LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Oct 18, 2024

MUFTI WA TANZANIA AHIMIZA KILA AMBAYE HAJAJIANDIKISHA DAFTARI LA WAPIGA KURA SERIKALI ZA MITAA KUHAKIKISHA ANAJIANDIKISHA NDANI YA SIKU TATU ZILIZISALIA

Korogwe, Tanga

Mufti Sheikh Mkuu wa Tanzania Alhaj Dk. Abubakar Zubeiry bin Ali amehimiza kila mwananchi anayestaili nchini kote asikose kujiandikisha katika Daftari la Wapiga Kura wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa ili waweze kutimiza haki yake ya kikatiba ya kuwachagua viongozi wanaowataka wa Serikali za Mitaa katika maeneo wanakoishi. 


Mufti Sheikh Mkuu ametoa mwito huo leo Oktoba 18, 2024,  baada ya kujiandikisha kwenye daftari hilo katika mtaa wa Kwamndolwa, Kata ya Kwamndolwa katika wilaya ya Korogwe mkoani Tanga. 


Amewahimiza vijana na watu wazima, wake kwa waume wafanye juu chini watumie siku tatu zilizosalia kwenda vituoni na kujiandikisha kabla zoezi halijafungwa rasmi keshokutwa, Jumapili Agosti 20, 2024.


"Siku kumi sio nyingi na wengi wetu katika zoezi kama hili tumezoea kujitokeza dakika za mwishoni na kujikuta tunakumbana na usumbufu wa foleni usio wa lazima kwa kuwa wengi tulichelewa kujitokeza.


Natoa mwito kwa wananchi wote ambao bado hamjajiandikisha shime mjitokeze leo, kesho na keshokutwa ambayo ndiyo siku ya mwisho", amesema Mufti.


Amewapongeza ambao tayari wameshajiandikisha, na kusisitiza kwamba zoezi hilo halihusiani na lile la Uchaguzi Mkuu ambapo kunakuwa na kadi za mpiga kura.


"Zoezi hili halihusiani na la uchaguzi mkuu hivyo usiache kujiandikisha kwa kuwa una kadi ya mpiga kura. Ni vitu viwili tofauti na zoezi hili lazima ukajiandikishe kivyake", alisema.


Uandikishwaji katika Daftari la Mpiga Kura la Uchaguzi wa Serikali za Mitaa umeanza rasmi Oktoba 11, 2024 na utaendelea hadi Jumapili Oktoba 20, 2024. 


Aidha, kwa mamlaka aliyonayo chini ya Kifungu cha 3 cha Sheria ya Sikukuu za Kitaifa (Public Holidays Act) Sura 35, Rais Dkt. Samia suluhu Hassanametangaza tarehe 27 Novemba, 2024 kuwa siku ya mapumziko ili kuwaruhusu wananchi kushiriki Uchaguzi wa Serikali za Mitaa.


Mufti Sheikh Mkuu wa Tanzania, akijiandikisha kwenye daftari hilo katika mtaa wa Kwamndolwa, Kata ya Kwamndolwa katika wilaya ya Korogwe mkoani Tanga, leo Oktoba 18, 2024

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages