Serikali, vyombo vyake na taasisi binafsi zapewa heko kwa mwitikio wa mfano
KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi, amepongeza utayari na mshikamano ulioonyeshwa na Watanzania mara baada ya tukio la kuanguka kwa jengo Kariakoo, akisema kuwa hatua hizo zimeonesha uzalendo na moyo wa udugu uliojengwa ndani ya Taifa letu.
Akizungumza leo, tarehe 17 Novemba 2024, alipotembelea eneo la tukio, Balozi Nchimbi alitoa pole kwa familia za waliopoteza maisha na kuwapa faraja waliojeruhiwa, huku akisisitiza umuhimu wa mshikamano katika nyakati za dharura.
“Kwa namna ya pekee, napenda kutoa pole zangu za dhati kwa familia za wenzetu waliopoteza maisha. Maisha ya kila Mtanzania yana thamani kubwa. Tunaomba Mwenyezi Mungu azilaze roho za marehemu mahali pema peponi,” alisema Balozi Nchimbi.
Aidha, aliwafariji majeruhi akisema:,’Kwa walioumia, walioko hospitali na hata waliotoka, tunawaombea uponaji wa haraka. Mwenyezi Mungu awajalie nguvu na afya njema ili muweze kurejea katika shughuli zenu.”
Shukrani kwa ushirikiano wa haraka
Balozi Nchimbi alitoa shukrani za dhati kwa wananchi wa kawaida waliokuwa mstari wa mbele mara baada ya tukio hilo kutokea.
“Shughuli za uokoaji zilianza mara moja, zikiongozwa na wananchi wa kawaida. Hii inaonesha moyo wa Utanzania wa kweli, ambapo unapomwona mwenzako kwenye shida, unaacha kila kitu na kumsaidia. Nawashukuru kwa moyo huo wa kipekee,” alisisitiza.
Serikali, vyombo vyake na taasisi binafsi zapewa heko
Katika hotuba yake, Balozi Nchimbi aliipongeza Serikali na vyombo vyake, hasa Wizara ya Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), pamoja na timu zake zikiongozwa na Waziri William Lukuvi, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, na taasisi mbalimbali zilizoonesha mshikamano wa dhati katika kuhakikisha maisha yanaokolewa.
“Serikali inafanya kazi yake kwa ufanisi. Hiki ndicho tunachotarajia kutoka kwenye Serikali za CCM—kuwa na uwepo wa karibu wakati wa matatizo. Nawashukuru wote mnaoendelea kuwa hapa kushughulikia hali hii kwa ari kubwa,” alisema.
Aliongeza kuwa juhudi za vyombo vya ulinzi na usalama, taasisi binafsi, na wadau wengine zinapaswa kupongezwa kwa moyo wa kujitolea.
CCM yaahidi ushirikiano zaidi
Balozi Nchimbi alihitimisha hotuba yake kwa kusisitiza kuwa Chama Cha Mapinduzi kinaunga mkono juhudi zote za uokoaji na kiko tayari kutoa usaidizi wowote utakaohitajika.
“Uokoaji huu haupaswi kusimama. Kila maisha yanahesabika. Kama chama, tupo tayari kushirikiana ili kuhakikisha watu zaidi wanaokolewa,” alihitimisha Balozi Nchimbi.
KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi akipokea taarifa kuhusu shughuli ya uokoaji watu inayoendelea katika eneo yalipotokea maafa ya ghorofa kubomoka na kuanguka, Kariakoo, jijini Dar Es Salaam, alipofika hapo kushuhudia shughuli hiyo inavyoendelea, leo tarehe 17 Novemba 2024.Dk. Nchimbi akipata maelezo kutoka kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), William Lukuvi kuhusu maendeleo ya uokoaji. Kushoto ni Mbunge wa Ilala ambaye pia ni Naibu Spika wa Bunge, Mussa Azzan Zungu.Kitengo cha Maafa kiko chini ya wizara hiyo.
Dk. Nchimbi akiwa na Naibu Spika, Mussa Zungu.
Dk Nchimbi akikagua jengo lililoanguka.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇