LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Dec 17, 2024

HOTUBA ILIYOTOLEWA NA WAZIRI MHAGAMA AKIZINDUA MIFUMO YA KIDIJITALI NA VIFURUSHI VYA BIMA YA AFYA KWA WOTE

Nawasalimia kwa Jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.........

Awali ya yote nianze kwa kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha kukutana hapa tukiwa na afya njema katika tukio hili muhimu.


Leo ni siku ya furaha kubwa sana kwangu binafsi, Wizara, Sekta ya Afya na Umma wa Watanzania kwa ujumla, kwa sababu ya tukio hili muhimu la uzinduzi wa Mifumo ya NHIF ambayo inakwenda kuleta mapinduzi makubwa katika utoaji wa huduma kwa wanachama wake na wadau wake muhimu kama

Watoa Huduma.


 Hili ni tukio kubwa na la muhimu sana kwetu.

● Bima ya Afya kwa wote

Ndugu Washiriki,

1

Mtakumbuka Sheria ya Bima ya Afya kwa wote tayari ilishatangazwa kuanza kutumika kupitia tangazo la Serikali Na. 700A la mwaka 2024 na kanuni zake zimetangazwa kutumika kupitia tangazo la Serikali 809 la mwaka 2024 hivyo.


Mifumo itawezesha Watanzania kupata taarifa muhimu kwa wakati na kuweza kujihudumia kwa kujiunga kiurahisi.


Wageni Waalikwa

Suala la Bima ya Afya kwa Wote ni kipaumbele kwa Serikali yetu ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mama yetu Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, sote tutakumbuka tangu anaingia madarakani lilikuwa ni agizo lake kuhakikisha hili linatekelezeka hivyo kwa upande wake amemaliza na sisi ndio tuna deni la kuhakikisha mazingira yote yako sawa kwa wananchi kujiunga na kupata huduma bora.


Serikali imehakikisha imeweka miundombinu imara katika maeneo yote ya wananchi kwa kujenga Zahanati, Vituo vya Afya, Hospitali ngazi ya Wilaya, Mkoa, Kanda hadi Taifa. 


Hivi sasa tuna takriban vituo 10,004 nchi nzima. Kati ya

vituo hivyo vituo 7,181ni vya serikali, vituo 1,975 ni vituo binafsi na 848 ni vituo vinavyosimamiw na Taasisi za kidini. Serikali imefanya uwekezaji mkubwa wa Vifaa tiba na dawa kuwawezesha wananch kunufaika na huduma hizo ambazo

Serikali yao imewekeza. 


Nafurahi kuwajulisha kwamba Serikali ya awamu ya Sita

imekuja na suluhisho muhimu yaani BIMA YA AFYA KWA WOTE. Hii ni kumwezesha mwananchi kupata huduma za afya bila kutetereka kutokana na gharama za matibabu.


Tutambue kuwa tuna kazi kubwa kulingana na takwimu zilizopo za wananchi walioko ndani ya mfumo wa bima ni asilimia 15 tu, ambapo NHIF inahudumia asilimia nane (8) tu ya Watanzania hivyo unaweza kuona kuwa zaidi ya asilimia

2

85 ya watanzania wako nje ya Mfumo wa bima. Nitoe rai hapa kuwa kila mmoja aliyeko hapa aone anawajibika moja kwa moja kuhakikisha anahamasisha na kuelimisha wananchi juu ya umuhimu wa bima ya afya.


Kwa Watoa huduma sasa tambueni kuwa suala la kutoa huduma bora kwa wananchi kupitia bima ya afya ni la lazima na sio hiari. Bima ya afya kwa wote ni utekelezaji wa Sheria Na 13 ya mwaka 2023. 


Hivyo hakikisheni mnaweka mazingira rafiki na yanayowavutia wananchi kuona umuhimu wa kuwa na bima ya afya.


● Upatikanaji wa Huduma

Tunatambua kuwa upatikanaji wa huduma bora za matibabu hasa kwa mwananchi wa kawaida pamoja na upatikanaji wa huduma ya dawa kwa sasa umeongezeka sana kutokana na jitihada kubwa zinazofanywa na Serikali yetu hususan kuongeza fedha katika eneo hilo. 


Pamoja na mafanikio haya, Wizara imeendelea kusimamia na kudhibiti mianya yote ya upotevu wa dawa ili kuhakikisha wananchi na wanachama wa Mfuko huu wanapata huduma bora wanapokuwa katika vituo vya kutolea huduma.


Wakati Wizara ikichukua hatua hizi, naiagiza NHIF kuangalia namna Mfuko unavyoweza kuendeleza ushiriki wake katika suala zima la uboreshaji wa huduma katika vituo vya kutolea huduma kutokana na fursa zilizopo.


 Natambua Mfuko umekuwa ukitoa mikopo nafuu kwa hospitali za Serikali, Taasisi za Dini na Hospitali binafsi. Mikopo kwa ajili ya vifaa tiba ( 74.2%), Ukarabati vituo vya afya 21.4%) na dawa (4.3%).

3

Nina uhakika kuwa ushiriki wa NHIF katika kuwekeza kwenye uboreshaji wa miundombinu ya vituo vya matibabu na upatikanaji wa vifaa tiba na dawa utaendelea kuimarisha sana upatikanaji wa huduma na utapunguza malalamiko kwa wanachama wake na wananchi kwa ujumla.


 Wizara yangu iko tayari kuwashika mkono pale mtakapoona mnakwama ili kuhakikisha Mfuko huu unatimiza malengo yake na wakati huo huo unabaki kuwa endelevu.



Aidha pongezi hizi pia nazitoa kwa Mkurugenzi Mkuu Dkt. Irene Isaka ambaye amekabidhiwa taasisi hii nyeti kuiongoza hasa katika wakati huu ambao kama nchi yetu inatekeleza magauzi makubwa katika sekta ya Bima ya Afya kwa wote,

Hongera sana.


● Uzinduzi wa Mifumo

Tukio la leo ambalo limetukutanisha hapa ni uzinduzi wa Mifumo ambayo inaanza kutumika katika kuwahudumia wananchi moja kwa moja bila kulazimika kufika katika Ofisi za NHIF, jambo hili ni kubwa na niwapongeze sana. 


Kama mnavyokumbuka hili lilikuwa ni agizo la Mhe. Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye aliagiza Mifumo yote ya Serikali sasa ianze kusomana na agizo hili lilikuwa hadi Desemba mwaka huu, hivyo kwa Taasisi yetu NHIF mmefanya vizuri kulifanyia kazi na kuhakikisha mifumo yenu sasa inasomana na Taasisi zingine lakini imezingatia mahitaji ya kuwahudumia wananchi.


Ndugu Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, Kama alivyodokeza Mkurugenzi Mkuu kwenye taarifa yake kuwa, Mifumo ninayozindua leo ni pamoja na Mfumo wa Usajili wa Wanachama ambao unamwezesha mwananchi kujihudumia popote alipo kwa njia ya mtandao.

4

Mwanachama ataweza kuona taarifa zake na kuhuisha pale anapohitaji. Mfumo mwingine ni wa uwasilishaji madai na uchakataji madai hayo. Nimejulishwa kwamba kwa upande wa uwasilishaji wa madai, tayari asilimia 80 ya vituo vimeshaunganishwa. Hivyo kurahisha uchakataji wa madai, kudhibiti udanganyifu na kulipa mapema watoa Huduma.


Nipongeze sana hatua hii kutokana na ukweli kuwa, hapo awali NHIF ilikuwa ni Taasisi ambayo imegubikwa na changamoto nyingi zikiwemo za ucheleweshaji huduma kwa wanachama, kuchelewesha malipo kwa watoa huduma pamoja na udanganyifu. Mifumo hii inakwenda kusaidia kuondoa changamoto hizi na hatimaye kutoa huduma zenye ubora unaotakiwa.


Waheshimiwa wageni Waalikwa

Sasa naomba niseme kidogo kuhusu hili la Mpango wa Toto Afya Kadi. Mpango huu ulisaidia sana familia za wananchi hasa zile zilizokuwa na changamoto za kiafya. Mpango huu pamoja na uzuri wake ulileta hasara kwa kuwa kwa kila shilingi 100 mtoto alitumia takriban shilingi 600. 


Natambua NHIF imekuja na mpango wa kusajili makundi ya watoto na hivyo kupunguza athari. Nimejulishwa pia kwamba leo nitazindua mpango wa usajili wa mtoto mmoja mmoja iwapo itatokea kwamba mtoto hayupo shule. 


kwa dhati kabisa niwapongeze kwa kuwa wasikivu na kufanyia kazi maoni kutoka kwa wananchi na wadau wengine ambapo mmefanyia kazi na leo tunazindua utaratibu wa kumwezesha mtoto kujiunga kwa makundi au mmoja mmoja.


Sasa nitumie fursa hii kuwaomba wananchi kuwasajili watoto wao ili waweze kuhudumiwa kwa utaratibu wa bima ya afya lakini pia kuhakikisha mnakuwa walinzi wa hizi huduma ili Mfuko usiibiwe kupitia huduma za watoto

watakaojiunga kwani kwa kufanya hivyo mtakuwa sehemu ya kulinda uhai wa Mfuko.


Wageni waalikwa mabibi na mabwana

Moja ya wadau wakubwa wa Mfuko huu ni Watoa huduma ambao wanahudumia wanachama wenu na mnawalipa kwa huduma hizo.


 Kama alivyosema

Mkurugenzi Mkuu kuwa kwa sasa Mfuko umeweza kushughulika na changamoto ya makato ya madai ya watoa huduma lakini pia Mfuko kwa sasa unalipa Madai kwa wakati na ujio wa Mifumo hii sasa NHIF inakwenda kuondoa kabisa malalamiko ya Watoa huduma.


Kutokana na hili, Wizara yangu inatarajia kuona Watoa huduma wakiwahudumia wanachama kwa ubora na kuwapa taarifa sahihi wanazopaswa kupewa lakini pia hakikisheni sasa mnawasilisha Madai sahihi ili muweze kulipwa madai ambayo ni halali. 


Vitendo vya udanganyifu havivumiliki hata kidgo tutachukua hatua kali dhidi ya vituo vitakavyojihusisha na udanganyifu au mwanachama yeyote.

Serikali inayo matarajio makubwa sana kwa Mfuko huu, niwaombe mjielekeze katika maeneo yafuatayo:-


a. Pamoja na maboresho haya ya Mifumo yaliyofanyika na tunayokwenda kuzindua muda mfupi ujao, endeleeni kubuni namna bora za kufanya tathnimi na kuongeza wigo wa wanachama na huduma ili kuondoa changamoto zinazolalamikiwa bila kuathiri uhai na uendelevu wa Mfuko.


b. Najua Mfuko uko katika hatua za kuja na vifurushi mbalimbali ili kuwezesha wananchi kujiunga kupitia sheria ya bima ya afya kwa wote,hakikisheni mnawashirikisha wadau muhimu ili kuweza kupata maoni

6

kutoka makundi yote ili kuwezesha kupata vifurushi vinatakavyosaidia wanachi moja kwa moja.


c. Natambua Mfuko una Kituo cha Huduma kwa Wateja kwa njia ya simu bila malipo kinochotoa huduma masaa 24 siku 7 za wiki. Hata hivyo, hakikisheni mnaweka watumishi wenye ujuzi wa aina mbalimbaliwakiwemo Madaktari wauguzi na wafamasia ili kuweza kutatua.

c hangamoto zinazowasilishwa kwa wakati.


d. Aidha, hakikisheni mnatoa taarifa kwa umma kwa wakati kwa maeneo yanayohitaji ufafanuzi ili kuepusha wananchi kupata taarifa zisizo sahihi kupitia vyanzo vingine.


e. Eneo jingine hakikisheni Menejimenti inatekeleza maelekezo mbalimbali yanayotolewa na mamlaka za usimamizi ikiwemo Wizara yangu, Kamati za Kudumu za Bunge, Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali,

Benki Kuu ya Tanzania na Mamlaka ya Usimamizi wa Bima (TIRA).


f. Natambua Mfuko unafanya jitihada mbalimbali za kudhibiti vitendo vya udanganyifu, nitumie nafasi hii kupongeza NHIF na kukemea tabia ya baadhi ya watoa huduma kutumia Mfuko kujipatia mapato yasiyo halali na kwa udanganyifu lakini pia Mfuko utuletee taarifa ya wanaobainika na vitendo hivi.


Nilianza kwa kuwashukuru naomba nimalizie kwa kuwashukuru. Naishukuru pia Menejimenti ya Mfuko kwa maandalizi mazuri ya shughuli hii. 


Baada ya kusema hayo niko tayari sasa kwa ajili ya kuizindua rasmi Mifumo yetu ya Usajili wa Wanachama na Uchakataji wa madai pamoja na kuzindua TOTO Afya!

Asanteni sana kwa kunisikiliza.



Waziri wa Afya, Jenista Mhagama na Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), Dkt. Irene Isaka wakiwakabidhi kadi watoto wa shule mfano wa kadi ya Toto Afya wakati wa uzinduzi wa Toto Afya ambapo pia ilizinduliwa mifumo ya kidigitali na vifurushi vya Bima ya Afya kwa Wote. Kulia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Ukimwi, Eribariki Kingu.

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages