Na Bashir Nkoromo, Blog ya Taifa ya CCM
Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) imesema, Mfumo mpya wa Kielektroniki wa ununuzi wa umma (NeST) umeiwezesha Serikali ya Rais wa Awamu ya Sita Dk. Samia Suluhu Hassan, kuokoa Ma-trilioni ya fedha katika mwaka wa fedha 2023/2024.
Imesema katika mwaka huo wa fedha wa 2023/2024 PPRA iliweza kuokoa zaidi ya sh. Bilioni 14.94 kupitia ukaguzi, na sh. Trilioni 2.7 kupitia ufuatiliaji kwa njia ya mfumo huo mpya wa kielektroniki wa ununuzi wa umma (NeST), ambao umeongeza uwazi, uwajibikaji na kupunguza mianya ya rushwa.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mkuu wa PPRA Dennis Simba wakati akitoa wasilisho la Utendaji na mafanikio ya Mamlaka hiyo katika kipindi cha miaka mitatu ya Uongozi wa Rais huyo wa Awamu ya Sita Dk. Samia, katika kikao kazi baina yake na Wahariri wa habari kilichoratibiwa na Ofisi ya Msajli wa Hazina na kufanyika leo Novemba 4, 2024 jijini Dar es Salaam.
Simba amesifu mfumo huo wa NeST akisema umeongeza usalama na upatikanaji wa taarifa, pamoja na kuweka mazingira mazuri na wezeshi katika mnyororo wa ununuzi wa umma.
Akieleza mafanikio zaidi yatokanayo na ujenzi wa mfumo wa NeST, Simba amesema ni pamoja na kusajiliwa kwa wazabuni 28,590 katika mfumo huo, kutolewa kwa mikataba ya zabuni 62,267 yenye thamani ya zaidi ya shilingi trilioni 10.2, kuwekwa kwa bajeti ya ununuzi ya zaidi ya shilingi trilioni 38.6 kwenye mfumo huo kama fursa ya wazi kwa ajili ya wazambuni pamoja na kusajiliwa kwa zaidi ya taasisi 21, 851 kwenye mfumo huo.
Aidha amezungumzia pia mgawanyo wa zabuni kwa wazawa na wazabuni wa nje ambapo mpaka kufikia mwisho wa mwaka wa fedha 2023/24, watanzania wamepata asilimia 99.6 ya zabuni huku China ikishika nafasi ya pili ikifuatiwa na Kenya, Afrika Kusini pamoja na Umoja wa Falme za Kiarabu.
Mfumo huo mpya wa kielektroniki wa ununuzi wa umma (NeST), ulianza kutumika Julai 1, 2023 ambapo umekuwa na mafanikio makubwa yakiwepo ya kudhibiti matumizi mabaya ya ofisi, kudhibiti upotevu wa fedha za umma pamoja na kukabiliana na vitembo vya rushwa katika maeneo mbalimbali.
Katika kuhitimisha kikao kazi hicho, pia Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri (TEF) Deodatus Balile alipata nafasi ya kuzungumza, akatumia nafasi hiyo kutoa mwito kwa wamiliki wa vyombo vya habari kufungua akaunti ya mfumo huo wa NeST ili kuweza kupata matangazo, akifafanua kuwa mfumo huo ni njia ya kisasa ya kupata matangazo ambayo yatasaidia kuinua uchumi wa vyombo hivyo vya habari.
Mkurugenzi Mkuu wa PPRA Dennis Simba, akitoa wasilisho la Utendaji na mafanikio ya Mamlaka hiyo katika kipindi cha miaka mitatu ya Uongozi wa Rais wa Awamu ya Sita Dk. Samia Suluhu Hassan, katika kikao kazi baina yake na Wahariri wa habari kilichoratibiwa na Ofisi ya Msajli wa Hazina na kufanyika leo Novemba 4, 2024 jijini Dar es Salaam.
Wasilisho hilo hili hapa👇
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇