Na.
Faraja Mbise, DODOMA
Wananchi
wameshauriwa kushiriki katika kila hatua ya maendeleo ya nchi ili kuimarisha
demokrasia kwa sababu wanaposhiriki katika maendeleo wanapata fursa ya kuibua
changamoto na fursa zilizopo sambamba na kueleza mawazo yao na kutoa
mapendekezo.
Hayo, yalisemwa na
Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Alhaj Jabir Shekimweri alipokuwa akizungumza na wadau
mbalimbali wa maendeleo katika Mdahalo wa Miaka 63 ya Uhuru wa Tanzania Bara,
uliofanyika katika ukumbi wa Mikutano wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
“Ndugu
zangu, sisi kwenye serikali, kwa maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, hata kwenye hatua ya kuweka miongozo,
tunawajibika sana kuhakikisha wananchi wanashirikishwa katika hatua zote za
kujiletea maendeleo.
Viongozi mtakubaliana na mimi hata wakati wa kupigania
uhuru viongozi hawa mashuhuri tunaowasema hawakuwa pekeyao. Hata leo kuleta
maendeleo ya Tanzania hatuwezi kuwa na viongozi pasipo kuwashirikisha wananchi.
Wananchi wanashirikishwa sana katika maeneo yao, kwanza kkuibua
vipaumbele vya maendeleo” alisema Alhaj Shekimweri.
Alitoa
pongezi kwa Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania, kwa kupiga hatua kubwa ya
maendeleo tangu Tanzania bara ilipopata uhuru wake mpaka hivi sasa. “Natoa
pongezi nyingi kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu
Hassan, kwa kuadhimisha miaka 63 ya Uhuru wetu na kuendeleza mambo mengi sana
ya maendeleo yenye tija kwa nchi yetu. Pia kujenga diplomasia na mahusiano ya
kimataifa na mataifa mengine katika namna ambayo pia inaendelea kunufaisha nchi
yetu.
Tunamtia nguvu katika kila changamoto anayopitia kama kiongozi, najua
mahitaji ya watanzania ni makubwa, najua kuna vita kubwa ya kiuchumi na
kimaadili. Lakini kwa hakika watanzania tunatambua kwamba, nchi yetu miaka 63
baada ya Uhuru, imepiga hatua kubwa sana ya kimaendeleo na kwamba ipo katika
uelekeo mkubwa zaidi wa kufanya maendeleo makubwa zaidi” alipongeza Alhaj
Shekimweri.
Kuhusu mila, tamaduni
na jadi zetu, Mkuu wa Wilaya ya Dodoma aliwaasa wananchi kuzienzi na kutunza
mila na tamaduni zetu. “Maana ya kuwa huru, ni kuwa na taifa lenye utambulisho
wake wa mila, desturi na tamaduni zake. Na tunamuenzi Mwalimu Nyerere, hapo
aliwahi kusema, ‘asiyejali mila zake ni mtumwa’. Sisi watanzania tuna tamaduni
nzuri sana, mila nzuri sana, jadi nzuri sana na tunazienzi, zitambua na
kuzithamini” alisema Alhaj Shekimweri.Kwa
upande wake Mstahiki Meya wa Jiji la Dodoma, Prof. Davis Mwamfupe aliwataka
wananchi kulinda Uhuru wa Tanzania kwa kufanya kazi ili waweze kujitegemea
kiuchumi na kuwasisitiza kuwa, hiyo ndio maana halisi ya kuwa na uhuru. “Hakuna
uhuru wa taifa kama hakuna uhuru binafsi, hatuwezi kuulinda uhuru wa taifa kama
hatuwezi kulinda uhuru wetu binafsi, tujikomboe kifikra, kiuchumi ndipo
tunaweza kuikomboa nchi kama taifa.
Kwahiyo, tujiimarishe sana kuhakikisha
kwamba tunalinda uhuru wetu. Mwalimu Nyerere wakati ule ilikuwa Uhuru na Kazi,
baadae tulipogndua kuwa kazi ni muhimu tukasema uhuru ni kazi, hapa falsafa
maana yake ni nini: hatuwezi kusema tumejikomboa tuko huru kama hatufanyi kazi,
lakini hapa inatukumbusha wazi kwamba, uhuru wetu utakuwa na maana pale
tutakapokuwa na uwezo wa kujitegemea na utajitegemeaje ni kwa kufanya kazi kwa
bidii” alisisitiza Prof. Mwamfupe.
Nae Kaimu Mkurugenzi
wa Jiji la Dodoma, Joseph Fungo alizungumzia maendeleo ya Teknolojia ya Habari
na Mawasiliano (TEHAMA) jinsi yalivyorahisisha suala la mawasiliano katika
utendaji kazi ukilinganisha na kipindi cha nyuma wakati wa kupambania Uhuru wa
Tanzania bara. “
Miongoni
mwa vitu ambavyo nchi yetu imepiga maendeleo makubwa sana ni kwenye teknolojia
kwa maana ya matumizi ya TEHAMA. Zamani ilikuwa unapotaka kusafiri lazima ufike
stendi ukakate tiketi lakini sasahivi, huna haja ya kwenda stendi, unaweza
ukafanya hivyo ukiwa nyumbani kwako. Zamani ilikuwa kama unataka kutoa au
kuweka hela benki lazima uende kwenye benki na ukapange foleni, lakini siku hizi
unaweza kufanya miamala kwenye simu na kwa mawakala ni kwasababu ya matumizi
makubwa ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano.
Na kwenye eneo hilo la mikopo
ya asilimia 10 unajisajili kwenye mfumo huna haja ya kuja ofisini. Kwahiyo,
matumizi ya teknolojia tunaona jinsi ambavyo yamekua na sisi kama Halmashauri
ya Jiji la Dodoma tunaendelea kutumia hiyo mifumo” alisema Fungo kwa ujasiri
mkubwa.
Akizungumzia masuala
ya mmomonyoko wa maadili, Mwanasheria wa Baraza la Machifu Mkoa wa Dodoma,
Samwel Chimanyi aliwataka wananchi hasa vijana kuachana na makundi ambayo yanaathiri
mifumo ya maadili ya kitanzania.
“Hili eneo mkalitafsiri vizuri nyie mlioko
shuleni, tuachane na kuiga makundi ambayo yamejielekeza kwenye tabia zinazoathiri
mifumo ya maadili yetu. Kwahiyo, watemi wanaendelea kutoa rai na kulaani vikali
masua unyanyasaji
wa kijinsia na vitu vinavyoendelea ambayo sio vizuri kwa maadili ya kitanzania”
alitoa rai Chimanyi.
Kuimarika
kwa ushirikishwaji wa wananchi kutokana na mfumo wa kidemokrasia wa vyama
vingi, mchangiaji wa mada kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Nasma Ally
alizungumzia kuhusu ushirikishwaji wa wanawake katika kuwania nafasi mbalimbali
za uongozi. “Kupitia mfumo wa vyama vingi, ushirikishwaji wa wananchi pamoja na
mkusanyo wa mawazo katika taifa letu uliimarika.
Sambamba na hilo Serikali ya
Tanzania iliweza kuanzisha Tume huru ya Taifa ya Uchaguzi ambayo inasimamia uchaguzi
wa huru na haki. Demokrasia ni haki na usawa, kwakuzingatia hilo pia, Serikali
ya Tanzania iliweza kuongeza ushiriki wa wanawake katika masuala ya uongozi.
Hii ilifanyika pale Tanzania ilipoongeza siti maalumu kwa wanawake. Takwimu
zinasema kutoka mwaka 1990 asilimia 4.6 zilikuwa ni kwa ajili ya wanawake
Bungeni za viti maalum, kwa mwaka 2020 asilimia 36.6 ni siti maalum za wanawake.
Tunapoona wanawake wanashiriki katika masuala ya nchi, hii inonesha kwamba
jamii pamoja na serikali mwanamke ni kiongozi wa familia, jamii na ana mchango
mkubwa sana katika kuilea jamii na kupelekea maendeleo ya taifa” alisema Ally.
Hata hivyo,
Mwenyekiti wa Wanawake na Samia Dodoma, Fatuma Madidi alichangia mada kwa kugusia
maendeleo ya miundombinu
katika sekta ya usafirishaji na elimu kwa kuipongeza serikali kwa kujikita
katika maendeleo tangu ulipopatikana uhuru wa Tanzania bara. “Ile dhana ya Baba
wa Taifa ya kufuta ujinga imekamilika na kwamba sasa kila mmoja ana haki ya
kwenda shule na kusoma. Katika swala la miundombinu utaona kwamba, sasahivi
barabara nyingi zinaingilika na na zinapitika na hakuna hata ule muingiliano
baina ya wilaya na wilaya, na mkoa kwa mkoa. Sasahivi lile tatizo la usafiri
limekuwa ni historia” alichangia Madidi.Tanzania
bara huadhimisha uhuru wake ifikapo Desemba 09 ya kila mwaka na kaulimbiu ya
maadhimisho hayo ya miaka 63 ya Uhuru wa Tanzania Bara ni “Uongozi
Madhubuti na Ushirikishwaji wa Wananchi ni Msingi wa Maendeleo yetu”.
Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Alhaj Jabir Shekimweri alipokuwa akizungumza na wadau mbalimbali wa maendeleo katika Mdahalo wa Miaka 63 ya Uhuru wa Tanzania Bara, uliofanyika katika ukumbi wa Mikutano wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
Baadhi ya wadau walishiriki kwenye mdahalo hilo.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇