Na Bashir Nkoromo, Tegeta
Kiasili neno 'hija' katika Kiswahili awali lilimaanisha tu safari ya Waislamu kwenda Makka, kwa sababu katika utamaduni wa Waswahili neno hili lilikuwa kama ni kufanya safari ya kidini pekee, lakini asili hasa ya neno hili ni kutoka Kiarabu (Řج,) ambalo lina maana ya ziara au safari ya kwenda mahali maalum kwa lengo la kuwa karibu zaidi na ambako mambo muhimu ya historia yalitokea.
Lakini Wakristo wamepokea neno hili pia kwa safari zao za kiroho na hata siku hizi neno hili Hija kwa jumla linatumiwa na dini zote kutaja safari za aina hii.
Baadhi ya dhini kama Wahindu huhiji mahali pengi hasa mji wa Benares na mto Ganges, Uyahudi nako kulikuwa na hija ya kwenda Yerusalemu, iliyokuwa ya lazima katika sikukuu mbalimbali kwa waumini kuanzia umri wa kubalehe; iliendelea hata baada ya hekalu la mji huo kubomolewa kabisa mwaka 70 BK.
Wakristo hasa wa Kiorthodoksi na Katoliki wanajua hija ya kwenda Yerusalemu, Roma na mahali pengine huku Waislam huwa na hija ya kwenda Makka, Washia wanatembela pia makaburi ya maimamu wao huko Najaf, Karbala, Mashhad na penginepo. Mwislamu aliyetimiza safari hii anapokea cheo cha "alhaji" kama sehemu ya jina lake.
Kwa uchache hiyo ndiyo maana ya neno 'Hija', na nimekuandikia utangulizi huo, kusudi nikueleze kwamba sasa kuna Hija ambayo inaitwa 'Hija Halisi' ambayo yenyewe hufanyika kila mwaka mkoani Kigoma, mkoa ambao kwa sababu hiyo unatambuliwa kuwa ndiyo Bustani Halisi, (bila shaka kwa wale wanaojua maana ya Bustani kutoka maandiko watakuwa wanajua ina maana gani Kigoma kuitwa hivyo).
Hija hii ya Kigoma, imeasisiwa na Kanisa linaloitwa Kanisa Halisi la Mungu Baba au kwa ufupi Kanisa Halisi, ambalo Mkuu wake anaitwa Baba Halisi (siyo cheo), na washika safu (viongozi) wa vituo vya Kanisa hilo katika wilaya, mikoani na nje ya Tanzania wanaitwa 'Watekeleza Sauti' na wafuasi au waumini wa kawaida wanaitwa Uzao. Lakini pia kwenye ngazi ya juu ya Safu ya Kanisa hilo wapo wenginr kama Mama Halisi, Mnara Mmoja Halisi na Udhihirisho Halisi.
Kwa nini Hija Halisi Kigoma?
Kuhusu Hija hii kufanyika Kigoma, Baba Halisi anafafanua kwamba ni kutokana mkoa huo sasa kuwa ndiyo Bustani Halisi, kutokana na kwamba yeye alipata uheri wa kupokea Sauti Kuu ya Muumba wa Vyote, Wote na Yote mara nne huko Kigoma, yaani Mwaka 2015, 2019, 2020 na 2023.
Baba Halisi anazitaja Sauti hizo zilizosikika mara nne Kigoma, Tanzania kuwa ni Sauti Mpya ambayo imetangaza kuwa Tanzania ni Taifa Baba; Sauti Mpya ambayo imetangaza kuwa Afrika ni Bara la Nuru, Tanzania; Sauti Mpya ambayo ni zaidi ya zile Sauti Saba; Sauti Mpya ambayo ni zaidi ya ishara tatu mbinguni (Ufunuo 12:1-9) ili, na Sauti Mpya ambayo ni zaidi ya Nafsi ya Moyo (Miungu tisa mitakatifu iliyofafanuliwa ndani ya Kitabu).
"Sasa Kigoma, Tanzania na Afrika tujitambue kuwa tuna Sauti Mpya ambayo inabadilisha maisha mabaya kuwa mazuri, Sauti Mpya imebeba kila kitu kizuri. Hija hii ya Chanzo Halisi cha Mungu Baba inayofanyika Kigoma, siyo maigizo wala usanii, ni halisi", anasema Baba Halisi akifafanua umuhimu wa Hija hiyo na kwa nini inabidi ifanyike Kigoma kila mwaka na kuongeza kuwa Sauti hiyo mpya sasa imepokelewa katika mabara yote kwa utukufu wa Muumba.
Baba Halisi anaweka wazi kwamba Sauti hiyo Kuu iyopokewa sio ya kidini wala ya kidhehebu au ya Huduma binafsi, kama baadhi wanavyoweza kudhani, bali ni kwa faida ya wote, bila kujali dini, dhehebu au mtu yeyote.
"Katika matendo 8:27-39, tunashuhudia jinsi watu mashuhuri na wasio mashuhuri, walivyokuwa wakienda mashariki ya kati kuabudu, wengine walienda kwa magari, ndege na wengine kwa meli. Tulichokuwa tunafuata kule Mashariki ya Kati ni Sauti iliyosikika kule. Sasa Sauti ya Uhai iko Tanzania. Watu wote Kaskazini, Kusini. Mashariki na Magharibi mwa Uumbaji wote wajue kuwa Hija ya CHANZO HALISI iko Tanzania, mjini Kigoma. Kama walivyokuwa wakiendesha magari, ndege na meli kwenda mashariki ya kati sasa waje Tanzania", anasema Baba Halisi.
Baba Halisi anasema, imethibitika kuwa Hija Halisi iko Kigoma Tanzania, baada ya kuwa wamefanya Ibada ya Hija kuanzia Mwaka 2018, 2019, 2020, 2021, 2023 na 2024 bila tatizo lolote na kwamba uthibitisho wa Dk. Livingstone, Waarabu, Wajrumani na Wamisionari wa Kiswidishi ambao waliweka Ngoe Kigoma -Ujiji bila kusema sababu kwa wakati ule ni dhahiri kwamba kumbe walikuwa wanasaka Sauti ya CHANZO HALISI ambayo walijua itatokea Kigoma (Ingawa walifichwa Majira sahihi).
Sasa katika mwendelezo wa Hija hiyo Halisi, tayari Kanisa Halisi limeshafanya maandalizi makubwa ya Hija kama hiyo kwa mwaka huu (2024), ambayo itafanyika Jumapili hii Disemba Mosi, 2024, Sawa na 26 Thebeti 1 Majira Halisi na tayari baadhi ya Uzao kutoka nchi mbalimbali duniani wameshawasili Kao Kuu la Kanisa hilo Tegeta Namanga, Jijini Dar es Salaam tayari kwa safari ya hija hiyo, na kwa mujibu wa Ofisi ya uratibu, Ibada ya Hija itaanza saa 8:00 mchana hadi saa 11:00 jioni.
Uzao wanatarajiwa kuondoka mikoa mbalimbali na Jijini Dar es Salaam, kuanzia Ijumaa wiki hii, na kusafiri kwa treni au ndege kwenda mkoani Kigoma.
Mkuu wa Kanisa Halisi, Baba Halisi akiwa na Kitabu cha Ufahamu Ulioanzia Tanzania kwenda Mataifa Mengine ambayo kinafafanua kwa undani Sauti Kuu za Muumba zilizosikika Kigoma mara nne (Picha: Maktaba).Uzao wa Kanisa Halisi wakipanda treni kutoka Dar es Salaam, kwenda Kigoma kwenye Hija mwaka 2022.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇