanachama mbalimbali walimshukuru Msafiri Ng’ambi kwa ushirikiano wake mzuri na chama na kumuomba aendelee kuwa karibu na chama katika kuleta maendeleo ya kweli Itigi.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇