Na Mwandishi Maalum, Zanzibar.
Rais Mstaafu Dk. Jakaya Kikwete, amepongeza kasi ya maendeleo yanayofanyika Zanzibar chini ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Mwinyi na kusisitiza kuwa mafanikio hayo, ambayo yanapaswa kupongezwa na kuenziwa.
Dk. Kikwete ametoa sifa hizo, wakati akihutubia jana, wakati wa hafla ya uzinduzi wa Kituo kipya cha Afya Kizimkazi, katika Wilaya ya Kusini Unguja, ambao ni moja ya matukio katika kusherehekea miaka 61 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar, ambayo kilele chake kitakuwa Januari 12, 2025.
Dk. Kikwete alibainisha kuwa kituo hicho cha kisasa kina uwezo mkubwa wa uchunguzi wa maradhi na tiba, hivyo ni mkombozi wa huduma za afya kwa wakazi wa Kizimkazi na maeneo jirani.
Alihimiza umuhimu wa kutunza majengo na vifaa vya kituo hicho ili kuhakikisha huduma hizi za thamani zinadumu kwa muda mrefu."Tukitunze kituo kidumu; ni chetu, ni mali yetu, ni kwa ajili yetu," alisisitiza Dkt. Kikwete.
Rais Mstaafu aliambatana na mkewe, Mama Salma, ambaye ni Mbunge wa Mchinga, na viongozi wengine wa kitaifa. Hafla hiyo ilihudhuriwa na mamia ya wananchi wenye furaha kubwa.
Kwa mujibu wa taarifa rasmi, Kituo cha Afya Kizimkazi kinatarajiwa kuhudumia zaidi ya wananchi 13,000 kutoka shehia za Kibuteni, Kizimkazi Mkunguni, na Kizimkazi Dimbani, pamoja na maeneo jirani kama Muyuni.
Katika mwaka 2024 pekee, jumla ya watu 12,389 walihudumiwa kituoni hapo, wakiwemo wanaume 5,068 na wanawake 7,325.
Kituo hiki kimejengwa kwa ushirikiano wa wadau mbalimbali, wakiwemo Samia Foundation, Foundation for Humanitarian Initiatives ya Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), Benki ya NBC, pamoja na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Dkt. Kikwete aliutaja ushirikiano huu kama mfano wa kuigwa katika juhudi za maendeleo, hivyo aliitaka Wizara ya Afya kuhakikisha upatikanaji wa wafanyakazi wa kutosha na matengenezo ya mara kwa mara ili huduma ziwe endelevu na zenye ubora.
Hotuba yake ilihitimishwa kwa kaulimbiu ya "Amani, Umoja na Mshikamano kwa Maendeleo Yetu – Mapinduzi Daima," kabla ya kutangaza rasmi kufunguliwa kwa Kituo cha Afya Kizimkazi.
Wananchi walionekana kufurahishwa sana na tukio hili, wakisema kuwa kituo hicho ni zawadi kubwa kwa maisha yao."Huu ni mwanzo wa zama mpya kwa huduma za afya hapa Kizimkazi," alisema mmoja wa wakazi kwa furaha.
Kwa uzinduzi wa miradi kama huo, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaendelea kuthibitisha dhamira yake ya kuleta maendeleo ya kweli kwa wananchi wake kwa vitendo.
Rais Mstaafu Dk. Jakaya Kikwete, akikata utepe kuzindua Kituo kipya cha Afya Kizimkazi, katika Wilaya ya Kusini Unguja, January 4, 2025. Kushoto kwake ni Waziri wa Afya Zanzibar Nassor Ahmed Mazrui, na kulia kwake ni Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja Ayoub Mohammed Mahamoud na wa pili kushoto ni Mama Salma Kikwete.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇