LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Jan 5, 2025

MSIGWA: SERIKALI IMEPIGA HATUA KUBWA KATIKA UZALISHAJI UMEME, WAKUU NCHI ZA AFRIKA KUKUTANA TANZANIA MWEZI HUU KUHUSU NISHATI HIYO

Na Bashir Nkoromo, CCM's Blog, UDSM

Serikali imesema imefanikiwa kufikisha umeme katika vijiji 12,278, sawa na asilimia 99.7 ya vijiji vyote nchini katika kipindi cha mwaka 2020 hadi mwaka jana 2024.


Pia katika kipindi hichi vitongoji 32,827 vimefikiwa na umeme kati ya vitongoji 64,359, sawa na asilimia 51. 


Imesema, hatua hiyo imeongeza fursa kwa wananchi kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi na kuboresha sekta muhimu kama elimu, afya, biashara, na usafiri. 


Hayo yamesemwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, leo Januari 5, 2025, katika ukumbi wa Maktaba, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, akifungua semina ya wahariri na Waandishi wa habari kujirisha Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika kuhusu Nishati utakaonyika Januari 27-28, 2025, katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam.


Msigwa amesema kwa mujibu wa takwimu, zaidi ya taasisi 12,905 za afya na elimu zimeunganishwa na umeme, hatua ambayo imeimarisha utoaji wa huduma kwa wananchi.


Amesema zaidi ya hayo Serikali imewekeza katika vyanzo mbadala vya nishati kama umeme jua, jotoardhi, na upepo, ambapo uzalishaji unatarajiwa kuongezeka kwa megawati 1,100. 


"Hii inalenga kuvutia uwekezaji zaidi katika sekta ya viwanda, ambapo idadi ya viwanda vya uzalishaji wa vifaa vya nishati kama nguzo na nyaya imeongezeka kutoka 23 mwaka 2020 hadi kufikia viwanda 78 mwaka 2024. 


Uzalishaji wa ndani wa vifaa hivi siyo tu unatoa ajira kwa Watanzania, bali pia unapunguza gharama za usambazaji wa nishati vijijini na mijini", alisema Msigwa.


Kuhusu Mkutano huo wa Wakuu wa Nchi za Afrika kuhusu Nishati Msigwa amesema ni matokeo ya juhudi kubwa za kidiplomasia za Rais Dk. Samia Suluhu Hassan. 


"Rais Dk. Samia ameonyesha uongozi wa mfano barani Afrika kwa kusimamia ajenda ya nishati safi ya kupikia, ambapo kupitia Mkakati wa Kitaifa wa Matumizi ya Nishati Safi wa mwaka 2024-2034, Tanzania imelenga kufikia asilimia 80 ya kaya kutumia nishati safi ifikapo mwaka 2034. 


Hatua hii inalenga kuboresha afya za wananchi na kulinda mazingira dhidi ya uharibifu wa misitu unaotokana na matumizi ya kuni na mkaa", alisema Msigwa.


Msigwa alisisitiza, mkutano huo utaweka msingi wa kupatikana kwa umeme kwa Waafrika milioni 300, ambapo nchi 14 za Afrika zitatia saini makubaliano hayo mbele ya marais zaidi ya 10 wa Afrika.


Aidha, Msigwa amewahimiza waandishi wa habari kushirikiana kwa dhati na Serikali kufanikisha mkutano huo, huku akibainisha kwamba Tanzania inayo nafasi ya kipekee kuimarisha taswira yake kimataifa kupitia tukio hili.


“Ndugu wahariri na waandishi wa habari, ninyi ni daraja muhimu kati ya Serikali na wananchi. Hakikisheni taarifa sahihi kuhusu juhudi za Serikali zinawafikia wananchi. 


Kupitia mkutano huu, tunawataka kuelewa kwa undani ajenda zake na kuelimisha umma kuhusu umuhimu wake,” alisema Msigwa. 


Msigwa alimalizia kwa kutoa mwito kwa Waandishi wa habari kuweka ajenda moja ya kuijenga taswira chanya ya Tanzania kimataifa, akisisitiza kwamba “Tanzania Kwanza!”

Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, akifungua semina ya wahariri na Waandishi wa habari katika ukumbi wa Maktaba, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, leo Januari 5, 2025.

Semina hiyo ni ya kujirisha Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika kuhusu Nishati utakaonyika Januari 27-28, 2025, katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam. Picha: Bashir Nkoromo.

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages