Wiki iliyopita mji wa Kigoma, ulikuwa na hekaheka tunayoweza kusema ilikuwa ya kipekee, Wakati Waumini wa Kanisa Halisi kutoka ndani na nje ya Tanzania walipomiminika kushiriki Ibada yao ya Hija ya Chanzo Halisi ambayo waumini hao wamekuwa wakiifanya kila mwaka katika mji huo.
Ibada Kuu ya Hija hiyo ilifanyika katika Uwanja wa Michezo wa Mwanga Community Centre, Jumapili ya Disemba Mosi, 2024 au 26 Thebeti 1 Majira Halisi kwa Kalenda ya Kanisa hilo na iliongozwa na Kiongozi Mkuu, BABA HALISI, akiachilia somo la 'Hija ya Uzinduzi wa Maisha tuliyokusudiwa tangu Chanzo'.
Hija hiyo ilikuwa ya mara ya nane (8) kufanyika Kigoma, tangu Kanisa hilo lilipoanzishwa nchini Tanzania, na ilihudhuriwa na maelfu ya Waumini (Uzao) na Watekeleza Sauti (viongozi) kutoka vituo vya mikoa ya Tanzania Bara na Zanzibar, na wa kutoka mataifa manane ya nchi za nje yakiwemo Marekani, Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Zambia na Congo-DRC.
Akizungumza mwanzoni mwa Ibada hiyo, BABA HALISI aliwashukuru Viongozi wote wa serikali mkoa wa Kigoma na Wananchi wote wa mkoa huo kwa kuwapokea vizuri yeye na uzao wote, akavishukuru vyombo vya ulinzi na usalama, wamiliki wa nyumba za wageni, hoteli, wamiliki wa vyombo vya usafiri ikiwemo bodaboda na mabasi.
Upande wa vyombo vya usafiri BABA HALISI, aliwashukuru kipekee Shirika ya Reli Tanzania (TRC) na Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) kwa kutoa huduma bora kwa Uzao na Watekeleza Sauti waliosafiri kwa vyombo hivyo kutoka Jijini Dar es Salaam, hadi Kigoma.
BABA HALISI akasema TRC waliwasafirisha vema Uzao na Watekeleza Sauti kwa kuwa treni iliyowasafirisha kutoka Jijini Dar es Salaam, ilifika Kigoma mapema kuliko ilivyotarajiwa, ilifika mchana, huku kwa upande wa ATCL akiwapongeza na kuwaombea baraka kwa Muumba, akisema, waliweza kuweka flight ya kwenda Kigoma wakati haikuwepo kwenye ratiba yao siku hiyo.
Pamoja na Ibada ya Hija hiyo kufana vilivyo ikizingatiwa kuwa ilifanyika kwa amani na utulivu ikihudhuriwa na viongozi wa serikali, siku moja kabla ya Ibada hiyo ulifanyika uzinduzi wa Mafunzo ya Ujasiriamali (Ibada ni Uzalishaji) yaliyoratibiwa na kutolewa bure na Kanisa hilo, kwa wananchi walijitokeza hasa kina mama na vijana wa mji wa Kigoma-Ujiji.
Hakika ufunguzi wa mafunzo haya ulitia fora sana hasa kwa kuhudhuriwa na Mkuu wa Wilaya ya Kigoma Dk. Rashid Chuachua na Mbunge wa Kigoma Mjini Kirumbe Ng'enda ambao hotuba zao zilifanya amsha-amsha kwa namna ambavyo zilionyesha kwamba kwa kuratibu mafunzo hayo Kanisa Halisi chini ya BABA HALISI limefanya jambo muhimu sana.
Kilichozidisha kutia moyo na kuamsha furaha na kicheko kwa BABA HALISI, MAMA HALISI, Watekeleza Sauti, Uzao na Washiriki wa mafunzo hayo, ni pale DC Dk. Chuachua alippzipa heko falsafa za Kanisa Halisi za Amani, Upendo usiobagua na Ibada ni Uzalishaji (kwa haki), na pia kutamani kujua kwa nini tangu BABA HALISI hadi Uzao wote ubini wao ni Halisi na nini siri ya Kanisa Halisi kuvaa vazi jeupe.
"Heri Kiongozi wa Kanisa Halisi la Mungu Baba, Baba Halisi. Baba Halisi oyeee! " akasema DC Dk. Chuachua akisalimia mwanzoni mwa hotuba yake, kisha akasema "Kuna vitu nitaomba mnifundishe, siyo lazima sasa hivi hata wakati wowote mkiwa na nafasi. Kwa nini kila Kiongozi ubini wake ni Halisi, na kila kitu kinaitwa Halisi?, na pia siri ya kuvaa nguo nyeupe, kimsingi vitu hivi vinanivutia sana napenda kuvijua".
Kisha DC Dk. Chuachua akasema, "Heri, kadiri tunavyoishi duniani hatuwezi kumalizi kila kitu, ndiyo maana tutaendelea kujifunza, maana leo ni mara ya kwanza nasimama mbele ya waumini wa Kanisa hili na kujifunza salamu mpya (Heri), ambayo sijawahi kuisikia mahala popote, ndiyo kwanza najifunza".
Akiendelea na hotuba yake, DC akasema "Baba Halisi, mimi nilete salamu zangu za pongezi kwako na Kanisa lako ambalo lina falsafa ya kipekee sana. Siku moja nilitembelewa na Baba na Mama Haisi, na mimi pia ni Baba na Mama Halisi hapa Kigoma (akimaanisha Mtekeleza Sauti na Kanisa wake wa Kigoma), nikawaambia mimi nafurahishwa sana na falsafa yenu, naiona ni falsafa ya kipekee sana, nikisema falsafa nina maana ya mawazo, fikra na mwelekeo wenu, baada ya kuona mna mambo makubwa matatu ya maana sana kwa ustawi nchi yetu na kwa usatwi wa Kigoma yetu".
"Cha kwanza ni mahubiri yenu yanayojielekeza kwenye amanani, hakika mnafanya kazi kubwa ambayo pia inafanywa na serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na mama yetu Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, ya kulinda na kuhubiri amani, hongereni sana.
Pia mna jambo moja kubwa wenyewe mnaliita ibada ni uzalishaji. Nimefurahishwa sana pia na mtazamo wenu katika jambo hilo. Kwamba Watanzania wanapofanya shughuli zao za Ibada wafahamu kwamba uzalishaji ni ibada, sasa ninyi mnalitekeleza hili kwa vitendo, mambo haya mawili ya kuhubiri amani na kueleza ibada ni uzalishaji mnayabeba samnjari na jambo moja kubwa, upendo usiobagua. Sasa hapa nafarijika zaidi. upendo usioagua. Kuna mwandishi mmoja Shaaban Robert alisema endapo dini zote zingetekeleza wajibu wake ipasavyo basi duniani pangekuwa mahali bora sana pa kuishi. nadhani mmnenielewa. Maana yake falfasa ya upendo uisiobagua ni muhimu sana kwa ustawi wa jamii yetu.
Baba Halisi ukasema, hapa watu hawaulizwi dini zao. Kwa hiyo ninyi mnafanya jambo hili kama sehemu ya wajibu wenu kama Kanisa kuwaonyesha wananchi kwamba ibada ni uzalishaji, na huu ni upendo usiobagua, mnawafundisha na kuwalelekeza juu ya misingi yakujiongezea kipato bila kuwabagua, tunawapongeza sana na tunawashukuru kwa mtazamo huu, mtazamo chanya na bora sana, mnapowafanya wananchi waweze kujiongezea kipato maana yake pia mnaisadia serikali", alisema DC Dk. Chuachua.
"Baada ya kusema hayo naomba niwaeleze kwamba Tanzania tunaye Rais tena mwanamke, ametengeneza misingi imara ya kuinua fursa kubwa kwa wananchi hususan kina mama na vijana, fursa ya mikopo ya asilimia 10, mbunge yupo hapa anafahamu fedha zinazotengwa kwa kuwa yeye ni Mjumbe katika Baraza la madiwani", akasema DC Chuachua.
Baada ya kueleza kwa kina mikopo ya Rais Dk. Samia inavyotolewa kwa kinamama, vijana na wenye ulemavu kupitia Halmashauri zote, na kueleza kwamba mikopo hiyo inatolewa kwa upendo usiobagua, DC Chuachua aliliomba Kanisa Halisi kumuombea Rais Dk. Samia ili azidi kulihudumia taifa kwa hekima, busara na upendo usiobagua.
DC Dk. Chuachua alihitimisha hotuba yake kwa kuwaahidi Kanisa Halisi kwamba Serikali itaendelea kuwaonyesha ushirikiano. "mkiona kuna jambo lolote tuambieni tuwasaidie" akasema DC Chuachua.
Baada ya DC kuhitimisha hotuba yake, BABA HALISI alipata nafasi ya kuzungumza, akasema, "Mimi nadhani katika miaka yote tuliyokuja hapa Kigoma, hatujapata upendo namna hii, na zaidi hatujawahi kupata mbunge, tunashukuru sana". kisha akasema;
"Mheshimiwa DC kuhusu yale uliyotaka kuyajua naomba nikujibu hapa hapa, nikikujibu pembeni haitakuwa haki. Kuhusu kwa nini ubini ni Halisi, mimi niliyesimama mbele yako nimepewa uheri wa kupokea Sauti mara nne hapa Kigoma, nilipopokea Sauti kwamba Tanzania ni Taifa Baba, Hapo nipata jina BABA HALISI siyo cheo, jina hili limesajiliwa kisheria, ukienda kwenye Goverment gazete utaona, huyo unayemuona hapo tangu hapo naye ni Mama Halisi, na yule akiwa hapa ni Mtekeleza Sauti Halisi na Waumini wote ni Uzao Halisi, kwa hiyo sote tumekuwa familia moja ndiyo maana ubini wetu ni Halisi", akafafanua BABA HALISI.
Kuhusu vazi jeupe, BABA HALISI akasema; ''Katika kitabu Mwanzo 3 tunasoma kuwa, kitu kikubwa ambacho Adamu alikuwa nacho alinyanyang'anywa", akasema BABA HALISI na kufafanua kuwa vazi alilonyang'anywa Adamu ni ufahamu, na kutaja wengine walivuliwa mavazi kuwa ni Nuhu ambaye alibaki uchi akalaani watoto, "tukivaa hivi ni vazi ili tusilaani watoto", akasema BABA HALISI na kuendelea kutoa mifano zaidi ya waliovuliwa mavazi akiwemo Yesu. "... tumekataa mateso na utumwa wa fikra, ndiyo maana tuna vaa hivi wala siyo fashion".
Baada ya Baba Halisi kumaliza hotuba yake, Mtekeleza Sauti wa mkoa wa Kigoma, Kweli Halisi alifafanua maana ya salamu ya 'Heri' akisema ni kumtakia kuwa baraka kwa Muumba yule unayemsalimia.
Mwishoni, baada ya kufungua mafunzo hayo DC Chuachua alipata fursa ya kukagua bidhaa mbalimbali zilizotengenezwa na wajasiriamali kwenye mafunzo hayo.
Tazama DC Dk. Chuachua akiwa kwenye ufunguzi wa mafunzo hayo.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇