Diwani wa Kata ya Mondo na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Chemba Mkoa wa Dodoma Mh.Said Sambala amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuipatia Kata ya Mondo fedha nyingi za miradi ya maendeleo hususan katika ujenzi wa miundombinu ya huduma za jamii katika kata hiyo.
Ameitaja mradi hiyo kuwa ni pamoja na sekta ya afya, elimu, maji na mingineyo. Hivyo, Mh. Sambala amewataka wananchi wa Kata ya Mondo kuunga mkono juhudi za Mheshimiwa Rais kwa kuhimiza watoto kwenda shuleni bila kukosa.
Aidha, amewataka wazazi kuwapatia watoto wao mahitaji ya msingi kikiwemo chakula. Vile vile ameitaja jamii kujenga utamaduni wa kuwa walinzi wa miundombinu hiyo ili itumike kwa vizazi vingi vijavyo.
" Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa zaidi ya Shilingi Bilioni Moja na Milioni Miatatu kwenye Kata yetu ya Mondo kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya huduma za jamii ikiwemo elimu" alisema Mheshimiwa Sambala na kuongeza
...Vile vile ametuongeza Shilingi Milioni Mia Moja kwa ajili ya ujenzi wa Zahanati ya Kijiji cha Waida. Tunajukumu la kuunga mkono juhudi hizi za Mheshimiwa Rais kwa kutimiza wajibu wetu wa malezi bora kwa watoto wetu pamoja na kuwa walinzi wa miundombinu ya miradi hii ili itumiwe na vizazi vingi vijavyo."
Katika kutatua changamoto zinazoikabili shule hiyo ikiwemo ya utoro Mheshimiwa Sambala amemshauri Mwenyekiti wa Bodi ya Shule hiyo Bwana Thomas Chorray kuitisha kikao haraka ili kujadili changamoto hizo na kuzitafutia ufumbuzi. "Nadhani kuna haja ya Bodi ya Shule tukutane haraka kuzipatia ufumbuzi changamoto za shule hii ikiwemo changamoto sugu ya utoro.
Utoro haukubaliki katika zama hizi. Kuwepo kwa utoro tafsiri yake ni moja tu kwamba mahala fulani jamii yetu hatuko sawa."
Kauli hii ameitoa kufuatia takwimu za wahitimu wa mwaka huu kuonesha karibu nusu yao yaani wanafunzi 103 kati yao wavulana 36 na wasichana 67 wameshindwa kuhitimu kwa sababu ya utoro ikilinganishwa na wanafunzi 112 kati yao wavulana 54 na wasichana 68 waliohitimu leo.
Haya yamejiiri Jumamosi Oktoba 12, 2024 alipokuwa anatoa salamu za Serikali wakati wa mahafali ya 27 ya Shule ya Sekondari Mondo iliyoko Kata ya Mondo Halmashauri ya Wilaya ya Chemba mkoa wa Dodoma akiwa Mgeni Maalumu.
Katika hatua nyingine Mheshimiwa Sambala amewataka wahitimu wa miaka ya nyuma kuungana katika kutatua changamoto za shule hii. "
Mheshimiwa Mgeni Rasmi mimi ni mmoja wa wahitimu wa shule hii pamoja na wenzangu Mkuu wa Shule Msaidizi na Mjumbe mmoja wa Bodi ya Shule.
Ninaaomba kutumia fursa hii kuwasihi wenzangu tuliopo ndani ya Kata hii, na maeneo mengine ndani na nje ya mkoa wa Dodoma kuunganisha nguvu zetu na kuanzisha utaratibu maalumu wa kurudisha fadhila kwa shule yetu. Kupitia njia hii ni dhahiri tutapunguza changamoto zinazoikabili shule yetu pendwa" alisema Sambala.
Vile vile Mh. Sambala ametumia fursa hiyo kuwahimiza wananchi wa Kata ya Mondo na Wilaya ya Chemba kwa ujumla kujitokeza kwenye zoezi la kujiandikisha kwenye daftari la wakazi ili kupata sifa ya kushiriki uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika Novemba 27 mwaka huu. "Ninawaomba wananchi wa Kata ya Mondo na Wilaya ya Chemba kwa ujumla tuhimizane kujiandikisha kwenye daftari la wakazi ilitupate sifa ya kushiriki uchaguzi huu."
Mgeni Rasmi katika mahafali haya yaliyohudhuriwa na mamia ya wananchi alikuwa Profesa Fadhil Hamza Mgumia kutoka Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini aliyemwakilisha Mkuu wa Chuo Profesa Hozen Mayaya.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Chemba Mkoa wa Dodoma Mh.Said Sambala
Baadhi ya wahitimu.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇