Na Bashir Nkoromo, Official CCM, Mikocheni
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameutaka uongozi wa Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) kuongeza wigo wa kuimarisha upatikanaji wa vitabu kwenye shule zote nchini kwa kushirikisha na kampuni za uchapishaji na wadau wa sekta binafsi ili kupunguza gharama za uchapishaji.
Amesema anafahamu TET imedhamiria kuchapa vitabu kwa wingi ili kufikia uwiano wa kitabu kimoja kwa mwanafunzi mmoja, jambo ambalo litaleta manufaa makubwa katika elimu na Taifa kwa ujumla. “Hivyo, kwa dhamira ya dhati kabisa, sote hatuna budi kuliunga mkono jambo hili.”
Waziri Mkuu ameyasema hayo leo Ijumaa, Machi 7, 2025, alipozungumza mwishoni mwa matembelezi ya hisani ya kuadhimisha miaka 50 ya TET aliyoyaongoza hadi kwenye Ofisi za Taasisi hiyo (TET), Mikocheni jijini Dar es Salaam, ambapo ametumia fursa hiyo kumpongeza Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa mageuzi makubwa aliyoyafanya katika sekta ya elimu.
Amesema, mbali na TET kutumia matembezi hayo ya hisani kuchangisha fedha za kuchapisha vitabu, ni vema kwa uongozi wa taasisi hiyo ukaongeza wigo wa kuimarisha upatikanaji wa vitabu kwa kushirikisha na kampuni za uchapishaji na wadau wa sekta binafsi ili kupunguza gharama za uchapishaji.
Waziri Mkuu amefafanua kuwa ushiriki wa wadau katika uchapishaji wa vitabu utasaidia kutatua changamoto ya upungufu wa vitabu shuleni, na kufikia lengo la kitabu kimoja kwa mwanafunzi mmoja. “Vitabu ni chanzo cha maarifa na maendeleo, na ni muhimu katika kuhakikisha elimu bora kwa wanafunzi.”
Akizunguzmia kauli mbiu ya maadhimisho hayo inayosema ''kitabu kimoja mwanafunzi mmoja", Waziri Mkuu amesema inawiana na malengo ya kitaifa ya kuhakikisha kuwa watoto wa Tanzania wanapata elimu bora. “Kupitia elimu bora, Taifa linaweza kufikia malengo yake ya maendeleo endelevu na kuboresha ustawi wa jamii.”
Mapema, Mkurugenzi Mkuu wa TET, Dk. Aneth Komba alisema maadhimisho ya miaka 50 TET pamoja na kampeni ya kitabu kimoja mwanafunzi mmoja yanatarajiwa kuhitimishwa Juni mwaka huu na yanalenga kukusanya sh. bilioni 297 kwa ajili ya kufikia azma ya kitabu kimoja, mwanafunzi mmoja na ununuzi wa kompyuta za kuhifadhi vitabu.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akiongoza matembelezi ya hisani ya kuadhimisha miaka 50 ya TET yaliyofanyika leo kuanzia Chuo Kikuu cha Dar es Salaam hadi kwenye Ofisi za Taasisi hiyo (TET), Mikocheni jijini Dar es Salaam.
Waziri Mkuu akiwa na viongozi mbalimbali wakiwemo wa TET kwenye matembezi hayo.Baadhi ya wanafunzi wakishiriki matembezi hayo.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇