Na Lydia Lugakila, Karagwe
Wazalishaji wa miche na wakulima wa zao la Kahawa katika Kijiji cha Kishoju Kata ya Kihanga Wilayani Karagwe Mkoani Kagera wamempongeza Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa pendekezo la ugawaji bure miche ya kahawa ambayo imekuwa mkombozi kwao.
Mwenyekiti wa wazalishaji hao chini ya Bodi Kahawa Tanzania (TCB) Dionizi Mzee ambaye pia ni mzalishaji wa miche bora ya Kahawa, amesema wanamshukuru Rais Dk. Samia kwa kutenga fungu kwa ajili ya Wakulima hao na kuwawezesha kupata ruzuku ya Miche ya kahawa ambayo kwa sasa imeonekana kama dhahabu usoni mwao.
"Kwa kweli shukrani nyingi ni kwa Rais pia wizara ya kilimo kwa namna walivyosimamia zoezi hilo la ugawaji miche bora ya Kahawa kwetu" alisema Dionizi.
Alisema ugawaji miche huo unasimamiwa na bodi ya Kahawa hivyo pia shukrani zimwendee Mkurugenzi Mkuu wa bodi ya Kahawa kwa ununuzi wa miche hiyo na kusambaza kwa wakulima pia Meneja Mkuu wa bodi ya Kahawa Kanda ya ziwa na Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe kwa usimamizi mzuri wa ugawaji huo.
Alisema kuwa Serikali kila Mwaka inatenga bajeti ya kununua miche Milioni 20 ambapo msimu wa 2024/2025 tayari wameishapewa zabuni ya kuzalisha Miche mingine kwa ajili ya msimu ujao.
Dionizi aliongeza kuwa niaba ya Wakulima hao wanazidi kuipongeza Serikali kwani zao la kahawa lilipanda Bei hadi sh. 5,500 kwa kilo hali iliyoonyesha Serikali ilivyowekeza nguvu nyingi kwa wakulima hao.
Aidha aliipongeza Serikali ya Mkoa wa Kagera kupitia Mkuu wa Mkoa huo Hajat Fatma Mwassa alivyotembelea kitalu chake na kukagua pia kuridhishwa na uzalishaji ambapo pia Mwenge wa Uhuru Mwaka 2024 umezindua kitalu hicho.
Mzalishaji huyo alisema licha ya mradi wa miche bora ya Kahawa pia wanayo miti ya kutunza Mazingira waliyogawiwa bure na Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe ambayo itasaidia wakulima kutunza mazingira, huku wakitaraji kuzalisha zaidi ambapo pua amewaomba wakulima wenzake kuweka juhudi katika uzalishaji.
Kazi hiyo ya kuzalisha miche bora ya kahawa inasimamiwa na Dionizi akishirikiana na Dauson Alphonce,
Martin Mazimba, Bariki Dionizi ambapo pia mradi huu unatoa ajira kwa watu wasiopungua 15, wakiwemo wananchi wa kijiji cha kishoju na vijiji jirani.
Mzalishaji huyo aliongeza kuwa mwezi huu wa Novemba, Serikali kupitia bodi ya Kahawa Tanzania alisambaza miche bora ya kahawa aina Robusta, kutoka kwenye Kitalu chake katika kata 6 ndani ya Halmashauri ya wilaya karagwe ikiwemo kata ya Kihanga, Rugera Ndama, Chonyonyo, Nyakahanga, Chanika huku jumla wa wakulima mia nane (800) wakichukua miche hiyo bure.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇