Jeshi la polisi nchini Tanzania linawashikilia wafanyakazi wanne wa kampuni ya kutoa ya mikopo ya kifedha ya OYA kwa tuhuma za mauaji ya Juma Mfaume kwa kumshambulia sehemu mbalimbali za mwili mume wa mdaiwa wa mkopo.
Taarifa ya Kaimu Kamanda wa Polisi mkoa wa Pwani, Muhudhwari Msuya inasema tukio hilo limetokea Jumatatu katika wilaya ya kipolisi Mlandizi ambapo wafanyakazi hao walifika nyumbani hapo kwa lengo la kudai fedha za marejesho ya mkopo kwa mke wa Mfaume.
Kwa mujibu wa polisi, baada ya kufika nyumbani kwa Mfaume aliwaelekeza kuwa mkewe hakuwepo lakini watuhumiwa hao walilazimisha kuingia ndani kwa nguvu huku wakimshambulia kwa kumchapa na fimbo sehemu mbalimbali za mwili wake na kupelekea kuanguka chini na kupoteza fahamu.
Kamanda Msuya alisema kutokana na hali hiyo watuhumiwa walimbeba Mfaume kwenye gari lao kwaajili ya kumpeleka hospitali lakini alifariki akiwa anapewa matibabu.
Alisema, "Mwili wa marehemu umefanyiwa uchunguzi na daktari kisha kukabidhiwa ndugu kwa taratibu za mazishi.”
Hata hivyo, Jeshi la Polisi linatoa wito kwa makampuni na taasisi za kifedha kufuata taratibu za kisheria katika kudai fedha kutoka kwa wateja wao ili kuepusha usumbufu na madhara yanayoweza kutoka ikiwemo uharibifu wa Mali, kujeruhi na vifo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kampuni ya OYA ya nchini Tanzania, Alpha Peter ameiambia BBC kuwa waliodaiwa kusababisha kifo ni watumishi wa taasisi yao na kwamba kitendo hicho hakikuwa maelekezo ya kampuni hiyo.
Peter alisema, “Kilichofanyika, si maelekezo wala utaratibu wa taasisi yetu pale tunapoenda kudai marejesho kwa wateja wetu. Kwasasa tuko karibu na familia kuifariji lakini pia tunaendelea kutoa ushirikiano kwa jeshi la Polisi wakati huu wakiendelea na uchunguzi wa tukio hilo.”
Kampuni ya OYA ya nchini Tanzania ilisajiliwa mwaka 2020 na kwasasa inatoa huduma kwenye mikoa nane.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇